Na Khamisuu Abdallah
MWAKILISHI wa jimbo la Amani, Fatma Mbarouk Said amezitaka jumuiya za maendeleo nchini kuzidisha mashirikiano katika utendaji wa kazi zao ili waweze kufikia maelengo waliyoyakusudia.
Akifungua mafunzo ya siku tano ya utayarishaji wa mpango na mikakati kwa Jumuiya maendeleo ya vijana mayatima na watu wenye mahitaji maalum ‘ODIYAS’ ya jimbo la Amani huko katika skuli ya Elimu Mbadala
Rahaleo.
Mwakilishi huyo alisema mashirikiano mazuri kwa wanajumuiya hao ndio njia pekee itakayoweza kuwajengea upendo kwa kufanyakazi kwa bidii na kujiletea maendeleo kwa haraka.
Aidha alisema jimbo la Amani linajivunia kwa kuwaona wananchi wake wameweza kubuni mbinu mbali mbali na kuanzisha Jumuiya katika jimbo lao ambayo itakayoweza kuwasaidia katika kukabiliana na maisha yao na
jamii kwa ujumla.
"Jimbo la Amani pamoja na viongozi tumepata faraja sana kwa wananchi wetu kuwaona wanashirikiana na wanabuni mbinu mbali mbali ambazo zinaweza kukusaidieni katika maisha yenu ya kila siku na jamii kwa
ujumla”, alisema Mwakilishi huyo.
Aliwataka wanajumuiya hao kuwa waaminifu hasa katika matumizi ya fedha wanazopatiwa sambamba na kuweka kumbukumbu vyema pamoja na kutolewa kwa ripoti za matumizi.
Alifahamisha kuwa bila ya umakini katika matumizi ya fedha, jumuia hiyo haitakwenda na kutaka uadilifu ufanyike kwa kila mwanachama kupatiwa haki sawa na mwengine bila ya upendeleo.
Nae mmoja wa wanachama wa jumuiya hiyo Mwanaweza Hassan Omar, akisoma risala kwa niaba ya wanajumuiya wenzake alisema jumuiya yao inakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo ukosefu wa ofisi ya kudumu, kukosa vifaa vya kutendea kazi kama vile kompyuta, meza na viti.
Aidha walimuomba mwakilishi huyo kuwatizama kwa moyo wa huruma kuwatatulia matatizo yao ili waweze kujiletea maendeleo na kujikwamua na umasikini kwa kujiajiri wenyewe bila kusubiri ajira Serikalini.
Jumuiya ya maendeleo ya vijana, mayatima na watu wenye mahitaji maalum ‘ODIYAS’ inajishuhulisha na kazi za Mazingira na kutoa elimu ya Afya ambapo imeanzishwa Febuari 7, mwaka jana ikiwa na wanachama 21 Wanaume 11 na Wanawake 10.
No comments:
Post a Comment