
Baraza ya wazee wa wanafunzi waliofutiwa mitihani Zanzibar wamekutana na waandishi wa habari leo hii, kutoka kushoto ni Bw. Juma Simba, Bi Najma Mustapha Giga, Mwenyekiti Bw. Ali Hassan na Saleh Mohammed
Yataka Mitihani yote irudiwe kwani ilivujaNa Zahira Bilali Said, Maelezo
Kamati ya Wazee wa Wanafunzi walofutiwa matokeo yao ya Mitihani wa Kidato cha Nne Zanzibar imesema haikubaliani na uamuzi wa kuwafutia matokeo wanafunzi wale tu walioshutumiwa kufanya udanganyifu badala yake imetaka Wanafunzi wote kufutiwa matokeo yote kwa vile mitihani ilivuja.
Katika taarifa yao iliyotolewa kwa Vyombo vya Habari Kamati hiyo imesema Baraza la Mitihani linapaswa kuurejea Mtihani huo kwa Zanzibar na Tanzania Bara kwani kufanya hivyo kutapunguza malalamiko na dhana iliyoibuaka ya tatizo hilo kuwa kasoro nyengine mpya ya Muungano
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Ali Hassan Khamis amesema ikiwa Baraza la Mitihani NECTA litaona ugumu kuurudia mtihani basi libainishe kwa walimu wao makosa ya kila mwanafunzi kwa wale waliofutiwa na wale wenye mashaka na matokeo yao.
Ali amesema Wazanzibari wameanza kupoteza imani na Baraza hilo hasa baada ya kutoa matokeo kwa baadhi ya wanafunzi ambao tayari walishafutiwa matokeo yao hapo kabla na kupewa ufaulu wa Daraja la Nne na Daraja Ziro
Akitaja mapungufu ambayo yalijitokeza katika Baraza hilo amesema kuna baadhi ya wanafunzi walifanya mitihani ya masomo ya Sanaa lakini wakapewa matokeo ya masomo ya Sayansi na baadhi yao walifanya masomo ya Sayansi na kupewa matokeo ya Sanaa.
Aidha amesema Baraza hilo limekosa umakini katika kufanya kazi zake kwani kuna baadhi ya wanafunzi wameandikiwa "Absent" kwa maana hawakufanya mtihani lakini kiukweli wanafunzi hao walifanya mitihani yao kikamilifu.
Kwa upande wake Mkurungezi Mtendaji wa Jumuiya ya Kuzuia,Kukinga na Kuondosha Maafa na Majanga Zanzibar Najma Murtaza Giga amelishauri Baraza la Mitihani kuukubali ukweli kwamba mitihani ilivuja na hivyo waondoshe adhabu waliyoitoa kwa wanafunzi hasa ikizingatiwa muhusika wa kwanza wa kosa hajajulikana
Najma amesema ikiwa Baraza la Mitihani halitozingatia taarifa yao na kuitolea jibu muafaka Jumuiya italazimika kushirikiana na Kamati ya Wazazi kupeleka ombi lao Mahakama Kuu ya Zanzibar Vuga kwa kutumia hoja za msingi za kisheria ili Mahakama hiyo iweze kutoa tamko la kumtaka Katibu Mtenfdaji wa Baraza Joyce Ndalichako na Baraza lake kufuata vizuri kanuni na sheria za Baraza hilo
Aidha ameongeza kuwa Jumuiya yao imesikitishwa na baadhi ya wanafunzi ambao wamevunja sheria na kutumia njia za udanganyifu wa aina mbali mbali katika kujibu mitihani yao
Kwa mujibu wa Takwimu ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar wanafunzi wasiopungua 13,000 wa shule za Serikali na binafsi walifanya mtihni ambapo wanafunzi 60 tu walibahatika kufaulu daraja la Mwanzo.
Wanafunzi 160 walibahatika daraja la Pili, wanafunzi 776 walifaulu Daraja la Tatu, Wanafunzi 8150 walipata Daraja la Nne, Wanafunzi 2948 walifeli kabisa ambapo kwa upande wa walioufutiwa matokeo ni wanafunzi wasiopungua 1000
No comments:
Post a Comment