KAMATI ya kudumu ya Baraza la Wawakilishi ya Habari, Utalii, Mifugo na Uwezeshaji, imewataka watendaji wa taasisi za Serikali kupanga mipango kwa umakini ili iweze kuleta maendeleo kwa wananchi na kuifanya Serikali kuonekana inawatumikia wananchi na kuiondoshea lawama.
Maelekezo hayo yametolewa jana na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Asha Bakari Makame, katika kikao cha kupokea taarifa kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, kilichofanyika ukumbi mdogo wa Baraza la Wawakilishi uliopo Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Alisema Baraza la Wawakilishi hivi sasa limekuwa likifanya kazi zake kwa maslahi ya wananchi na haitakuwa vyema watendaji kulazimisha mambo ambayo yatasababisha Serikali kupata lawama kutoka kwa wananchi.
Kauli ya Mwenyekiti huyo imekuja alipokuwa akitoa maelezo kuhusiana na hatua za kuibadili sheria ya Kamisheni ya Utalii Zanzibar, ambapo baadhi ya vipengele vyake vimebadilishwa ili kutoa nafasi ya ushirikishaji jamii kabla ya kuanzisha mradi badala ya mfumo wa sasa usiowahusisha, ambao unachangia kupingwa kwa miradi hiyo na wananchi.
Suala jengine ambalo Kamati hiyo, ililitilia mashaka ni kuonekana kwamba sheria hiyo inaelekea kurudisha mfumo wa zamani wa Kamisheni hiyo, ambao sheria yake ilifanyiwa marekebisho karibuni hasa katika masuala ya uongozi.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo, walihoji ni kwanini warejeshe utaratibu huo ambao ulionekana utendaji wake kuwa na matatizo na wamesema hawaoni sababu kurekebishwa kwa sheria hiyo ndani ya kipindi kifupi.
Kuhusu vipengele vinavyohusu sheria ya kuwashirikisha watu ndani ya sheria hiyo Wajumbe wa kamati hiyo walieleza kuingiwa na wasiwasi mapendekezo yake kama yaliwashirikisha wananchi kwa kutambua nini wanachotaka wafanyiwe ndani ya sheria hiyo na huenda yakawa ni mawazo ya wataalamu pekee.
Wajumbe hao walieleza haja ya mabadiliko hayo kuzingatia maoni ya wananchi, kabla ya kukamilishwa taratibu za kiserikali.
Akitoa maelezo yake Mwenyekiti huyo alisema haoni mantiki ya kurudishwa kwa mfumo huo na kushauri watendaji wa Wizara hiyo wanahitaji kuwa makini ili wasitoe mwanya kwa wananchi kumuingiza kiongozi wa nchi lawamai.
Alisema Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanachohitaji kupelekewa ni mambo yatayoweza kuwapa ushawishi Wajumbe wa Baraza hilo kwa kuangalia zaidi maslahi ya wananchi ili kuiepusha serikali kuingia matatani.
Aidha Mwenyekiti huyo aliishauri Wizara hiyo na taasisi nyengine za Serikali kutokubali kupokea wala kutoa maamuzi kwa njia yam domo, bali wafuate utaratibu wa maandishi ambao ndio mufaka serikalini.
Katika kuisaidia Tume ya Utangazaji Zanzibar kuweza kutoa elimu ya kuanzia kwa wananchi kuhusiana na uhamaji kutoka mfumo wa mawasiliano ya Analogi kwenda digitali, Kamati hiyo imeagiza kuwa ni lazima taasisi zilizo chini ya Wizara ikiwemo Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) kulipa deni inalodaiwa na Tume hiyo ambalo limeelezwa kufikia shilingi milioni 300 kwa ajili ya leseni ya utoaji wa mawimbi ya utangazaji.
Aidha Tume ya Utangazaji imeeleza kwamba inakwama kufanya shughuli zake kutokana na kutolipwa na taasisi nyingi kama vile vyombo vya habari binafsi.
Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mohammed Said Dimwa alisema ipo haja ya Baraza la Wawakilishi kuunda Tume ambayo itaweza kuchunguza baadhi ya mikataba inayofungwa bila ya kuihusisha wizara husika.
Naye Mjumbe wa Kamati hiyo, Ali Mzee Ali, alisema ipo haja kwa wizara hiyo ikafanya ziara itayoweza kuyatambua maeneo ya kihistoria kutokana na hivi sasa kuanza kupotea uhalisia wake kutokana na kuwepo uvamiizi mkubwa wa ardhi.
Akijibu baadhi ya hoja hizo, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Ali Mwimyikai, alisema wizara hiyo itahakikisha katika kulitatua tatizo la deni hilo katika kipindi kijacho cha bajeti.
Alisema tatizo lililojitokeza ni kutokana na wakati wa maandalizi ya bajeti za mwakani kutakiwa na Wizara husika kutobadili bajeti yao kwa kulazimishwa kutumia ukomo wa bajeti ambao ni mdogo ikilinganishwa na mahitaji halisi.
Alisema Wizara hiyo katika bajeti iliopita wizara hiyo imeweza kutekeleza malengo yake kwa asilimia 70, huku kukiwepo mengine ambayo hayajatekelezwa kutokana na kutopata bajeti ya kutosha katika bajeti ambayo hutengewa Wizara kwa taasisi zake.
Alisema hadi sasa wizara hiyo imeingiziwa shilingi 2,737,045,841.50 huku ikiwa imekusanya shilingi 164,069,440 kutoa mwezi Julai hadi kufikia Disemba mwaka jana.
Alisema wizara hiyo tayari hivi sasa imo katika kutekeleza changamoto mbali mbali ikiwapamoja na kuliimarisha shirika la Magazeti ya Serikali wachapishaji wa Gazeti la Zanzibar Leo na Zanzibar Leo Jumapili ili liongeze ubora.
Aidha kuliimarisha shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) kusimamia mabadiliko ya mfumo wa matangazo kuingia katika digitali, kukiimarisha Chuo cha Utalii, Shirikala Utalii, Chuo Cha Habari Zanzibar, Idara ya Utamaduni na Michezo.
Kamati hiyo ilipata nafasi ya kutembelea maeneo mbali mbali yanayohusiana na kazi za Wizara hiyo ikiwemo Hifadhi ya Msitu wa Jozani, Eneo linalowekwa mtambo na mnara wa masafa ya kati wa Redi Zanzibar, ambao umehamishwa kutoka Chumbuni na kupelekwa Bungi, Makumbusho ya Kasri, Forodhani na Ofisi za Tume ya Utangazaji Zanzibar.
No comments:
Post a Comment