Habari za Punde

Dk. Shein Awatangazia Neema Wazee.

Ni kutekeleza ahadi, ilani, azma ya mapinduzi

Na Mwantanga Ame

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amewakikishia uhakika wa kupata huduma zote muhimu wazee wanaoishi katika vituo vya wazee Unguja na Pemba, ikiwa ni kuendeleza malengo ya Mapinduzi ya Zanzibar na ustawi wa jamii nchini.

Katika kufanikisha ahadi hiyo ambayo ameitoa wakati akinadi ilani ya uchaguzi ya CCM alipokuwa akiomba kura kuchaguliwa kuwa Rais na kuisisitiza alipozindua Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, Dk. Shein ameeleza mikakati kadhaa ambayo imepangwa na Serikali yake kufikia lengo hilo muhimu, ambalo limekuwa likitekeleza tokea awamu ya kwanza ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuendelzwa hadi awamu hii ya saba.

Akizungumza na wazee wanaotunzwa katika nyumba za Sebleni mjini hapa, Dk. Shein alieleza kwenye mpango huo wazee wataimarishiwa huduma za chakula kwa kuwahakikishia kuwa watakula kama wanavyokula watu wengine katika nyumba nyengine nchini, pamoja na kuwekewa daktari maalum na muuguzi ili kuwapatia huduma za afya hapo hapo kwenye makaazi yao.

Mbali ya kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa ahadi alizotoa Dk. Shein, alisema utunzaji wa wazee wa Unguja na Pemba ni muendelezo wa mambo mazuri yaliyofanywa na Awamu zilizopita katika kufanikisha malengo ya Mapinduzi ya Zanzibar, kama yalivyoanza kutekelezwa na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, marehemu Mzee Abeid Amani Karume.

Akiwahutubia wazee hao, Dk. Shein, alisema serikali kuanzia sasa inaanza kutekeleza ahadi hiyo mara moja, kwa kuandaa mpango utaowafanya wazee 63 wanaoishi katika nyumba hiyo, wanakuwa na chakula cha uhakika kwa kupatiwa milo mitatu kwa siku.

Matunzo mingine, Dk. Shein, aliahidi kuwapatiwa ni kuzijenga nyumba tano zilizomo katika makaazi ya wazee hao huku ikihakikisha nyumba hizo zinakuwa na sehemu bora na za uhakika za kulala.

Eneo jengine, aliloahidi kulifanyia kazi ni pamoja na kuwajengea jiko la kisasa ambalo litakaloweza kutumia bila ya matatizo huku akiwekwa mtu maalum atae hudumia ili kuwaepusha kutokea matatizo ya kuungua moto, pamoja na kuitengeneza shemu ya kulia na kupumzika, ambayo aliagiza kupewa kipaumbele katika mipango ya wizara husika.

Aidha, Dk. Shein, aliwaeleza wazee hao kuanzia sasa eneo lao litalindwa na ulinzi wa uhakika Kikosi cha JKU, ikiwa ni hatua ya kuimarisha ulinzi wa mali za wazee wanaoishi nyumba hizo.

Dk. Shein, alieleza huduma ya umeme nayo itaimarishwa katika nyumba hizo ikiwa pamoja na kusimamia upatikanaji wa huduma ya maji ambapo tayari visima vimeshachimbwa na taasisi husika zimemuahidi kufanya hivyo ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.

Yote hayo ambayo yamepangwa kufanyika kwa wazee wa Unguja, pia yatatekelezwa kisiwani Pemba, ikiwa ni kuendeleza dhamira ya malengo ya ASP, Sera ya serikali na Ilani ya Chama cha Mapinduzi, inayotaka wazee kupewa huduma bora kwa usawa katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Alisema ingawa kuna mabadiliko ya viongozi katika mfumo wa serikali, lakini ukweli ni kwamba viongozi wote walioshika madaraka wameiendeleza dhamira ya malengo ya mapinduzi ya 1964 na serikali ya awamu ya saba itahakikisha hayo inayatekeleza kabla ya kufikia 2015.

Alisema wakati serikali inashughulikia maisha yao, lakini suala kubwa ambalo wazee hao watapaswa kuwa nalo, ni kutulia katika makaazi yao na sio kuranda kutafuta maisha.

“Serikali yenu imeamua kushughulikia maisha yenu kuanzia sasa mtulie, kama mtu anatembea basi iwe kwa kunyoosha miguu sio kutafuta maisha, kama watu wanakula mara tatu basi nanyi mtakula mara tatu hii milo ya kawaida tutaweka utaratibu kama zamani yaliwezekana kwanini leo tusiweze”, alisisitiza Dk.Shein.

Akiendelea alisema yeye binafsi anafurahia kuona wazee wanalala katika sehemu nzuri na serikali hashindwi kufanya hivyo, kwani anaamini uwezekano huo upo kulingana na matumizi ya fedha za serikali.

Alisema fedha zinazotolewa kwa ajili ya posho la wazee la shilingi 40,000 ni kweli halitoshi kwa ajili ya kuendesha maisha yao, na ndio maana serikali imeamua kuwaandalia mpango huo utaowasaidia kukabiliana na ukali wa maisha hasa chakula na mambo mengine muhimu, huku ikilifanyia mabadiliko kila hali itaporuhusu.
Dk. Shein, aliwataka watendaji katika Wizara ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana Wanawake na Watoto, kuhakikisha wanasimamia vyema utekelezaji wa mpango huo kwa kuzingatia kipaumbele eneo la Wazee katika bajeti yao.

Awali Dk. Shein alikagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba iliyoungua moto mwaka jana, ambapo aliridhishwa na maendeleo yake.

Dk.Shein, alizishukuru taasisi binafsi ambazo zimekuwa zikijitolea kuwasaidia wazee wa nyumba hizo ukiwemo Umoja wa Wastaafu wa Zanzibar, ambao ulijitolea kuwachimbia visima wazee hao.

Mapema Waziri wa Wizara ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana Wanawake na Watoto, Zainab Omar Mohammed, alieleza Wizara yake inahitaji kuona serikali inawasaidia kupata daktari ataekuwa wa kudumu katika nyumba hizo na ulinzi wa vikosi na gari kwa ajili ya kuwahudumia wazee hao.

Nae Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Fatma Gharib Bilal, akisoma taarifa ya Wizara hiyo alisema ujenzi wa nyumba iliyoungua hivi sasa matengenezo yake yako mbioni kukamilika ambapo zaidi ya shilingi milioni 163 zimeshatumika kukamilisha ujenzi huo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.