Habari za Punde

Duni: Mnazimmoja Kimbilio la Wanyonge

Azindua maabara, kitengo cha meno
Saratani, moyo, figo kuchunguzwa

Na Salum Vuai, Maelezo

TATIZO la wananchi wa Zanzibar wanaosumbuliwa na magonjwa mbalimbali yasiyokuwa ya kuambukizwa kufuata vipimo nje ya visiwa hivi, sasa limefikia kikomo.

Nafuu hiyo imepatikana kufuatia kukamilika kwa matengenezo makubwa yaliyokuwa yakifanywa kwenye maabara ya hospitali kuu ya Mnazimmoja, sambamba na kitengo cha meno, na hatimaye kuzinduliwa hapo jana.


Uzinduzi huo ulifanyika jana ambapo waziri wa Afya Juma Duni Haji aliyekuwa mgeni rasmi, alieleza kuwa hiyo ni hatua kubwa kuelekea kuipandisha hadhi hospitali hiyo na kuwa ya rufaa kama serikali ilivyoagiza.

Duni alisema ili hospitali iweze kuwa ya rufaa, haitoshi kuwa na majengo mazuri pekee, bali kuna mambo manne ya msingi yanayohitajika ili iwe na sifa hiyo.

Alivitaja vigezo hivyo kuwa ni huduma bora, vifaa kamili na vya kisasa, kuwafikia watu wote pamoja na gharama nafuu za matibabu.

Hata hivyo, alieleza kuwa, mafanikio hayo hayawezi kupatikana kwa kipindi kifupi, lakini hatua iliyofikiwa sasa, ni ishara kuwa hospitali hiyo iko mbioni kufika mfundani na kupata hadhi ya rufaa ili iweze kuwanufaisha wananchi wa Zanzibar.

Alisema hiyo ni faraja kubwa kwani awali ni magonjwa 30 tu ndiyo yaliyokuwa yakiwezekana kufanyiwa uchunguzi hapa nchini, na kufuatia kukamilika kwa maabara ya hospitali kuu ya Mnazimmoja, idadi hiyo sasa imefikia 60.

"Hospitali ya Mnazimmoja ndio uso wa wizara yetu, pamoja na kuwepo hospitali nyingi nchini, lakini bado hii ndio kimbilio la wengi na mategemeo yao kwa ajili ya kupata huduma za kiafya”, alifafanua.

Kwa upande wa maslahi ya madaktari na wauguzi, aliwahakikishia kuwa utaratibu wa kuyarekebisha ili angalau waweze kupata haki zao za msingi unafanyiwa kazi na Wizara inayohusika na utumishi wa umma, na kuwataka waongeze bidii na kufanya kazi kwa uzalendo wakijua kuwa huduma zao ni muhimu kwa kuokoa maisha ya wananchi.

Waziri huyo aliwashukuru wafadhili waliosaidia kuzitengeneza idara hizo za maabara pamoja na kitengo cha meno, na kuvipatia vifaa vya kisasa ili kuwaondoshea usumbufu wananchi wa Zanzibar.

Mapema, Mkurugenzi wa hospitali hiyo Dk. Jamala Adam Taibu, alisema matengenezo ya maabara yamefadhiliwa na shirika la kimataifa ICAP la Marekani kwa gharama ya shilingi milioni 500, na kitengo cha meno kimefadhiliwa na shirika la MCW kwa gharama ya zaidi ya dola 200,000.

Kwa upande wa maradhi ya meno, alisema mbali na vifaa na huduma za kisasa za kung'oa, pia kutakuwa na matibabu tafauti ya kuhifadhi na kuyaimarisha meno ili kuyaweka katika mazingira ya kutokuoza na kuuma.

Wakizungmza katika hafla hiyo, mwakilishi wa ICAP, Ayela Zeudi na Marion Beckman kutoka MCW, walielezea dhamira yao ya kuendelea kutoa misaada mbalimbali ya kiafya kwa Zanzibar na Tanzania kwa jumla.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.