Na Mwantanga Ame
SPIKA wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, amewataka viongozi kuacha kumiliki vifaa vinavyotumika kuendeshea uvuvi haramu katika bahari ya Zanzibar.
Kificho alisema hayo jana alipokuwa akifungua semina ya siku moja iliyowakutanisha kwa pamoja wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Wabunge, Wakuu wa Mikoa na wavuvi.
Alisema vitendo vya uvuvi haramu vimekuwa vikiongezeka katika visiwa vya Unguja na Pemba, na haitakuwa vyema ikiwa viongozi wataendelea kutaajwa kuhusika kutokana na baadhi yao kumiliki vifaa vua uvuvi.
Alisema serikali baada ya kupisha sheria ya kusimamia uvuvi, wavuvi watalazimika kuacha kujishungulisha na vitendo vya uvuvi haramu, kwani vimeanza kuhatarisha kutoweka kwa rasilimali za baharini ikiwemo kuharibu matumbawe ambayo ni muhimu kwa mazalia ya samaki.
“Kulinda rasilimali za baharini lengo lake sio kumkomoa mvuvi asiweze kuvua samaki baharini, bali lengo kuvuna rasilimali za baharini kwa faida ya vizazi vijavyo”, alisema Spika Kificho.
Spika Kificho, alisema haitakuwa busara na haikubaliki kwa kwa wavuvi kujali maslahi ya kupata kipato kikubwa cha mavuno ya samaki, huku wakiharibu matumbawe na rasilimali nyengine kutokana na kutumia vifaa vya uvuvi haramu.
Alisema jitihada za kuzuia uvuvi haramu zisipochukuliwa inaweza kuwa janga kwani takwimu zinaonesha kuwa kuna wavuvi 34,571 ambao kwa bahati mbaya wanatumia maji katika kina cha kawaida ambacho hufikiwa na wavuvi wengi.
Mapema Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Said Ali Mbarouk alikiri kuwepo kwa kasi ya uvuvi haramu katika maeneo mbali mbali ya pwani ya mwambao wa visiwa vya Unguja na Pemba hali inayoibua mivutano kati ya wavuvi na watendaji wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi.
“Ni kweli mivutano imeibuka kati ya wavuvi katika shehia za Unguija na Pemba, pamoja na watendaji wa Idara ya Uvuvi zaidi pale wanapofuatilia shunguli za uvuvi na kupambana na wavuvi wanaonedesha uvuvi haramu”,alisema.
Alisema hivi sasa kumekuwa na mambo ya kusikitisha kwa baadhi ya watu kushindwa kutunza raslimali za nchi ziliopo kwa kufanya uharibifu wa makusudi.
Waziri huyo alisema tayari wizara hiyo imeshaandaa mipango mbali mbali ya kukabiliana na vitendo hivyo kwa kuwahusisha viongozi wa taasisi.
Nae Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, amesema kuwa suala la uvuvi haramu hivi sasa limekuwa ni kero ingawa Wizara hiyo imeweza kuchukua hatua mbali mbali za kuwapatia elimu jamii ili kupiga vita vitendo hivyo.
Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi Zanzibar Mussa Aboud Jumbe, akitoa mada juu ya uvuvi haramu alisema tatizo hilo linakuwa kutokana na kasi ya vijana kuamua kuingia kufanya kazi za uvuvi kama ndio ajira waliyoichagua.
No comments:
Post a Comment