Habari za Punde

Maalim Seif Akutana na Viongozi wa Vyama vya Michezo

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na viongozi wa vyama vya michezo Zanzibar, kwenye mkutano na wadau hao ulifanyika Baraza la Wawakilishi la zamani. Kulia ni Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Zanzibar, Sharifa Khamis. 


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiwa na viongozi wa vyama vya michezo Zanzibar, kwenye mkutano na wadau hao ulifanyika Baraza la Wawakilishi la zamani 
(Picha, Salmin Said, OMKR). 

Na Hassan Hamad OMKR

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, ameiagiza Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar kuwasiliana na Wizara inayohusiana na mambo ya Michezo Tanzania Bara ili kujadiliana juu ya namna ya kutatua changamoto za kimichezo ya kitaifa na kimataifa.

Maalim Seif ametoa agizo hilo baada ya kukutana na viongozi wa vyama vya michezo Zanzibar katika mkutano uliofanyika baraza la wawakilishi la zamani Mnazimmoja, ambapo wadau hao wa michezo walilalamikia ushirikishwaji mdogo wa wanamichezo wa Zanzibar katika michezo inayoiwakilisha Tanzania.

Amesema serikali ina nia thabiti ya kurejesha hadhi ya michezo Zanzibar ili kuirejeshea sifa yake ya kimichezo iliyokuwa nayo hapo awali.


Wadau hao wa michezo wamesema hadhi ya michezo imeshuka Zanzibar kutokana na sababu mbali mbali zikiwemo upungufu mkubwa wa viwanja vya michezo hasa ile michezo ya ndani (Indoor games).

Sambamba na hilo wadau hao wa michezo wamesema serikali iliidharau michezo na haikutoa mkazo unaostahiki kuwaendeleza wanamichezo na kuibua vipaji vya wanamichezo.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar Abdillahi Jihadi Hassan amesema tayari Wizara yake imeshaanza mchakato wa kuwasiliana na Wizara ya Elimu Zanzibar wenye lengo la kurejesha michezo maskulini, ambayo itaibua vipaji ambavyo vitaendelezwa na kurejesha hadhi ya michezo Zanzibar.

Baadhi ya wadau hao wameiomba serikali kutodharau michezo ya asili ikiwemo mchezo wa karata, mchezo wa ng’ombe na kuogelea ambayo inaendana na utamaduni wa Zanzibar na husaidia pia shughuli za utalii.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.