MATANGAZO MADOGO MADOGO

Monday, April 2, 2012

Dk. Shein apangua Mawaziri : Shamuhuna apelekwa Elimu, Shaaban Ardhi

Nyanga aenda Kilimo, Jihad Mifugo

Mbarouk apewa Habari, Mansoor hana wizara maalum

Na Mwandishi wetu

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amefanya mabadiliko ya kuwabadilisha wizara baadhi ya Mawaziri.

Katika mabadiliko hayo, Dk. Shein amemteua Ramadhan Abdalla Shaaban kuwa Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, kuchukua nafasi Ali Juma Shamuhuna.

Kabla ya mabadiliko hayo, Waziri Shaaban alikuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali.

Waziri Shamuhuna ameteuliwa kuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, wizara ambayo ilikuwa ikishikiliwa na Waziri Shaaban.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyosainiwa na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, Dk. Shein amemteua Suleiman Othman Nyanga kuwa Waziri wa Kilimo na Maliasili kuchukua nafasi ya Mansoor Yussuf Himid ambae sasa anakuwa mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na Waziri asiyekuwa na wizara maalum.

Kabla ya mabadiliko hayo, Nyanga alikuwa mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na Waziri asiyekuwa na Wizara maalum.

Aidha Dk. Shein amembadili wizara aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Abdilah Jihad Hassan ambae sasa anakuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi.

Aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo, Said Ali Mbarouk sasa anakuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo.

Katika uteuzi mwengine, Dk. Shein amemteua Sheha Mohammed Sheha kuwa mshauri wa Rais Pemba.

Uteuzi huo umeanza tarehe 2 Aprili 2012.