Habari za Punde

Kamati Yaundwa Kuchunguza Baraza la Manispaa

Na Mwantanga Ame

SPIKA wa Baraza la Wawakilishi amewateuwa wajumbe wanne kuunda Kamati Teule itayosimamia kumchunguza Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa na mikataba tata inayodaiwa kuingiwa na Baraza hilo.

Hatua ya Spika Kificho, inakuja baada ya wajumbe wa Baraza hilo kukubaliana kuundwa kamati Teule kutokana na kutoridhika na ripoti iliyowashilishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Mwinyihaji Makame.

Wajumbe hao waliliambia Baraza hilo hawakubaliani na ripoti waliyopatiwa kutokana na kukosekana kwa uchunguzi ambao waliuhitaji kufikishwa mbele ya baraza hilo ambapo hapo awali ulifanywa na kamati ya Madiwani wa Baraza hilo.

Wajumbe hao walieleza ripoti iliyowasilishwa na waziri huyo ulikuwa ni muhtasari wa mapendekezo ya Kamati ya pili ya Serikali iliyoundwa kuchunguza kadhia hiyo ambayo haikuonesha uchunguzi uliofanywa kwa mahitaji ya maeneo ambayo walipendekeza.

Walisema ndani ya ripoti ya serikali juu ya uchunguzi huo imekuja zaidi na mapendekezo ya mwenendo wa baadae wa Baraza hilo jambo ambalo hawakubaliani nalo na kuitaka Wizara hiyo kuwapatia ripoti halisi.

Hata hivyo baada ya Wajumbe hao kupatiwa ripoti ya Madiwani walieleza hawakuridhika nayo na kuliomba Baraza hilo kuwaruhusu wajumbe wa Baraza hilo kuunda Kamati Teule ya Baraza kuchunguza kadhia hiyo.

Kutokana na maombi hayo Spika Kificho, alikubaliana na Wajumbe hao kuunda kamati ya watu wanne ambao watalichunguza baraza hilo.

Akitaja watu wataofanya uchunguzi huo, Spika Kificho alisema ni pamoja na Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe Ismail Jussa Ladhu, Mwakilish wa Kuteuliwa Asha Bakari Makame, Mwakilishi wa Wanawake Mwanaidi Kassim Mussa na Mwakilishi wa Chonga Abdalla Juma.

Wajumbe hao wa Kamati watafanya uchuguzi wao kwa kufuata hadidu rejea nne ambazo ni kuchunguza mikataba ya uwekaji mabango ya matangazo katika bara bara mbali mbali iliyoingizwa baina ya Baraza la Manispaa na makampuni tofauti na utekelezaji wa masharti ya mikataba hiyo.

Eneo jengine ambalo watalichunguza ni lenye kuhusu taratibu za uidhinishaji wa matumizi na uuzaji wa raslimali za Baraza la manispaa Zanzibar.

Pia Spika Spika Kificho, alisema suala jengine litalofanyiwa kazi na Kamati hiyo ni pamoja na kuangalia taratibu za uajiri na upandishaji wa vyeo katika Baraza la Manispaa na kama zilizingatia sifa zinazohitajika kushika nafasi watu waliopewa.

Aidha eneo jengine ni kumchunguza Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa juu ya madai ya kutofuata sheria na kanuni kwa makusudi, ubadhirifu wa fedha na kuhusika kwake katika migogoro inayolikumba Baraza la Manispaa.

Kamati hiyo inatarajiwa kuifanya kazi hiyi kwa kuhakikisha inaikamilisha kabla ya kipindi cha kuanza kwa kikao kitachojadili bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2012/2013 kinachotayariwa kuanza Juni 13, mwaka huu.

1 comment:

  1. At least we see sign of accountability, na hili suala la uajiri wa upendeleo na kupandishana vyeo kwa wasiostahili sio Manispaa tu uchunguzi unahitajika pia na wizara na mashirika mengine. mungu ibariki Zanzibar

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.