Habari za Punde

Pinda Awashangaa ‘Wakubwa’ Kudharau Kupanda Miti

Na Jumbe Ismailly, SINGIDA

WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amekemea utamaduni uliojengeka kwa baadhi ya watendaji wa serikalini kuhofia kupanda miti kwenye nyumba za serikali, kwa madai kuwa nyumba hizo haziwahusu wao.

Pinda alisema kumekuwepo baadhi ya watendaji wa serikali wanaoishi kwenye nyumba za umma kuwa na utamaduni wa kutopanda miti kwenye nyumba hizo kwa kisingizo kwamba haitakuwa na manufaa si jambo la msingi.

“Jamani mimi huwa nashangazwa sana na baadhi ya watendaji serikalini, wanapokuwa kwenye nyumba ya serikali hata kwa miaka 10, lakini cha kushangaza ni kutoona umuhimu wa kupanda miti kuzunguka nyumba anayoishi”, alifafanua waziri mkuu.

“Hivi kweli ukipanda miti hautakuwa na faida nayo wakati wote utakapokuwa ukiishi kwenye nyumba hiyo, kisa tu nyumba hiyo siyo yako na ukihamishwa atakuja mtu mwingine kunufaika nayo”? Pinda alihoji.

Waziri huyo alieleza hayo alipokuwa akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya taifa ya upandaji miti yaliyofanyika katika kijiji cha Ilongero, katika Halmashauri ya wilaya ya Singida.

Alisema siyo kweli kwamba unapopanda miti ni lazima unufaike uliyeipanda, lakini litakuwa jambo la busara sana uwepo wa miti hiyo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na hata kijacho.

Alisema utamaduni huo uliojengeka kwa baadhi ya Watanzania wachache, kwamba siyo busara kupanda miti katika eneo la nyumba ya kupanga, ni mawazo yaliyopitwa na wakati na hayanabudi kulaaniwa na watanzania wote wapenda maendeleo.

Aliwataka watanzania kujenga utamaduni wa kupanda miti ya kutosha kwenye maeneo yao, hususani kwenye nyumba za kupanga ikiwa ni njia moja wapo ya kuhahakikisha nchi inakuwa na misitu ya kukidhi mahitaji.

Alizitaja baadhi ya faida za uwepo wa miti hiyo kuwa ni pamoja na kusaidia upatikanaji wa hewa safi kwa viumbe hai, kivuli na kuboresha mandhari ya mahali husika.

Katika hatua nyingine, Pinda alisema Mkoa wa Singida umechaguliwa kuandaa maadhimisho ya siku ya upandaji miti kitaifa kwa sababu mkoa huo hauna misitu ya kutosha na kusababisha uwe mojawapo ya mikoa inayokabiliwa na ukame.

“Takwimu zinaonesha kuwa Singida ina ukubwa wa eneo la kilomita za mraba 49,438 ambazo ni sawa na hekta 51,595,667,na kwamba kati ya eneo hilo misitu inakadiriwa kuwa na hekta 464,361, sawa na asilimia 0.9 ya eneo lote la Mkoa wa Singida”,alisema.

Pinda alisema kutokana na hali hiyo upo umuhimu wa kila mwananchi katika maeneo aliko ikiwemo kwenye nyumba za kupanga, kupanda miti ya kutosha na pia kutunza uoto wa asili.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.