Na Waandishi wetu
KWA takriban mwaka mmoja na nusu, wananchi wa Kama wilaya ya Kaskazini ‘B’ wamekuwa wakiishi kwa hofu na kushindwa kupata usingizi kutokana na vitendo vya udhalilishaji vinavyoaminika kufanywa kwa njia za kishirikina.
Uchunguzi uliofanywa na waandishi wa habari hizi umebaini kuwa udhalilishaji huo hufanyiwa wanawake wakati wa usiku mkubwa ambapo huvuliwa nguo walizojifunika wakati wa kulala pamoja na kupapaswa katika maeneo ya siri.
Wananchi katika eneo hilo, walithibitisha kufanyiwa vitendo vya kashfa ikiwemo kuvuliwa nguo na kupapaswa wakiwa wamelala na mtu wasiyemfahamu na kwamba hata milango ya nyumba uifunge hufunguliwa na mtu huyo kuendelea na vitendo hivyo.
Mmoja wa wananchi hao Aziza Shaabani Mohammed alisema vitendo hivyo zaidi wamekuwa wakifanyiwa wanawake na kwamba zaidi nusu ya kijiji hicho na vijiji jirani mambo hayo yamekuwa yakifanyika kila usiku.
“Siku hiyo nimelala, kama saa nane usiku nilishituka usingizini nikahisi navutwa shuka niliyojifunika, nikanyanyua kichwa kidogo nikaona mtu mrefu mweusi kavaa bukta ananipiga tochi, wakati shuka langu kalitupa chini”, alidai Aziza mmoja wa mkaazi kijijini hapo.
Alisema baada kutokezewa na hali hiyo, alipiga kelele za kuomba msaada ndipo alipotoweka na kwamba hakumjua hata njia aliyopita na baada ya majirani kufika hawakumkuta.
Alisema anapoingia mdhalilishaji huyo huwa haonekani kwa sura, lakini kivuli chake kinaonekana na kwamba kabla ya kuwavua nguo wanawake na kuwapapasa huwamurika tochi.
Alisema vitendo hibyo vimekuwa kero kubwa na kwamba vimewaka kwenye hofu huku chumba kimoja mtu na mkewe wakilazimika kulala na watoto wao.
“Huwezi kuaminisha kulaza watoto wa kike chumba chao mbali kwa hali kama hii, watu wazima wanahofu na woga seuze wao”, alisema Aziza.
Naye Mbweni Yussuf Ali akielezea mkasa huo alisema mtu huyo ameshajitokeza katika chumba chake cha kulala kwa vipindi vine tofauti, hali inayomtia hofu na kushindwa kulala usingizi kwa amani.
“Ni ajabu huwezi kujua amepitia wapi anapoingia chumbani mwako anafungua milango yote na akikupapasa mkono wake ubaridi”,alisema.
Dada huyo alisema anafikiri kuwa suali hilo halifanywi na mtu mmoja kwani mmoja anaweza kuingia moja na mwengine nyumba nyengine kwa wakati mmoja watu hupiga kelele za kupapaswa.
Naye, Rukia Twaha alidai kuathiriwa na tukio hilo na kutokuwa na imani ya kuwalaza watoto wake peke yao kwa kuhofia kudhuriwa.
“Siku hiyo alipokuja usiku mkubwa sana akaingia chumbani kwa watoto wangu na kulala nao, walipotaka kupiga kelele aliwaambia msipige kelele mimi baba yenu”, alidai Rukia.
Nae mjumbe wa Sheha wa Shehia hiyo ya Kama, Omar Hassan Khamis wakati akizungumza katika mahojiano hayo, alidai kuwa taarifa hiyo tayari imesharipotiwa katika ofisi ya Sheha pamoja na Kituo cha Polisi Mfenesini.
Alisema kuendelea kuwepo kwa matukio kama hayo kijijini hapo ni kutokana na kutokuwepo kwa kikundi cha ulinzi shirikishi, ambacho kwa kiasi kikubwa kingeweza kupunguza vitendo vya kihalifu.
Juhudi za kumpata Sheha wa Shehia hiyo Foum Juma Foum kuthibitisha tukio hilo hazikufanikiwa kwani baada ya kufika nyumbani kwake hakuwepo.
Kwa upande wake Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai mkoa wa Kaskazini Unguja (RCO) Suleiman Hassan Suleiman, alisema hakuna taarifa rasmi za tukio hilo.
Hata hivyo aliahidi kulitolea taarifa kamili suali hilo mara tu baada ya kuwasilishwa ofisini kwake.
No comments:
Post a Comment