Habari za Punde

Balozi Seif Ziarani Cuba, Israel


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi anaondoka Nchini leo kuelekea Nchini Cuba Kupitia Nchini Israel kwa ziara  ya wiki mbili ya Kiserikali.

Balozi Seif katika ziara hiyo anafuatana na Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi, Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mh. Mohammed Aboud Mohammed na Mkurugenzi wa Idara ya Maafa Zanzibar Nd. Ali Juma Hamad kwa upande wa Israel wakati ziara ya Cuba ataambatana  na Waziri wa Afya Mh. Juma Duni Haji pamoja na Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Afya Dr. Malik Abdulla Juma.


Akipitia Nchini Israel Balozi Seif anatarajiwa kukutana na Uongozi wa Taasisi zinazosimamia na kushughulikia masuala ya Maafa, Uokozi pamoja na majanga ya Matetemeko.

Hatua ya ziara hiyo imelenga kuimarisha juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha kwamba inakuwa na uwezo zaidi wa kukabiliana na Maafa na Majanga kwa haraka wakati yanapotokea.

Akiwa Nchini Cuba Balozi Seif na Ujumbe wake anatarajiwa kukutana na Viongozi   mbali mbali wa Serikali ya Nchi hiyo katika suala zima la Kuimarisha Uhusiano uliopo wa muda mrefu uliopo kati ya pande hizo mbili.

Uhusiano huo utalenga zaidi katika masuala makubwa ya Sekta ya Afya ambapo Cuba imekuwa mshirika mkubwa wa Zanzibar katika kusaidia huduma za Afya katika kipindi cha zaidi ya miaka 40 iliyopita.

Zanzibar hivi sasa inaendelea kufaidika na huduma za Madaktari Bingwa wa Cuba wanaoendelea kutoa huduma za Afya pamoja na Mafunzo kwa Madaktari 50 Wazalendo wanaotarajiwa kuhudumia Hospitali mbali mbali za Unguja na Pemba mara baada ya kumaliza mafunzo  yao.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi atamaliza ziara yake Tarehe 19 Mei na kupitia Ras Al Khaima kwa mualiko wa Mfalme wa Nchi hiyo Bwana Saoud Bin Qasimi.

Viongozi hao wawili watapata fursa ya kuzungumzia Miradi kadhaa ya Nchi hiyo inayokusudiwa kuwekezwa hapa Zanzibar ikiwa na lengo la kuimarisha uhusiano wa pande hizo mbili.  
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi  anatarajiwa kurejea nyumbani Tarehe 22 Mei mwaka huu.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

2 comments:

  1. Jamani serikali inaenda kukitafuta nini Israel? Kweli nchi yetu maskini jamani lakini kuomba kwengine kuna gharama za kiutu. Sisi ni binaadamu tunapaswa kuyahisi mateso ya Wapalestina kabla ya kutafuta urafiki huu kwa manufaa ya kisiasa.

    ReplyDelete
  2. Kwa kawaida Mm sipendi 'uhafidhina' na misimamo isiyo na macho lkn. ktk hili ndugu yangu nakuunga mkono! hasa kile ulichoiita "gharama za kiutu"

    Kwa mtu muelewa na anaefuatilia siasa za kimataifa, atagundua hawa jamaa NOMA!.. ndio 'ARCHITECTS' wa migogoro mingi inayoendelea duniani leo hii.

    Wana uwezo wa kubuni tishio ambalo hata duniani halipo, na wazungu bila kupima wakalifanyia kazi!..kwa vile wao wanaamini kua Wayahudi ni wateule wa Mungu.

    Tokea waruhusiwe kufungua tena ubalozi wao hapa nchini baada ya kifo cha 'mwalimu' maafa yake tumeaanza kuyaona!

    Wamewachukua baadhi ya wachungaji na kwenda nao Israel kuwafundisha dini, baada ya kurudi wameanzisha makanisa ya kilokole, kazi yao kubwa ni kuisifia ISRAEL kuwa ni taifa teule na hivyo hatuna budi kuipenda na kuiombea!

    Wananukuu mstari wa BIBLIA usemao 'Aitukuzae Israeli nae atatukuzwa na ailaanie, nae amelaaniwa' lkn. wanasahau kua waisraeli waiotajwa sio wale wa leo!

    Baadhi ya maeneo ya nchi yetu leo hii yanapepea mabendera ya Israel utadhani tupo TEL-AVIV!..sasa utaifa wetu uko wapi?

    Chonde-chonde Viongozi wetu wa Z'bar tusije na sisi tukafika huko!

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.