Habari za Punde

JB Aisifu Zanzibar, Watu Wake kwa Ukarimu.



Na Aboud Mahmoud

MWENYEKITI wa Jumuiya ya wasanii wa filamu Tanzania 'Bongo Movies' Jacob Steven (JB), ameisifu Zanzibar na watu wake kutokana na tabia njema za ukarimu, utu, ustaarabu na mapenzi yao kwa wageni.

Kauli hiyo ameitoa juzi wakati wa uzinduzi wa filamu 'Toba' uliofanyika hoteli ya Bwawani, na kuhudhuriwa na wananchi wengi sambamba na viongozi wa ngazi mbalimbali serikalini.

JB alieleza kuwa, akhlaki hizo za Wazanzibari ndizo zilizowashawishi wasanii wa Tanzania Bara kutengeneza filamu yenye maudhui ya dini na tamaduni za Kiislamu, na kuja kuizindua kisiwani hapa.

Aidha, alisema sifa hizo za wananchi wa Zanzibar, zina ziada ya vionjo ya vivutio mbalimbali na mandhari za kupendeza, ambavyo huwavuta wageni wengi kutoka nchi za ng'ambo kuja kuvishuhudia.

Kwa upande mwengine, alisema ipo haja kwa serikali kushirikiana na wasanii wa filamu na wa sanaa nyengine ili katika kuitangaza vyema Zanzibar kupitia tasnia ya filamu na fani nyenginezo.

"Kutokana na vivutio vingi vilivyopo Zanzibar ambavyo dunia nzima haina, kama serikali itashirikiana na wasanii hao itasaidia kuitangaza vyema nchi kitaifa na kimataifa kupitia misingi ya mila na tamaduni za Kizanzibari", alifahamisha.

Wasanii mbalimbali wa filamu ambao ni maarufu akiwemo Issa Mussa (Cloud) na Vicent Kigosi (Ray) na Wema Sepetu, wameshiriki katika filamu hiyo ambayo uzinduzi wake ulipambwa na burudani za kasida na Maulid ya Homu kutoka madrasa mbalimbali za mjini Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.