Habari za Punde

Mpango wa Usafi ni Jukumu letu Waanzishwa

Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar imekusudia kuanzisha siku maalum ya USAFI NI JUKUMU LETU ambayo itakuwa ikitekelezwa kila siku ya Jumamosi ya mwanzo ya mwezi kuanzia Jumamosi ya Kesho tarehe 05 May, 2012. 

 Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi imeeleza kwamba kazi hizo za usafi kwa siku ya kesho zitaanza katika kituo cha Bustani ya Forodhani saa 12 asubuhi na kuwataka wananchi na wafanyakazi wa taasisi za Serikali na Binafsi kushiriki kikamilifu katika kazi hiyo. 


 Taarifa hiyo imefahamisha kwamba suala la usafi ni jukumu la kila mtu hivyo kila mmoja wetu anastahiki kudumisha usafi katika eneo lake analoishi.

 Jambo hilo kwa kiasi kikubwa litaweza kuyaweka mazingira ya mji wa Zanzibar na vitongoji vyake katika hali ya usafi endelevu na kuifanya azma hiyo iweze kufanikiwa.

 Hivyo taarifa hiyo imeziomba taasisi zote za Serikali na binafsi kuripoti hapo kesho katika uzinduzi wa Mpango huo hapo Forodhani Mjini Zanzibar. Aidha wakuu wa Taasisi wamehimizwa kuwaarifu wafanyakazi wao kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo muhimu pamoja na vyombo vyote vya habari ili kuweza kuhamasisha wananchi ipasavyo. 

 IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.