Habari za Punde

Nchunga Awakwepa Wazee Yanga

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MKUTANO wa wazee wa klabu ya Yanga uliokuwa ufanyike leo jijini Dar es Salaam umefutwa.

Mwenyekiti wa klabu hiyo iliyokumbwa na mvutano Lloyd Nchunga, amechukua hatua hiyo kwa kuufuta mkutano huo kati yake na wazee ambao aliuitisha kabla.

Nchunga amekaririwa akisema kuwa, uamuzi wa kuufuta mkutano huo umetokana na baadhi ya wanachama kutoa taarifa za kupotosha, hivyo amewataka kusubiri hadi Julai 15 utakapofanyika mkutano mkuu wa wanachama.

"Nimechukua hatua ya kuufuta mkutano huo ili baadhi ya wanachama wasije kupotosha kwa kudai kuwa nimeitisha mkutano kinyume na katiba kwani mimi sijaitisha mkutano mkuu wa wanachama", alifafanua.

Aidha ametaja sababu nyengine ya kuahirisha mkutano huo, imetokana na barua waliyopata kutoka kwa aliyekuwa mfadhili mkuu, Yussuf Manji ambayo kamati tendaji ya klabu hiyo inatarajiwa kukutana kesho kwa ajili ya kuijadili.

Mapema, iliarifiwa kuwa, wanachama wa Yanga wa matawi yote ya Mkoa wa Dar es Salaam, walitarajiwa kukesha jana ili kufanya maandalizi ya mkutano huo mkuu ambao sasa umefutwa.

Katika taarifa za awali, ilielezwa kuwa wazee wa klabu hiyo walitaka mkutano huo ulioota mbawa, ndio uwe mkutano mkuu, badala ya dhamira ya Nchunga kutumia fursa hiyo kutangaza Julai 15, kuwa ndiyo siku ya mkutano mkuu.

Wakati wazee hao wakisema hivyo, aliyekuwa mfadhili mkuu wa klabu hiyo Yussuf Manji, alitoa masharti kwa uongozi huo ili arudishe ufadhili wake, ambapo miongoni mwa masharti hayo ni kurudisha nyuma tarehe ya mkutano mkuu wa wanachama kwa siku 30.

Awali, Mwenyekiti wa vijana wa matawi ya Mkoa wa Dar es Salaam Bakili Makele, alisema mkutano huo wa kukesha jana, ni maandalizi ya ule uliopangwa awali kufanyika leo, kabla kufutwa na Mwenyekiti Lloyd Nchunga.

Tangu iliposhindwa kutetea taji la ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, ikiwemo kufungwa na watani wao wa jadi Simba kwa mabao 5-0 Mei 6, mwaka huu, hali ndani ya klabu ya Yanga yenye makao makuu yake mtaa wa Jangwani, si shuari ilitawaliwa na misuguano huku wazee wakidai wakabidhiwe timu yao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.