Joseph Ngilisho, ARUSHA
JAMBAZI sugu lililokuwa likitafutwa kwa
muda mrefu mkoani hapa, aliyetambulika kwa jina la Peter Toshi mkaazi
wa Daraja mbili jijini ARUSHA, amekufa baada ya kupigwa risasi na askari polisi
katika majibishano ya kurushiana risasi wakati akijiandaa kufanya uhalifu
akiwa amefuatana na mwenzake.
Kamanda wa polisi mkoani hapa, Liberatus
Sabas alisema kuwa tukio hilo limetokea Agosti 29 mwaka huu majira ya saa 5
usiku katika eneo la Sinoni daraja mbili ndani ya Manispaa ya Arusha.
Sabas alisema kuwa, kuuawa kwa jambazi
huyo ambaye alikuwa akitafutwa muda mrefu ni baada ya wasamaria wema kutoa
taarifa kwa jeshi la polisi kuhusiana na watu hao ambao ni majambazi baada
ya kuwatilia mashaka.
Alisema kuwa jambazi huyo akiwa na
mwenzake walikuwa wamesimama katika eneo la bar ya tanzanite iliyopo eneo la
sinoni ambapo walikuwa wakijiandaa kwa ajili ya kwenda kufanya uhalifu.
Alisema kuwa, baada ya polisi kupata
taarifa hiyo walifika eneo la tukio, ambapo majambazi hao walipowaona polisi
ghafla walianza kuwarushia risasi ndipo polisi walianza kujibu mapigo na
hatimaye kufanikiwa kuumpiga jambazi huyo ambaye alifariki dunia.
Alifafanua kuwa, katika majibizano hayo ya
risasi jambazi mwingine alifanikiwa kukimbia na jeshi la polisi linaendelea na
uchunguzi zaidi katika kumsaka aliyekimbia.
Aidha baada ya jambazi huyo, kufariki
alipekuliwa na kukutwa na silaha moja aina ya Pistol aina ya Tisas ikiwa
imefutwa namba zake huku ikiwa na risasi 3 tu.
Alifafanua zaidi kuwa, jambazi huyo hivi
karibuni alitoka mahabusu akikabiliwa na tuhuma mbalimbali za mauaji na
unyang’anyi wa kutumia silaha na amekuwa akiendelea na uhalifu mkoani
hapa na jeshi la polisi limekuwa likimsaka kwa muda mrefu sana.
Sabas alisema kuwa, jeshi la polisi mkoani
hapa linaendelea na uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo, na amewaomba
wananchi mbalimbali kuhakikisha kuwa wanatoa ushirikiano wa kutosha
klatikakuwafichua wahalifu wote.
Hata hivyo taarifa kutoka eneo la tukio
zimedai kuwa jambazi huyo akiwa na mwenzake alipanga kwenda kufanya mauaji kwa
mkazi mmoja wa eneo hilo(jina limehifadhiwa) anayedaiwa kuwa ni rafiki
yao baada ya kubaini kuwa amekuwa akiwasaliti kwa kutoa taarifa zao za uhalifu
kwa polisi.
Mwili wa jambazi hiuyo umehifadhiwa katika
chumba cha maiti katika hospitaloi ya mkoa Mount meru kwa ajili ya uchunguzi
huku jeshi hilo likiendesha msako ka jaambazi mwingine aliyefanikiwa kutoroka.
No comments:
Post a Comment