Habari za Punde

Hatimae kile choo cha uwanja wa ndege chakamilika

 Mrakibu Mwandamizi wa Polisi SSP Mkadam Khamis akimpa Taarifa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ya kukamilika rasmi kwa matengenezo ya choo maalum cha kuchunguzia wasafiri wa anga wanaotiliwa mashaka kwa kujihusisha na usafirishaji wa dawa za kulevya kilichopo uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar Nd. Said Iddi Ndembwagani mara baada ya kuwasili uwanjani hapo kukaguwa choo maalum kwa ajili ya kuchunguzwa wasafiri wanaotuhumiwa kuingiza dawa za kulevya nchini.

Na Othman Khamis Ame, OMPR

Mpango maalum ulioandaliwa na Jeshi la Polisi wa Kushirikisha watendaji wa Taasisi tofauti zinazojihusisha na mapambano dhidi ya uingizwaji wa Dawa za kulevya hapa Nchini utasaidia kuondosha urasimu katika uendeshaji wa kesi zinazowahusu watuhumiwa wa dawa haramu.
Mkuu wa Kitendo cha mapambano dhidi ya dawa za kulevya Mrakibu mwandamizi wa Polisi SSP Mkadam Khamis alieleza hayo mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyefika ghafla mapema asubuhi katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar.
Balozi Seif alifanya ziara hiyo fupi ikiwa na lengo la kukagua choo maalum kilichojengwa kwa ajili ya kuwatambuwa wasafiri wanaotiliwa mashaka kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya kwa kutumia anga.

Mrakibu mwandamizi wa Polisi SSP Mkadam Khamis alisema mpango huo umelenga kupunguza au kuondosha kabisa malamiko yanayotolewa na upande wa walalamikaji au mawakili kwa kudhani kuwa kesi dhidi ya watuhumiwa wa dawa hizo zimekuwa zikipangwa kwa makusudi na Watendaji wa Jeshi la Polisi.
“ Sidhani kama kutakuwa na malalamiko makubwa hivi sasa kutoka upande wa walalamikaji au mawakili wanaofuatilia kesi dhidi ya watuhumiwa wa dawa za kulevya kwa vile wahusika wa pande zote watakuwa wakihusika katika kushuhudia maovu yanayofanywa na washukiwa wa makosa hayo”. Alisisitiza SSP Mkadam.
Mrakibu mwandamizi huyo wa Polisi Kamanda Mkadam alifahamisha kwamba upo umuhimu pia wa kufikiriwa kuwekwa choo kama hicho katika Bandari Kuu ya Zanzibar iliyopo Malindi.
SSP Mkadamu Khamis alisema hatua hiyo inaweza kusaidia sana udhibiti wa uingizwaji wa dawa haramu za kulevya katika maeneo yotemawili ya usafiri wa Bahari sambamba na ule wa uwanja wa ndege.
Akizungumzia tatizo la Fedha chafu ambazo hupatikana kupitia biashara haramu ya dawa za kulevya Mrakibu Mwandamizi huyo wa Polisi alifahamisha kwamba tabia ya baadhi ya watu kusafiri na fedha nyingi imekuwa ikitiliwa mashaka na walinzi wa maeneo ya usafiri kwa kukosa mpango maalum unaoelezea usafirishaji wa uhakika wa fedha hizo.
Alisema mpango huo ukiwekwa vizuri unaweza ukasaidia kupunguza tamaa kubwa iliyojengeka hivi sasa kwa baadhi ya watu na hasa Vijana kujiingiza katika biashara ya dawa za kulevya ili wajipatie utajiri wa haraka.
Mrakibu mwandamizi wa Polisi Kamanda Mkadamu alimueleza Balozi Seif kwamba choo hicho hivi sasa kiko katika kiwango kinachokubalika katika matumizi yaliyokusudiwa baada ya kumalizika matengenezo yake.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliwapongeza watendaji wa Kitendo hicho kwa hatua nzuri waliyofikia ya kukamilisha matengenezo ya Choo hicho.
Balozi Seif alisema hatua hiyo imekamilisha kilio cha muda mrefu kilichokuwa kikitolewa na Watendaji wa Kitengo hicho cha ukosefu wa kifaa hicho ambacho ni muhimu katika utekelezaji wa majukumu yao katika mapambano dhidi ya uingizwaji wa dawa za kulevya Nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.