Habari za Punde

Wahitimu Zanzibar University watakiwa kutumia vyema taaluma waliyoipata

Na Khadija Khamis-Maelezo
Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Zanzibar TUNGUU wametakiwa kuitumia vyema taaluma waliyoipata Chuoni hapo ili iwe chachu ya maendeleo kwao na Taifa kwa ujumla.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Ali Juma Shamhuna kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohamed Shein katika Mahafali ya 10 ya Chuo hicho ambapo Wahitimu wa ngazi ya Vyeti, Stashahada,Shahada na Uzamili walitunukiwa vyeti.

Alisema Taaluma waliyoipata Wahitimu Chuo hapo ndio mkombozi wa maisha yao hivyo uangalifu unahitajika katika kuhakikisha kuwa inawasaidia kujikwamua kwenye umasikini na kuisaidia Serikali katika kuliletea taifa maendeleo.
“Taaluma mliyoipata muitumie vizuri katika maisha yenu ili imuletee maendeleo nyinyi wenyewe binafsi na hatimaye taifa kwa ujumla”alisema Waziri Shamhuna.
Aidha aliwataka Wahitimu hao kutotosheka na viwango walivyovipata badala yake wafanye mipango ya kujiendeleza zaidi kielimu ili kukabiliana vyema na kasi ya mabadiliko ya nchini.
Alisema kwa sasa Elimu imepanda ambapo kila mwaka Vyuo vikuu vinatoa Wahitimu tofauti hivyo na wao wasibweteke na walipoishia bali wajiendeleze na ngazi nyingine.
“Nakuusieni wahitimu nyote mliopata shahada leo msitosheke na hapo mlipofika hivi sasa bali mzidi kujielimisha zaidi na taaluma ili muweze kukabiliana na soko la ushindani.”alieleza
Aidha alisema kuwa wanafunzi ambao wamehitimu katika chuo hicho wawe mfano bora kwa wenzao ambao wanaendelea kusoma na wale ambao wanaotarajia kusoma chuoni hapo kwa kuweza kukijengea sifa kutokana na ufanisi wa maendeleo ya kazi zao.
Pia alikipongeza Chuo cha Tunguu kwa kupiga hatua kimaendeleo kwa kufanikiwa kutoa mafunzo ya fani tofauti ikiwemo Utawala, Uhandisi, Sheria, Mipango ya jamii na Uchumi.
Mapema Waziri huyo alizindua jengo jipya la chuo hicho lenye thamani ya shilling milioni 916 ambalo linatarajiwa kutumika kwa kutolea mafunzo ya Uhandisi.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho Profesa Mustafa Rashash aliwataka wahitimu hao kuwa makini katika harakati zao za kutafuta ajira ikiwemo kujilinda na vishawishi ambavyo vinaweza kuwaletea maambukizi ya Ukimwi.
Jumla ya wanafunzi 590 wamehitimu katika chuo Cha Zanzibar TUNGUU kwa mwaka 2012 ambapo kati ya wanawake ni 292 na wanaume 298.
IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.