Habari za Punde

E-government’ yawapa matumaini ya maendeleo Pemba


Na Maryam Talib, Pemba

MKUU wa mkoa wa Kaskazini  Pemba,  Dadi Faki Dadi amezindua  mradi  wa serikali ya mtandao  (e - government) kisiwani Pemba na kusema mradi huo utasaidia kurahisisha shughuli za kiutendaji serikalini.
Uzinduzi huo ulifanyika skuli ya Utaani Wete ambapo alifanya mazungumzo ya moja kwa moja kwa njia video kupitia kompyuta na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, D. Ali Mohamed Shein aliyekuweko Mazizini Unguja.
Alisema utaratibu huo wa kiutawala unatoa fursa kwa watendaji walioko mbali kijeografia kuwasiliana kwa urahisi, kupeana maagizo, na mrejesho wa utekelezaji kwa shughuli ambazo zinahitaji mwitikio wa haraka.
Akizungumza katika mahojiano nje ya uzinduzi huo, Dadi alisema kwa kuanzia Mkoa wake umejipanga kutumia utaratibu wa e- government kupambana na matatizo ya ubakaji wa watoto, unyanyasaji wa wanawake, kilimo, usalama  na magendo ya karafuu.

Alisema kwa sasa kuna ugumu mkubwa kupata taarifa za mambo hayo hasa yale yanayohusiana na ubakaji na unyanyasaji wa wanawake hali ambayo huchelewesha kupatikana kwa ushahidi na kuchukuliwa hatua za kufaa.
Mapema akimkaribisha Mkuu huyo wa Mkoa, Ofisa Mdhamini Ofisi ya Raisi Utumishi wa Umma na Utawala bora, Maua Mohammed Salim alisema kuanzishwa mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa mikakati ya wizara yake ya kuimarisha utawala bora katika visiwa vya Zanzibar.
Alisema uzinduzi uliofanyika ni hatua ya awali tu ya utekelezaji wa mkakati huo na katika hatua zinazofuata mpango huo  utaimarishwa zaidi kivifaa ili uweze kutumika katika shule za msingi na sekondari na kuboresha utoaji wa elimu.
Mmoja wa wanafunzi wa skuli ya Utaani aliehudhuria hafla hiyo, Mohammed Khamis aliipongeza serikali kwa hatua hiyo muhimu akisema utawasaidia wanafunzi wa kisiwani Pemba kutafuta taarifa za kielimu na kuwasiliana na walimu na wataalamu wengine walioko nje ya  kisiwa hicho.
Alisema kwa sasa wanafunzi kisiwani Pemba wengi wao wanategemea maktaba pekee kwa kupata vitabu vya kujifunzia na hawana fursa ya kutumia mtandao kutafuta taarifa zaidi za kielimu.
Mradi wa e- government umetekelezwa kwa mkopo nafuu kutoka serikali ya watu wa China kwa gharama ya dola za Marekani milioni 19.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.