Habari za Punde

Dk. Shein Akabidhiwa Mpira na Kamati ya Kuibua Vipaji Zanzibar Ikulu

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar  6.2.2013

   
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amekabidhiwa mipira na  Kamati ya Ugawaji Mipira chini ya mradi wa  ‘One World Football For Africa’ na kusisitiza haja na umakini katika ugawaji na usimamizi wake ili kuwafikishia walengwa katika maeneo yote ya Unguja na Pemba.
 
Dk. Shein aliihakikishia Kamati hiyo kuwa na yeye  kwa upande wake atachukua juhudi za kuigawa kila panapostahiki kwani lengo la ugawaji wa mipira hiyo ni kuhakikisha kuwa watoto nao wanapata fursa ya kucheza.           
Hayo aliyasema leo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Kamati ya Ugawaji Mipira, iliyofika Ikulu mjini Zanzibar kwa lengo la kumkabidhi mipira ili na yeye asaidie katika ugawaji kwa lengo la kuisambaza  kwa watu na sehemu husika pamoja na vikundi mbali mbali Unguja na Pemba.
 
Katika maelezo yake, Dk. Shein alisema kuwa licha ya juhudi zitakazochukuliwa na Kamati hiyo lakini pia, inawezekana wakatokea baadhi ya watu wakataka kuharibu utaratibu huo wa ugawaji wa mipira hiyo katika maeneo mbali mbali nchini.
 
Kutokana na hilo, Dk. Shein aliitaka Kamati hiyo kuwa makini na watu hao katika zoezi zima la ugawaji wa mipira hiyo 20,000 ambayo itakuwa chachu katika kuimarisha michezo hasa mpira wa miguu hapa nchini.
 
Dk. Shein alitoa pongezi kwa Kamati hiyo kwajuhudi zake za makusudi ilizozichukua hadi kufanikiwa kupata mipira hiyo ili kufanikisha mradi huo maalum kwa mashirikiano kati ya Baraza la Taifa la Michezo  Zanzibar na ‘Save the Children’.

 
Dk. Shein alisisitiza kuwa ni lazima vijana wacheze, hivyo mbali ya juhudi hizo zilizochukuliwa katika kupatikana mipira hiyo pia, ipo haja kwa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BMTZ) kutoa maelekezo juu ya michezo.
 
‘Tujitahidi kwa wale wanaogawa kufikisha pale panapokusudiwa kwani katika jamii wapo watu wenye hulka tofauti hivyo ipo haja ya kuhakikisha usimamizi mzuri unafanyika katika ugawaji wa mipira hiyo”,alisisitiza Dk. Shein.
 
Aidha, Dk. Shein aliieleza Kamati hiyo matumaini yake kuwa muda mfupi ujao Sera nzuri ya Michezo itakayosaidia kuiimarisha sekta hiyo nchini itapatikana.
 
Nae Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar Sharifa Khamis, alimueleza Dk. Shein kuwa Kamati hiyo inawajumbe kutoka Taasisi mbali mbali ambao watawahusisha watu, makundi na maeneo pamoja na Taasisi ambazo zinashughulikia vijana, walemavu, wanaowacha madawa ya kulevya kama vile Ofisi ya Wanawake na Watoto, Afisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, viongozi wa Majimbo na wengineo.
 
Mwenyekiti huyo alieleza kuwa mipira hiyo inaubora mkubwa na uwezo wa kuishi zaidi ya miaka mine na haitiwi pumzi na unaweza kuchezwa sehemu yoyote kama vile kwenye mawe, kwenye maji, kwenye michanga na kwengineko.
 
Mapema Makamo Mwenyekiti wa BMTZ Bwana Khamis Abdalla Said, alimueleza Dk. Shein kuwa Mradi huo umebuniwa kati ya Baraza hilo la Michezo Zanzibar pamoja na ‘Save the Children’ kwa kufanya kazi pamojakwa lengo la kuhakikisha wananchi wote wanashiriki michezo.
 
Alisema kuwa Mradi huo mkubwa ni wa mwanzo kufanyika hapa Zanzibar kwa nchi zilizo Kusini mwa  Jangwa la Sahara, Mradi ambao ulikamilishwa na ndani ya mwezi mitatu tu ambapo pia, Mradi huo utasaidia kuleta vuguvugu la michezo kwa vijana kama ilivyo azma ya Dk. Shein katika kuinua michezo nchini.
 
Aidha, Makamu Mwenyekiti huyo alieleza kuwa mradi huo ambao umetumia karibu ya Shilingi milioni 900 za Kitanzania ni mradi mkubwa na kushukuru Serikali kwa kusamehe kodi ya mipira hiyo.
 
Bwana Khamis alisema kuwa asilimia 50, ya mipira hiyo itapelekwa katika skuli za Serikali na za binafsi na asilimia 30 hadi 40 itapelekwa kwa timu za ZFA ambapo ndani yake mna timu zipatazo 1200 huku akieleza kuwa  watu wapatao 340,000 watanufaika na mipira hiyo.
 
Pamoja na hayo, Khamis alieleza kuwa Mradi huo umepelekea kuzaa mradi mwengine wa kuwafundisha makocha kwa muda wa m iaka mitatu ikiwa ni pamoja na kuwapa elimu ya stadi ya maisha kwa Makocha wa Unguja na Pemba.
 
Sambamba na hayo, makamu Mwenyekiti huyo alimueleza Dk. Shein kuwa mbali ya hatua hizo pia, kuna mradi wa ujenzi wa viwanja 10 vya ndani katika kila Wilaya ambapo kila kiwanja kitahusisha michezo mitano.
 
Pia, Makamu huyo alieleza ujio wa mtaalamu wa riadha kutoa nchini Ujerumani ambaye atatoa mafunzo hapa nchini ambapo tayari ameshasaidia kontena moja la vifaa vya michezo ya riadha yakiwemo magodoro, mikuki na matufe.
 
Akiyataja miongoni mwa makundi yatakayofaidika na mgao huo wa mipira Makamu Mwenyekiti huyo aliyataja kuwa ni ZFA, timu za mpira wa pete, timu za Majimboni, kwenye nyumba za mayatima, Vyama vya michezo, vikosi vyote, wenye ulemavu,Sober House, Wakuu wa Mikoa na Wilaya, watoto wa Juvinile na Junior na wengineo
 
Nae Mwakilishi wa ‘Save the Children’ alieleza kuwa Shirika hilo litaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika juhudi zake za kuimarisha maendeleo ikiwemo michezo kwa kutambua kuwa michezo hujenga urafiki, afya sanjari na kuepuka manyanyaso kwa watoto.
 
Mradi huo wa ‘One World Football For Africa’ aliuzindua Dk. Shein mwezi uliopita huko katika kiwanja cha Aman mjini Zanzibar.
 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.