Habari za Punde

India kuipatia Zanzibar dola 50m



Na Fatma Kassim, Maelezo
INDIA itaipatia Zanzibar mkopo wa dola milioni 50 za Marekani ili kuimarisha sekta ya afya Unguja na Pemba.

Hayo yameelezwa na Balozi mdogo wa India aliepo Zanzibar Pawan Kumar alipofanya mazungumzo na uongozi wa wizara ya Afya.

Alisema kutokana na uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya Zanzibar na India watahakikisha huduma za afya zinaimarika na wananchi wanapata huduma kwa ufanisi.

Alifahamisha kuwa India itasaidia mafunzo kwa wafanyakazi wa sekta ya afya, ujenzi wa hospitali mbili za wilaya Unguja na Pemba na kuvifanyia matengenezo vituo vya afya.

Aidha alisema India ina mpango wa kuleta walimu ambao  watasaidia  kufundisha namna ya uhifadhi wa vifaa vya hospitali kama vile CT Scan X-ray na vifaa vyenginevyo ili kuepuka usumufu wa kuharibika.


Katika upatikanaji wa mafunzo kwa wafanyakazi wa Zanzibar nchini India, nafasi za masomo 300 zilizotengwa kwa Tanzania 80 zimetengwa kwa ajili wa Wazanzibari ambazo kati ya hizo  zimo za sekta ya afya.

Kwa upande wake Waziri wa Afya Zanzibar, Juma Duni Haji aliishukuru India kwa misaada yake wanaitoa katika sekta afya.

Alisema mkopo huo utasaidia kuimarisha huduma za afya katika hospitali mbali mbali nchini na kuweza kutoa huduma zenye ubora na kuomba India kuzidi kusaidia sekta hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.