Na Kadama Malunde,Shinyanga
MWANAMKE mmoja Happiness Luhende mwenye umri wa miaka 28 mkazi wa Lubaga katika manispaa ya Shinyanga, ameuawa kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kunyongwa na mume wake kwa kutumia kamba ya katani baada ya kumtuhumu kuwa anamsaliti kwa kufanya mapenzi na wanaumme wengine.
Tukio hilo limetokea juzi jioni majira ya saa 12 jioni katika kata ya Lubaga, ambapo watu walioshuhudia tukio hilo walisema Majija Clement mwenye umri wa miaka 22-23 ambaye ni mume wa marehemu aliona ujumbe mfupi kwenye simu ya mkewe uliokuwa unaashiria kuwa umetoka kwa mwanamme mwingine ukimtaka akutane naye eneo fulani ,ndipo alipoamua kumpiga kisha kumnyonga kwa kutumia kamba ya katani.
Akizungumzia tukio hilo mjomba wa marehemu, John Sumari,alisema mpwa wake aliolewa mwezi Disemba mwaka jana na mpaka mauti yanamfika walikuwa hawajabahatika kupata mtoto.
“Marehemu ni mtoto wa dada yangu,wamekuwa wakigombana mara kwa mara,nimewahi kusuluhisha kesi mara mbili,kesi ya kwanza ilikuwa ni ya mwanamme kumtuhumu mke wake kuwa ana mwanamme mwingine baada ya kupigiwa simu,kesi ya pili ilikuwa mwezi uliopita ambapo Majija Clement alimtuhumu mke wake kwamba anafanya mapenzi na balozi wa eneo hilo,lakini hayo yaliisha na leo ndiyo haya tena yametokea,” aliongeza.
Walioshuhudia tukio hilo walisema mtuhumiwa ni mwenyeji wa wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza,na alikuja Shinyanga kwa mama yake na kubahatika kumwona Happiness akaanza kuishi naye kama mke wake na kuongeza kuwa mwanamme huyo anafanya shughuli za kuchoma tofali na ni mwendesha baiskeli maarufu kama daladala.
Mwenyekiti wa mtaa wa Lubaga, Shabani Mashishanga alisema mtuhumiwa alikuwa ni mhamiaji wa eneo hilo na ametoroka baada ya kufanya tukio hilo na jeshi la jadi (sungusungu) linamtafuta.
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga,Kamishina Msaidizi wa Polisi, Evarist Mangalla alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi huku akiwaomba kushirikiana na jeshi hilo kumtafuta mtuhumiwa ili sheria ichukue mkondo wake.
No comments:
Post a Comment