STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 30 Novemba, 2013
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema miradi ya Mfuko wa Maendeleo wa Jimbo ni ya wananchi hivyo wanapaswa kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi hiyo pamoja na kuhusika moja kwa moja katika matumizi ya fedha za miradi.
Ameitaka Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais kuwaelimisha wananchi kuwa miradi hiyo ni yao na kwamba wanapaswa kuwajibika kwa matumizi ya fedha za miradi hiyo kwa kukakikisha kuwa fedha hizo zinatumika kama zilivyokusudiwa.
Dk. Shein ameeleza hayo jana wakati wakati akihitimisha mjadala wa Taarifa ya Utekelezaji wa Mpangokazi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais kwa mwaka 2012/2013 na robo mwaka ya mwaka wa fedha 2013/2014.
Ametaka wananchi waelimishwe athari za kutosimamia matumizi ya fedha hizo kwa kuwa wanapaswa kutolea maelezo ya matumizi ya fedha za miradi wanayoitekeleza kabla ya Serikali kupeleka fedha nyingine kwa ajili ya Mfuko huo.
Sambamba na maelekezo hayo Dk. Shein ameitaka Idara ya Maaafa katika Ofisi hiyo kuandaa programu maalum za kutangaza shughuli zake ikiwemo kutoka tahadhari za mara kwa mara dhidi ya maafa yanayoweza kutokea.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekti wa Baraza la Mapinduzi ameipongeza Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais kwa kutekeleza majukumu yake ufanisi kwa mwaka wa fedha uliopita na kutolea mfano kuwa hakuna hata idara moja ambayo imetekeleza majukumu yake chini ya wastani wa asilimia 62.
Kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi alisisitiza usimamizi wa karibu wa Fedha za Mfuko wa Maendeleo ya JIimbo na kusisitiza kuwa fedha hizo ni za wananchi na hazina budi kutumika kwa miradi na wanachi na kuongeza kuwa fedha hizo lazima ziwasilishwe katika akaunti ya mfuko si vinginevyo.
Akitoa maelezo katika kikao hicho Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mohamed Aboud Mohamed alieleza kuwa Ofisi yake katika mwaka wa fedha uliopita iliweza kutekeleza malengo yake kwa asilimia 94.
Aliyataja baadhi ya malengo hayo kuwa ni pamoja na kuwajengea uwezo wafanyakazi wa Ofisi hiyo ili wawese kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, kuratibu shughuli za Muungano na miradi ya SMZ na SMT, kuimarisha huduma za Uendeshaji, usalama kazini na kutoa mafunzo kwa wafanyakazi juu ya kujikinga na majanga mbali mbali.
Malengo mengine ni kuimarisha shughuli za utafiti kwa kuwajengea uwezo watafiti chipukizi, vitengo vya utafiti vya Wizara za SMZ na kuendeleza mashirikiano na taasisi za utafiti za ndani na nje ya nchi na za kikanda.
Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Ofsi ya Makamu wa Pili wa Rais Dk. Khalid Salum alisema Ofisi yake imeweza kuratibu uhuishaji wa fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo kwa majimbo yote Unguja na Pemba na inaendelea kufuatilia na kutathmini miradi ya Mfuko huo pamoja na miradi mingine midogomidogo ya wananchi.
Kwa upande wa Pemba Ofisi iliratibu na kusimamia utekelezaji wa miradi 21yenye thamani shilingi milioni 529.8 na kuratibu maendeleo ya miradi mingine 184 ya TASAF iliyokamilika huku miradi 142 ilitembelewa na jamii kupatiwa elimu juu ya umuhimu wa miradi hiyo.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822
No comments:
Post a Comment