Habari za Punde

Waziri wa Habari Mbarouk Atembelea Kituo cha Kurushia Matangazo ya ZBC Bungi Zanzibar.

Na Abdulla Ali Maelezo-Zanzibar                                
Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar Mhe. Said Ali Mbarouk amesema zaidi ya shilingi milioni 100 za Kitanzania  zinahitajika ili kukamilisha ujenzi wa kituo kipya cha kurushia matangazo cha Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC). 

Hayo ameyasema wakati wa ziara yake ya kutembelea kituo hicho kilichopo Bungi Wilaya ya Kati Unguja.

Amesema lengo la ziara hiyo ni kuangalia ufanisi wa kazi kwa watendaji wa kituo hicho na kusisitiza kuwa ni jukumu la Wizara kufanya hivyo ili kuimarisha dhana ya uwajibikaji kwa watendaji wake.

Amesema kwa sasa Serikali inaweza kuendesha mitambo ya kurushia matangazo iliyopo kituoni hapo bila ya kutegemea mafundi kutoka nje ya Nchi kama vile China kwani ina mafundi wa kutosha wenye uweledi katika fani ya uhandisi wa mitambo ya Redio na Televisheni.


Aidha ametanabahisha kuwa Serikali ina jukumu la kuwaongezea ujuzi baadhi ya mafundi hao kwa kuwapeleka kusoma nje ya Nchi ili waende sambamba  na mabadiliko ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ya Umma.

Waziri huyo amewataka mafundi wa kituo hicho kurekebisha matatizo madogo madogo yaliyopo kituoni hapo ikiwemo kufunga mafeni pamoja na viyoyozi (Air Condition) ili kuzifanya mashine hizo zidumu kwa muda mrefu na kupunguza hasara ya kuungua mara kwa mara kutokana na joto kali linakuwemo katika vyumba hivyo vya kurushia matangazo.

Waziri Mbarouk amewataka wafanyakazi kuwa wabunifu katika utendaji wao wa kazi na kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa lengo la kuliimarisha shirika hilo kwani matangazo yake ni muhimu ndani na nje ya Nchi ikiwemo mwambao wa Kenya ambao wanategemea kwa kiasi kikubwa matangazo ya ZBC.

Nae fundi mkuu wa kituo hicho Nd. Ali Aboud Talib amesema wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo uchakavu wa  nyaya za kurushia matangazo (Cable) kutokana na kutumika kwa muda mrefu, kuwepo kwa msitu mkubwa kutokana na kukosekana kwa wafanyakazi wa kusafisha eneo hilo.

Vilevile amesema tatizo la usafiri ni usumbufu mkubwa kwao kwani hadi sasa kituo hicho kina gari moja ambayo haitoshelezi kwa kazi za kila siku pamoja na Taa za Mnara wa kurushia matangazo kuwa haziwaki.

Aidha amesema mashine za kurushia matangazo (Transmitter) hazina uwezo mkubwa ukilinganisha na vyomo vyengine vya habari vilivyopo Nchini kwani hadi sasa ZBC inatumia mashine yenye uwezo wa masafa ya 1 kilowatts ambapo vyombo vyengine vinatumia mashine zenye uwezo wa masafa hadi 4 kilowatts.

Fundi huyo amewataka wananchi kuwa wazalendo kwa kuangalia Televisheni yao ya nyumbani (ZBC) ili kuipa thamani ndani na nje ya Nchi jirani kwa kuwa na watazamaji wengi.

1 comment:

  1. Zamani tukiipenda sana TVZ name tukiingalia sana tulikuwa yunajivunia khasa ilikuwa TV ya heshima na ustaarabu lakini leo ahh! Imekuwa TV ya kuiga maovu na kuyaonesha kwa jamii eti kwenda na wakati hatutaitazama aslaan.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.