STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 29 Januari, 2016
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amevitaka vilabu vya Mafunzo na Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU)ambavyo vinaiwakilisha Zanzibar katika mashindano ya vilabu yanayoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuhakikisha kuwa vinapata ushindi mkubwa katika michezo yao ya awali ambayo inafanyika hapa nyumbani mwezi ujao.
Akizungumza katika hafla fupi ya kuvikabidhi vilabu hivyo vifaa vya michezo ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya vilabu hivyo Ikulu leo, Dk. Shein aliwataka wachezaji wa vilabu hivyo kucheza michezo hiyo kwa kujiamini na kusisitiza kuwa uwezo wa kupata ushindi mkubwa wanao.
“lazima mkaze buti na mcheze kwa kujiamini ili mpate ushindi mkubwa kwa kufanya hivyo kazi itakuwa rahisi mtakapocheza ugenini hivyo kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele” Dk. Shein aliwaambia wachezaji na viongozi wa timu hizo waliohudhuria hafla hiyo.
Katika mashindano hayo, timu ya Mafunzo inashiriki mashindano ya klabu bingwa Afrika kwa kupambana na Timu ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC) kwenye Uwanja wa Amaan tarehe 13 Februari, 2016 na timu ya JKU ambayo inashiriki Kombe la Shirikisho itapambana na timu ya Gaborone United ya Botswana katika uwanja huo huo siku inayofuata ya tarehe 14 Februari,2016.
Katika mnasaba huo alitoa wito kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo pamoja na Baraza la Michezo kuangalia uwezekano wa kupanga viingilio vya michezo hiyo vitakavyowawezesha wananchi wengi kuangalia mechi hizo na kutoa hamasa kwa wachezaji wa timu zetu.
Dk. Shein alisisitiza kuwa vilabu hivyo kushiriki mashindano hayo ni heshima kubwa kwao kwa kuwa ni kati ya mashindano pekee ambapo Zanzibar inashiriki kama nchi ukiachia mashindano yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka la Nchi za Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) ambayo ni ya kikanda.
“Hivyo lazima tuitunze heshima hiyo kwa kujiandaa vyema na sisi sote tuna matumaini makubwa kuwa mutafanya vizuri na mnakwenda kushindana si kushiriki” Dk. Shein alieleza.
Alibainisha kuwa historia inaonesha kuwa timu za vikozi vya Ulinzi na usalama vimekuwa vikifanya vizuri katika michezo mbalimbali hivyo timu za Mafunzo na JKU hazina budi kuendeleza historia hiyo kwa kushinda michezo hiyo na kuingia hatua nyingine ya mashindano hayo.
Aliongeza kuwa pamoja na kushindana timu hizo hazina budi kuzingatia nidhamu zitakapokuwa mashindanoni pamoja na kudumisha urafiki na timu pinzani ambazo zote zinatoka katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Uchumi ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
“Michezo si uhasama bali inajenga urafiki na upendo baina ya mataifa na ni wajibu wenu kuendeleza urafiki miongoni mwenu wanamichezo na hatimae kati ya nchi zetu” Dk. Shein alisema.
Katika hotuba yake hiyo fupi kwa wanamichezo hao Dk. Shein alisisitiza tena dhamira ya Serikali ya kuimarisha sekta ya michezo kwa kuongeza kasi ya ujenzi na uimarishaji wa miundombinu ya michezo pamoja na upatikanaji wa vifaa vya katika sekta hiyo.
“Tutaendelea kuimarisha miundombinu katika sekta ya michezo na kuwapatia vifaa hata kama timu zetu hazishiriki mashindano makubwa kama haya ya CAF” alieleza Dk. Shein.
Alifafanua kuwa serikali itaendeleza ujenzi wa viwanja vya michezo na burudani kote Unguja na Pemba na hivyo kuwataka wananchi wasishangae watakapoona baadhi ya maeneo ya wazi yanatumika kujenga viwanja hivyo kwa matumizi ya wananchi wote.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ Mheshimiwa Haji Omar Kheri alimhakikishia Mheshimiwa Rais kuwa Wizara yake hasa Idara Maaalum zinatekeleza ipasavyo sera ya michezo pamoja na maagizo yake kuhusu uimarishaji wa michezo nchini.
Waziri huyo alizishukuru Wizara za Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo pamoja na Wizara ya Fedha kwa ushirikiano wao katika kufanikisha ushiriki wa timu hizo katika mashindano hayo.
“sisi tunaifanyia kazi sera ya michezo na maagizo yako ikiwemo lile la michezo ni sehemu ya kazi pamoja na hili la kuhakikisha ushindi kwa timu zetu zinazozishiriki mashindano haya ya CAF” alieleza waziri huyo.
Kwa upande wake, Mwenye kiti wa Baraza la Michezo Zanzibar (BMZ)Bi Sharifa Khamis alimshukuru Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa mchango wake mkubwa katika kuimarisha michezo nchini.
Alibainisha kuwa katika kuunga mkono jitihada hizo za Rais, tayari Baraza lake kwa kushirIkiana na Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati imepata hati za viwanja 5 katika eneo la Mnazi Mmoja ambavyo vitatumiwa kwa michezo mbalimbali.
Mwenyekiti huyo wa BMZ alifafanua kuwa Baraza pia linaangalia maeneo mengine zaidi ili yaweze kupatiwa hati na iwe rahisi kupata wafadhili kuyaendeleza maeneo hayo kwa ajili ya michezo.
Bi Sharifa alieleza kuwa tukio la ugawaji wa vifaa kwa timu hizo ni muendelezo wa jitihada za Mheshimiwa Rais la kuwapatia vifaa wanachimzo wa Zanzibar na kubainisha kuwa hadi sasa vilabu 18 vimeshafaidika misaada hiyo kutoka kwa mheshimiwa Rais.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu na Utawala Bora, Dk. Mwinyihaji Makame, Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk Abdulhamid Yahya Mzee, wakuu wa vikosi vya Mafunzo na JKU pamoja na Makatibu wakuu wa baadhi ya wizara.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822
No comments:
Post a Comment