Habari za Punde

Dk.Shein Azitaka Mahkama za Watoto Kuongoza Kasi ya Usikilizaji Kesi za Watoto.

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                                                           08 Januari, 2016
---
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein ametoa changamoto kwa watendaji wa mahkama za watoto nchini kuongeza kasi, ari na kubuni mbinu bora zaidi zitakazowezesha mahkama hizo kumaliza kesi zao haraka.

Katika hotuba yake mara baada ya kuweka jiwe la msingi la jengo la Mahkama ya watoto huko Mahonda katika mkoa wa Kaskazini Unguja leo, Dk. Shein amesema pale ambapo ushahidi wa kesi hizo upo hakuna sababu za mahkama kuchelewesha kesi hizo.

Hata hivyo alikiri kuwa uendeshaji wa kesi za udhalilishaji watoto umekuwa ukikumbana na mazingira magumu hasa pale watu wanaopaswa kutoa ushahidi mahkamani wanapokataa kufanya hivyo.

“Naamini mahakimu hawana nia ya kuchelewesha kesi hizo lakini ukweli ni kuwa kesi hizo zina mambo mengi magumu ikiwemo mashahidi kukataa kufika mahkamani kutoa ushahidi” Dk. Shein alisema.

Alifafanua kuwa ni kweli ucheleweshaji kesi za udhalilishaji watoto na wanawake unasababisha manung’uniko kutoka kwa wananchi na taasisi zinazofuatilia kesi hizo lakini amewahakikishia wananchi kuwa Serikali itaendeleza jitihada zake kuhakikisha haki za mtoto zinalindwa kwa mujibu Sheria ya Mtoto ya Zanzibar, Namba 6 ya mwaka 2011 pamoja na mikataba mingine ya kimataifa kuhusu haki za watoto.

Alibainisha kuwa ujenzi wa mahkama hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Miaka Mitano (2013-2018) wa Mapitio na Marekebisho ya Sheria ya Watoto ambao umelenga kulinda haki za watoto wenye matatizo ya kisheria.

Kwa hivyo “natoa wito kwa taasisi zote zinazohusika katika utekelezaji wa Mkakati huo kutekeleza wajibu wao ili waende sambamba na azma ya serikali ya kuimarisha utawala wa sheria na dhana ya utawala bora hasa suala la zima la kulinda haki za watoto kwa mujibu wa Sheria Namba 6 ya mwaka 2011” Dk. Shein alisisitiza.  

Katika hotuba yake hiyo Dk. Shein aliipongeza Idara ya Mahkama kwa kushirikiana na taasisi nyingine zinazoshughulikia kesi za udhalilishaji watoto kwa kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kuwa kesi hizo zinashughulikiwa haraka na kutolewa hukumu.

“Nimevutiwa sana na utaratibu wa Mahkama, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka pamoja na Jeshi la Polisi kukutana kabla ya kesi kuanza ili kuangalia mazingira halisi ya kesi kwa dhamira ya kufanikisha uendeshaji wa kesi mahkamani” alisema Dk. Shein.

Aidha Dk. Shein alisifu jitihada zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa na serikali na taasisi zisizo za kiserikali za kuelimisha jamii kuhusu vita dhidi ya udhalilishaji watoto na wanawake na kwamba matokeo ya jitihada hizo ni kuongezeka kwa utoaji wa taarifa dhidi ya vitendo vya udhalilishaji katika vyombo husika.

Hata hivyo alisisitiza kuwa “bado kuna kazi kubwa mbele yetu ya kuendelea kuelimishana juu ya kupiga vita udhalilishaji watoto na wanawake ikiwa ni pamoja na kusisitiza malezi bora ya asili kwa watoto wetu”

Katika maelezo yake kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Jaji Mkuu wa Zanzibar Mheshimiwa Omar Othman Makungu alieleza kuwa ujenzi wa mahkama hiyo kunafanya idadi za mahkama za watoto kufikia 3 ambapo moja ni ya Vuga katika mkoa wa Mjini Maghribi na Chake Chake ambayo itakuwemo katika jengo la Mahkama mjini Chake Chake katika mkoa wa Kusini Pemba.

Alisema ujenzi wa mahkama hiyo ambao umefadhiliwa na Shiriki la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF kwa gharama ya shilingi milioni 77 pamoja na vifaa kwa makisio ya awali unatarajiwa kukamilika mwezi Machi, 2016.

Hata hivyo alibainisha kuwa kufuatia gharama za ujenzi kupanda watahitaji fedha nyingine zaidi shilingi milioni 30 kumalizia jengo na kuiomba serikali kuwapatia fedha hizo pamoja na samani ili mahkama hiyo iweze kufanya kazi mara tu itakapomalizika.

Akizungumzia kuhusu uendeshaji kesi Jaji Mkuu alisema changamoto nyingi walizokuwa wakipambana nazo hivi sasa zimepungua kufuatia hatua mbali mbali zilizochukuliwa na idara yake na washirika wengine.

Alizitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na ushirikiano na idara nyingine kumeharakisha uendeshaji wa kesi, kuwepo kwa kituo cha urekebishaji wa tabia kwa watoto waliopatikana na makosa (community Rehabilitation Centre), kuanza kutumika kwa kanuni za uendeshaji wa sheria ya mahkama za watoto na kukamilika kwa utaratibu wa kukusanya ushahidi.       

Alizitaja hatua nyingine kuwa ni kupatiwa mafunzo mahakimu wa mikoa juu ya uendeshaji wa kesi za aina hii na kuwepo wakili kutoka Kituo cha Msaada wa Sheria kusaidia watoto wanaoshtakiwa mahkamani. 
       
Jaji Mkuu aliishukuru UNICEF kwa msaada wake huo pamoja na Kituo cha Masaada wa Sheria Zanzibar kwa kuhudumia hafla hiyo. 

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na mashirika ya kimataifa wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi.


Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.