Habari za Punde

Na Nyakongo Manyama
Maelezo
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kwa kushirikiana na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road wanatarajia kutoa elimu, huduma na vipimo vya bure vya magonjwa ya saratani ili kuiwezesha jamii kujikinga na ugonjwa huo nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo (Jumatano) Jijini Dar es Salaam Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Ulisubisya Mpoki huduma hizo za matibabu na vipimo vitaenda sambamba na maadhimisho ya siku ya saratani duniani inayoathimishwa ulimwenguni kote tarehe 4. Februari ya kila mwaka.

Aidha Dkt. Mpoki ailwataka wananchi kujitokeza kwa wingi ili wapate huduma ya kupima ugonjwa wa saratani katika Hospitali ya Ocean Road ili kujihadhari na maambukizi ya ugonjwa huo.

“Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kwa kushirikiana na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road tunapenda kuwaambia wananchi wote wajitokeze kupima ugonjwa huo ikiwemo saratani ya tezi dume kwa wanaume na saratani ya matiti kwa wanawake bila ya malipo” aliongeza Dkt. Mpoki.

Dkt. Mpoki amewataka watu wenye Ulemavu wa Ngozi (Albino) wajitokeze kwa wingi ili waweze kupata vipimo na matibabu ya saratani ya ngozi na kuwataka wajilinde ili wasipate miale ya jua inayoathiri ngozi zao na kupelekea maambukizi ya ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa Dkt. Mpoki alisema ugonjwa wa saratani huchangiwa zaidi na ulaji usiozingatia kanuni za afya,matumizi ya vilevi, uvutaji wa sigara na matumizi makubwa ya sukari.


Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Saratani Duniani mwaka huu ni 

TUNAWEZA, NINAWEZA. KWA PAMOJA TUWAJIBIKE KUPUNGUZA JANGA LA SARATANI DUNIANI.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.