Habari za Punde

Mshtakiwa kosa la kubaka binti wa miaka 12 aanza kujitetea adai kutohusika na tukio hilo

Na Salmin Juma, Pemba

MAHAKAMA ya Mkoa Chake chake, imeanza kusikiliza utetezi wa mshitakiwa Seif Abeid Mohamed (22) Mkaazi wa Jondeni Mkoani Pemba, alieshitakiwa kwa kosa la kubaka msichana wa miaka (12), ambapo alidai mbele ya mahakama kutohusika na kesi hiyo bali linaloendelea ni kutokana na chuki kwa baba wa mlalamikaji na ameweza kumpa kosa lisilomuhusu.

Alidai kuwa, hana mazoea na mlalamikaji na kumfahamu kwake ni kumuona njiani tu katika maisha yake anayoishi isipokuwa baba wa mlalamikaji ana hasira nae ndio alipoamua kumpa kesi hiyo ili kumtia mashakani.

Alidai, siku ya tukio hilo alikua akitoka Bandarini Kastam akienda Jondeni njiani alimkuta baba wa mlalamikaji na kumwambia kuwa anamchukulia mwanawe mshitakiwa huyo baada ya kumkatalia baba wa mlalamikaji alidai kuwa atamshitaki.

Mshitakiwa baada ya kukamilisha utetezi wake mwendesha mashitaka kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa mashitaka Pemba (DPP) Seif Mohamed Khamis, alimuuliza mshitakiwa, mlalamikaji anamfahamu mshitakiwa alidai kuwa anamfahamu kwa kumuona tu na masafa anayoishi mshitakiwa na anapoishi mlalamikaji ni mbali.

Hakimu wa mahakama hiyo, Khamis Ali Simai, alifunga ushahidi wa mshitakiwa huyo kutokana na mshitakiwa kudai kuwa hana shahidi wa kumleta mahakamani, shauri hilo limeahirishwa tena hadi  Novemba 9 mwaka huu mshitakiwa atakaporudi tena mahakamani hapo kwa ajili ya hukumu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.