Habari za Punde

Mama Mwanamwema Shein SMZ Itaendelea Kuzipatia Ushirikiano Taasisi Zote za Dini Nchini Biila ya Ubaguzi.

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuzipatia ushirikiano taasisi zote za dini bila ya ubaguzi kwa kuzingatia misingi ya Kikatiba na uhuru wa kuabudu kama ilivyoanishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
 Hayo yameelezwa na Mke wa Rais wa  Zanzibar Mama Mwanamwema Shein wakati alipokuwa na mazungumzo na viongozi na Waumini wa Madhehebu ya dini ya Kikristo huko katika ukumbi wa Nyumba za Wazee Sebleni.

Katika maelezo yake Mama Shein, alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba chini ya uongozi wa Rais Dk. Ali Mohamed Shein inathamini sana mchango wa waumini hao kwa maendeleo ya ustawi wa jamii.

Alisema kuwa jitihada za taasisi za madhehebu ya dini zinatambuliwa katika kuungana na Serikali katika kuwapatia wananchi huduma ambali mbali za kijamii zikiwemo afya na elimu.

Alieleza kuwa jamii inatambua na kuthamini sana jitihada za waumini hao za kuhubiri amani hapa nchini.

Hivyo, Mama Shein alitoa wito kwa waumini hao wasichoke na waendelee kuilinda amani kwa nguvu zao zote kwani pasipo amani hakuna maendeleo wana waumini hawawezi hata kumuabudu Muumba wao.

Aidha, Mama Shein alieleza kuwa vitendo vya ukatili na udhalilishaji vinavyosababishwa na baadhi ya watu vinatokana na kuyadharau maamrisho ya Mwenyezi Mungu na kuamua kumfuata shetani ambaye siku zote huwa anashawishi kufanya mambo maovu.


Pia, Mama Shein aliwasisitiza waumini hao kuwasimamia watoto na vijana ili wawe makini katika matumizi ya mitandao ya kijamii sambamba na kujiepusha na madawa ya kulevya na kutoshiriki katika vitendo vyote  vya kuvunja sheria.

Nae Mke wa Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mama Asha Balozi alisisitiza haja ya mashirikiano na akiahidi kuviunga mkono vikundi vya maendeleo ya akinamama hao.

Mapema Mama Fatma Karume nae alitumia fursa hiyo kueleza uhusiano wa kihistoria uliokuwepo kati ya waumini wa dini ya kikristo na dini nyengine hapa nchini  huku akiwasisitiza haumini hao kuzidisha mashirikiano na kuendeleza amani na utulivu uliopo hapa nchini.

Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa UWT Zanzibar Tunu Juma alitumia fursa hiyo kumpongeza Mama Shein kwa kukamilisha ziara hizo za shukrani katika Mikoa ya Pemba mnamo Novemba 5 hadi 8 mwaka huu na kuendelea katika Mikoa ya Unguja kuanzia Novemba  21 na kumalizia jana tarehe 24.

Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto Maudline Castico aliwaeleza waumini hao juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali katika kupiga vita suala la unyanyasaji wa wanawake na watoto na kuahidi kuwa waumini hao wataendelea kushirikiana na Serikali yao.

Nao Waumini hao walieleza kusikitishwa na kulaani kwa nguvu zote vitendo vya ubakaji wanavyofanyiwa watoto na kutaka juhudi zaidi ziendelee kuchukuliwa katika kupiga vita vitendo hivyo.

Aidha, walitumia fursa hiyo kueleza mafanikio na changamoto mbali mbali zinazowakabili pamoja na kueleza matumaini yao kwa kuendelea kumuunga mkono Dk. Shein na kusema kuwa yeye kuwa Rais wa Zanzibar wanajivunia sana.


Wakati wa mchakato wa Kampeni za Uchaguzi uliopita Mama Shein alikutana na Waumini hao wa Unguja na Pemba ambapo aliwanasihi kuliombea taifa ili lizidi kuwa na amani na kuingia katika mchakato huo kwa salama. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.