Habari za Punde

Acheni kuanzisha makundi kusaka urais 2020 andaeni wanachama kushinda uchaguzi - Wito

Na Mwantanga Ame

MKE wa Makamu wa Pili wa Rais, Mama Asha Suleiman Iddi, amewataka wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuacha kutumia Baraza la Wawakilishi kuanzisha makundi ya kutafuta Urais wa Zanzibar kwa mwaka 2020 na badala yake wafanye kazi ya kuwaandaa wanachama wa CCM wataoweza kukipatia ushindi chama hicho katika uchaguzi Mkuu ujao.

Mama Asha aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa dhamira ya kuwataka kujiandaa kuwasaidia wananchi katika majimbo waliyoshinda kwa kuona wake zao wanajiunga na umoja wa wake wa viongozi unaoongozwa na Mke wa Rais wa Zanzibar, Mama Mwanamwema Shein.

Mama Asha, alisema alisema Chama cha Mapinduzi hivi sasa kinakabiliwa na kazi kubwa ya kuona ni vipi itaongeza wanachama wataokiunga mkono katika uchaguzi Mkuu ujao, na sio kupata makundi ya kutafuta nani awe Rais wa Zanzibar, mwaka 2020.

Alisema hiyo ni kutokana na hivi sasa ndani ya Baraza la wawakilishi tayari kumeanza kujitokeza makundi yanayodaiwa kuanzisha mtandao wa kutafuta Rais wa 2020, jambo ambalo bado wakati wake.

Alisema uchaguzi Mkuu wa Zanzibar, hivi sasa umemalizika na Chama kinachoendelea kutawala ni cha CCM, ambapo Wajumbe wa Baraza hilo wanapaswa kuona kazi wanayoifanya ni kuwatumikia vizuri zaidio wananchi katika majimbo yao na sio kuwachonganisha kwa nani awe Rais kwani hayo sio maazimio ya ahadi zao wanazotaka kutimiziwa.

Alisema inashangaza kuona hali hiyo ndani ya baraza hilo imekuwa ikifanyika bila aibu kwa kuanzisha makundi ya ukanda ya kaskazini na ukusini jambo ambalo ni hatari kwa chama hicho hapo baadae.

Hata hivyo, Mama Asha, alisema kazi ya kumpata Rais hawataweza kuijua Wajumbe wa Baraza hilo kwa watu wanaowaandaa kwani hilo ni jukumu la Mwenyezi Mungu, ambaye ndie huamua nani awe kiongozi wa Zanzibar ifikapo mwaka 2020, ambapo hivi sasa tayari ameshamtambua.

Kutokana na hilo Mama Asha, alisema ni vyema wajumbe hao kuacha kufikiria kupata madaraka kwa kukiweka chama hicho katika chumba cha wagonjwa mahatuti (ICU) na badala yaje wafanyekazi kuitafuta serikali.

Alisema Umoja wa Wake viongozi utapostawi utawasaidia wajumbe wa Baraza hilo kuweza kupata nguvu ya kufanya kazi vizuri katika kuwatumikia wananchi badaa ya kusubiri serikali kuu nda makundi.

Alisema katika kulitekeleza hilo ni vyema kwa wajumbe hao kujikubalisha kuwatoa wake zao kujiunga na umoja huo, ili uweze kuwasaidia kuwafikishia maendeleo katika majimbo yao, kwa vile michango watayokuwa wanaitoa itawarejea wenyewe.

Hata hivyo, Mama Asha, aliwataka wajumbe hao kuona wanachangia kuanzisha kamati katika majimbo yao zitazoweza kusimamia kupiga vita vitendo vya udhalilishaji katika maeneo yao.

Alisema hilo ni jambo la msingi kwa hivi sasa kwa vile tayari kumekuwa na matukio mengi yanaojitokeza kwa Unguja na Pemba.
Nae, Mjane wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Mama Fatma Karume, amesema ni vyema kwa Wajumbe wa Baraza la wawakilishi kujitambua, kwani kuna watu wameanza kupiga kelele za kudai kutaka uhuru wakati tayari Zanzibar iko katika utawa tangu 1964.

Alisema Dk Shein tayari ameshakabidhiwa nchi na hawapaswi kumsakama kwa hilo kwa vile uongozi wake umetokana na kupata kura kutoka kwa wananchi.

Mama Asha ameambatana na wake wa viongozi katika ziara hiyo, ambapo leo wanatarajia kufanya mazungumzo na waumini wa dini ya kikristo kwa dhamira ya kuwashukuru kwa kukiunga mkono chama hicho katika uchaguzi mkuu uliopita.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.