Habari za Punde

Kampuni ya Pennyroyal na kampuni ya ujenzi ya MCC Wasaini ujenzi wa kijiji cha kitalii


Na Salum Vuai, MAELEZO

HATIMAYE kampuni ya Pennyroyal (Gibraltar) Ltd imetiliana saini mkataba wa muda mrefu na kampuni ya MCC Overseas Ltd kutoka nchini China kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kijiji cha utalii huko Matemwe Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Hafla ya utiaji saini makubaliano hayo, ilifanyika juzi Disemba 14, 2016 katika hoteli ya Park Hayyt mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Mkataba huo ulisainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa ‘Zanzibar Amber Resort’ inayoendesha mradi huo, Brian Thomson pamoja na Mwenyekiti wa kampuni ya MCC Overseas, Weiman Zou.

Kupitia mkataba huo wenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 330, kampuni ya MCCO Ltd itakuwa na jukumu la ukandarasi wa mradi wa ‘Amber Resort’, ambapo itajenga villa za kifahari, majengo ya makaazi (apartments) na hoteli tano kubwa zenye hadhi ya nyota tano.

Ujenzi mwengine utahusisha marina, visiwa vya kifahari, kiwanja kikubwa cha kimataifa cha mchezo wa golfu na huduma zinazoendana na mji wa kitalii.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Pennyroyal (Gibraltar) Ltd Brian Thomson, alisema awamu ya kwanza ya ujenzi huo inatarajiwa kuanza katika kipindi kifupi kijacho na unakadiriwa kumalizika mwaka 2020.

Aidha alieleza kuwa, mradi huo utatekelezwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa, vyombo, mashine na utaalamu wa hali ya juu ambao utazingatia uhifadhi wa mazingira ya ardhi na bahari.

Thomson alifahamisha kuwa ni matumaini ya kampuni yake kwamba mradi huo wa pekee Afrika Mashariki, utabadilisha na kuimarisha kwa kiasi kikubwa maisha ya wananchi wa Mkoa wa Kaskazini na Zanzibar kwa jumla.

“Tunafahamu mahitaji ya wananchi, hivyo tunaamini mradi utasaidia kutoa ajira za kutosha pamoja na kuwafundisha vijana taaluma mbalimbali ili kuwaandaa na nafasi za kazi zitakazozalishwa,” alieleza Mkurugenzi huyo.

“Tukio hili la kusaini mkataba huu limeweka historia kwa kampuni yetu kuithibitishia dunia kuwa uwekezaji mkubwa kama huu utaleta mafanikio makubwa yatakayoibadilisha Zanzibar katika ramani ya dunia kwa kuwa na watalii wenye hadhi ya juu na kuizidishia Zanzibar haiba yake ya asili,” alifafanua.

Aliishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dk. Ali Mohamed Shein, kwa kuukubali kwa dhati mradi huo, pamoja na jitihada zake za kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazotokea katikati ya utekelezaji wake.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa MCCO Weiman Zou alisema kampuni yake yenye uzoefu wa ujenzi wa miradi mikubwa duniani, itahakikisha inaifanya kazi hiyo kwa ufanisi na viwango vinavyostahili.

Alisema kuteuliwa kwa kampuni yake kutekeleza ujenzi huo, ni fahari pia kwa nchi yake, ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikisaidia jitihada za serikali ya Zanzibar kuleta maendeleo ya kila sekta ikiwemo miundombinu.    

Aliishukuru Pennyroyal kwa kuiamini kampuni yake, na kueleza kuwa haitajuta wa uamuzi wake huo.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Khamis Mussa Omar, aliihakikishia kampuni inayofanya uwekezaji huo, kwamba serikali ya Zanzibar itaendelea kuiunga mkono na kuipa kila msaada itakaohitaji katika kufanikisha mradi huo.

Alisema kutokana na ukubwa wa mradi huo, kutakuwa na fursa nyingi kubwa za ajira, wakati na baada ya utekelezaji wake, ikiwemo upatikanaji wa soko la bidhaa za kilimo, uvuvi na huduma mbalimbali za kitalii ikiwemo usafiri.

Mussa alisema kuchelewa kuanza kwa mradi huo kumetokana na ubunifu mpana zaidi wa wawekezaji hao, ambao awali walihitaji ekari 60 za ardhi, na sasa wameomba zaidi ya ekari 400.

“Kuchelewa kwa namna hii ni katika matarajio chanya hivyo kwani sasa wawekezaji wanafikiria kuimarisha zaidi mradi huu, jambo ambalo ni la manufaa,” alisema.

Alieleza kufarijika kwake na serikali, kutokana na ujenzi huo kukabidhiwa mkandarasi kutoka Jamhuri ya Watu wa China, akisema nchi hiyo imekuwa rafiki wa kweli kwa Zanzibar tangu Mapinduzi ya Januari 1964.

IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR
TAREHE 15 DISEMBA, 2016

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.