Habari za Punde

Nasiha za Bi Hekima: Tusifumbie macho mambo yasiyostahili

Na Bi Hekima

Ijumaa iliyopita nilijaaliwa kusali katika Msikiti wa Chuo Kikuu Dar es Salaam. Kutokana na nafasi kuwa finyu baadhi yetu, wake kwa waume husali nje. Jambo mmoja linalonitia moyo ni kuona umati wa watoto wengi wa shule za msingi wakija msikitini siku za Ijumaa hususan. 

Tulikuwa tumetenganishwa na mpaka wa viti wanawake upande mmoja na wanaume. Miongoni mwa waliokuja kusali ni wanaume wawili walielekea kuwa wenye asili ya afrika kaskazini. Wakasali sunna na kuketi kusikiliza hotuba ya Ijumaa. 

Mara mmoja wao akamwita mtoto wa kiume aliyekuwa darasa la pili hivi na yule mtoto bila kusita akanyanyuka na kwenda. Akakaa ubavuni akawa anakumbatiwa na kupapaswa papaswa, mwanzo kama anavyofanywa mtoto lakini nikaanza kupata wahka nilivyoona kuwa hamalizi kumtia maungoni.

 Zaidi akawa sasa anafanya kama mchezo wa kumpiga na yule bwana mwengine kwa mkono wake au wa mtoto au kumtekenya halafu wanafanya kama kumuadhibu hivyo kugusana gusana. Toka mtoto kashikwa ubavuni mwisho akawa kalala mapajani wakati wote kazungushiwa bonge la HUG. 

Hakuna katika wanaume wa hapo alopepesa kwa kilichotokea. Baadhi ya wanawake wakitizama halafu wakatizamana lakini hakuna alosema au kufanya lolote. Watoto wenzake wakiangalia wengine wakitamani wangeitwa na wao bila ya shaka kuonyeshwa 'mapenzi' kwa maana ya affection. Mimi.nlikerewa na tukio lote maana nilona si sehemu yake: tumekuja ktk sala si kucheza tena mchezo wa tekenya baina wakubwa na mtoto

Baada muda nikamwita mmoja ya mtoto aniitie ustadh alikuwa akipanga viti. Nilimwambia kuwa kile kinachofanyika hakiendani na kuwepo sisi pale. Tumekuja kusali na suala la kuingiliana maungoni kiasi kile ilikua si vyema na si sehemu yake. Akaenda ustadh huyo bila kuwambia wale watu chochote. Kwa bahati yule mtoto akageuka nkamwita.  Alipokuja mtoto nkataka kujua 'yule mtu mzazi wake' (maana mtoto alikuwa mweupe) akajibu hapana;  'uncle wako,?' Hapana. Rafiki wenu wa familia? Hapana. 'Unamjua?' Hapana. 

Nkashangaa na kumuuliza,'inakuaje mtu humjui anakwita unakwenda bila kuhoji?'au 'inakuaje mtu humjui anakuingilia maungoni, anakutekenya anakulaza mapajani husemi kitu?'

 Akainama chini. Nkamwambia huo ndio mwanzo wa hadithi anazosikia za watoto kuharibiwa. Nkamwambia, 'ondoka ukakae na wenzako'. 

 Kwa bahati tulipomaliza kusali yule ustadh alirudi na mtu mwengine akaniambia nimfahamishe kile nilichomwambia. Nkamfahamisha na kumsihi wawe na mafunzo kabla au baada ya sala kuwatanabahisha watoto juu ya masuala kama haya maana watoto huponzwa na vitu vidogo. 

Nasaha zangu ni kuwa tusifumbie macho mambo ambayo hayastahili hasa yanayopindukia mipaka. Imekuwa heri wale waliomwita mtoto yule walikua 'tofauti' hivyo mara moja mtu umeweza kutanbahi kuwa mbona picha haiendi...je, wangefanya hivyo watu walofanana na mtoto?  Tuseme na watoto. Tuwafundishe kujimiliki na miili yao. Tuwafundishe wanaweza kumuitika mkubwa bila ya kujiweka mashakani. Aweze kutambua hiki kinafaa hiki hakistahili na kujihami.

 Sikitiko kubwa zaidi kwangu kwa tukio hili ni nanma katika jamii zetu tunaona tunayotaka kuyaona na kufumbia yale tusotaka kuyatambua kuwa yanatokea. Watu wanatizama hakuna anayefanya jambo au kumnusuru mtoto au.mnyongr. Wata kaa pembeni kulaumu au kusikitika lakini kwao vigumu kuchukua hatua kama jambo linaharibika. Hiyo ni dalili ya imani dhaifu. Na wala watu wasidhani kuchukua hatua ni kuhukumu watu na kuwajaza makwaju, la! 

Tuanze kwanza kuwatanabahisha  nini sahihi na kipi kina walakin inafaa kujiepusha nacho. Mwezi Mungu atupe utambuzi na hifadh dhiri ya kila la kudhuru.. Wasambazie walezi na wazazi wa watoto wake kwa waume wapate kuongea na watoto wao. Muhimu zaidi wazazi na wawalezi wawaonyesha watoto wao mapenzi nyumbani ili wasiwe na njaa ya kuhadaiwa na mtu mwengine kutokana na kiu ya 'kuonekana, kutakiwa, kufarijiwa!' Allah Aalamu ( Allaah ndie ajuae)No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.