Habari za Punde

Zaidi ya Shilingi Bilioni 200 Kuwanufaisha Vijana Nchini.


Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia,Profesa Joyce Ndalichako(wa pili kushoto) akiwasili katika taasisi ya Chuo cha Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela(NM-AIST) kuzindua mradi wa Vituo vya umahiri katika utafiti wa kilimo na magonjwa ya binadamu pamoja na mradi wa kuongeza ujuzi kwa kazi za uzalishaji zinazoleta tija uliofadhiliwa na Benki ya Dunia,kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Arusha,Mrisho Gambo,Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya NM-AIST,Profesa David Mwakyusa na Makamu Mkuu wa taasisi hiyo,Profesa Karoli Njau.

Waziri wa Elimu ,Mafunzo na Ufundi Profesa Joyce Ndalichako (wa pili kulia) akipata  maelekezo juu ya utendaji wa Kituo hicho

Waziri wa Elimu ,Mafunzo na Ufundi Profesa Joyce Ndalichako akizindua mradi wa Vituo vya Umahiri katika utafiti wa kilimo na magonjwa ya binadamu kulia ni Mkurugenzi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania,Malawi ,Burundi na Somalia Bella Bird.
Filbert Rweyemamu,Arusha
Benki ya Dunia imetoa Sh 200 Milioni  ili kuwezesha miradi ya elimu na ujuzi kwa ajili ya kazi zinazoleta uzalishaji wenye tija pamoja na vituo viwili vya umahiri vya kikanda vitakavyofungua ajira kwa vijana mara baada ya kuhitimu elimu.

Akizungumza katika uzinduzi wa miradi hiyo,Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia,Profesa Joyce Ndalichako alisema kuwa miradi hiyo itasaidia kuongeza watu wenye ujuzi wa kati ambao watafanya kazi katika sekta za kilimo,utalii,ujenzi ,nishati na madini.


Alisema kuwa miradi iliyofadhiliwa ni pamoja na vituo vinne vya umahiri katika masuala ya utafiti wa kilimo na magonjwa ya binadamu pia ipo miwili iliyochini ya taasisi ya Chuo Kikuu ya Nelson Mandela pamoja na vituo vingine viwili vilivyopo katika Chuo cha Kilimo cha Sokoine(Sua).


Mkurugenzi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania,Malawi ,Burundi na Somalia, Bella Birds alisema kuwa uboreshwaji wa rasilimali watu kwa kuongeza ujuzi uliokosekana utasaidia taifa kufikia malengo yake ya kufikia uchumi wa viwanda.


Bella alisema inakadiriwa kuwa vijana milioni 1 huitimu katika vyuo na kuingia katika soko la ajira kila mwaka hivyo anatarajia kuwa nafasi za ajira kwa vijana hao zitatengenezwa na sekta binafsi iwapo zitashirikiana vyema na serikali .


Makamu wa Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela Karoli Njau alisema kuwa mradi huo utasimamiwa kwa makini ili kuhakikisha kuwa malengo yanafikiwa hususan katika vituo vya umahiri pamoja na mradi wa ujuzi.


Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi  Tanzania (TPSF), Godfrey  Simbeye amesema kuwa kulikua na upungufu mkubwa wa watu wenye ujuzi nchini kutokukidhi mahitaji ya soko la ajira hivyo kulazimu waajiri kuajiri watu kutoka nje jambo linalogharimu fedha nyingi hivyo mradi huo utasaidia vijana 30,000 kupata ujuzi utakaokidhi mahitaji ya soko la ajira.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.