Habari za Punde

ZURA yawatoa wasiwasi wananchi kuhusu upungufu wa mafuta nchini

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa huduma za nishati na maji Zanzibar (ZURA) Haji Kali Haji akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusiana na hali ya upatikanaji wa mafuta Zanzibar huko Ofisini kwake Maisara Zanzibar  (picha na Kijakazi Abdalla –Maelezo)

Na Mwashungi Tahir         Maelezo Zanzibar      

MKURUGENZI Mkuu Mamlaka  Ya Udhibiti Wa Huduma Za Nishati Na Maji Zanzibar(ZURA) Haji Kali Haji  aliwataka wananchi kuondoa wasiwasi kuhusu tatizo la upungufu wa mafuta nchini kuwa yapo ya kutosha.

Alisema mafuta yapo ya kutosha ingawa kwa siku mbili kulijitokeza upungufu wa mafuta aina ya dizeli  na hii ni kutokana na kazi ya usambazaji katika wa mafuta hayo katika  vituo.  

Akizungumza na waandishi wa habari hizi huko ofisini kwake Maisara amesema wananchi hawatokuwa na tatizo hilo kwa upande wa dizeli na kuahidi baada ya siku mbili tatizo hili litaondoka kabisa.

“ Hali ya sasa ya mafuta hapa Zanzibar itaendelea kuweko na hawategemei  kuadimika  badala ya kuwepo mafuta ya kutosha na kuweza wananchi kujipatia huduma hii bila usumbufu”Alieleza mkurugenzi huyo.

Aidha alisema   kwa upande wa Kampuni ya GAPCO mafuta aina ya dizeli yapo lita 39,112 na vile vile watapokea mafuta mengine yaliyokuwa ya kampuni Zanzibar Petrolium (ZP) LITA 168,000 za dizeli.

Pia amesema kwa upande wa Petrol kampuni hiyo ya Gapco ina lita 405,000, na kwa upande wa Kampuni United Group kwa mwezi huu wa Septemba ina lita 2,267,000 za Petrol na lita 1,91,424 za mafuta aina yaq dizeli  na mafuta ya taa lita 629,000.

Kwa upande wa kampuni ya Zanzibar Petrolium (ZP) Mkurugenzi amesema lita 7,000,00 za Petrol wakati  Dizeli kampuni hiyo ina lita 800,000 na kwa upande wa mafuta ya taa wana lita 250,000.

Akiendelea kwa kusema katika mwezi wa Oktoba Kampuni ya ZP watakuwa na lita 1,200,000 za Petrol wakati mafuta ya dizeli watakuwa na lita 800,000 na mafuta  ya taa lita 250, 000.

Amesema kwa kipindi hiki cha miezi miwili Kampuni ya AUGUSTA ENERGY kutoka Switzerland  iliyoshinda zabuni ya uletaji mafuta Zanzibar itaingiza mafuta jumla ya lita 9,57,116 za Petrol na lita 7,867.538 za mafuta aina ya dizeli.

Na kwa upande wa Pemba , MT Ukombozi ilishusha mafuta lita 360,000 za dizeli na lita 400,000za mafuta ya Petrol.

Mkurugenzi huyo amesema kwa upande wa mafuta ya ndege Kampuni ya PUMA imeingiza jumla ya lita 2,300,000 kwa mwezi huu .

Pia amewahakikishia wananchi kuwa hawatopata usumbufu tena tayari Kampuni ya AUGUSTA ENERGY imeleta mafuta ya ziada tani 200 za Petrol  na tani 150 za Dizeli  mafuta ambayo kwa sasa yamo katika meli hiyo ikiwa ni ziada ya yale wanayotakiwa kuleta Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.