Habari za Punde

ZAECA yaokoa mashamba 30 ya eka tatu yaliotaka kufichwa


NA ZUHURA JUMA, PEMBA

ZAIDI ya shilingi milioni 84.7 zimeokolewa na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA) Kisiwani Pemba, kwa kuyaibua mashamba ya mikarafuu 30 ya Serikali, yaliyodaiwa kufichwa wakati wa zoezi la ukodishaji ulipokuwa ukiendelea.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Chake Chake, Mdhamini wa Mamlaka hiyo Pemba, Suleiman Ame Juma alisema, mashamba hayo waliyafichua baada ya watendaji wake kufanya uchunguzi wa kina, wa mashamba hayo ya mikarafuu.

Alisema kuwa, baada ya kufanya uchunguzi huo, walibaini kwamba jumla ya shilingi milioni 84,700,000 zingepotea na kuishia mikononi mwa wachache, ingawa walifanikiwa kuziokoa, kutokana na kufichwa kwa mashamba 30 ya eka tatu tatu ya Serikali, katika maeneo tofauti ya kisiwani Pemba.

“Zaidi ya mashamba 30 ya mikarafuu ambayo yalionekana kama sio ya serikali, lakini baada ya uchunguzi wetu  tumeyabaini, kwamba ni ya serikali na tumefanikiwa kuziokoa fedha hizo baada ya kukodishwa”, alisema Suleiman.

Alifafanua kuwa, kuna mashamba yamekuwa yakifichwa na baadhi ya watendaji au watu wa kawaida, na kuonekana kama sio ya serikali, ambapo watendaji mbali mbali serikalini, hutumia mwanya huo kwa kuyatumia wao, jambo ambalo ni kosa kisheria.

“Kwa kweli mashamba yanafichwa kwa lengo la kuyatumia kwa shughuli zao binafsi, lakini tutaendelea kuchunguza, ili kuondoa suala zima la uhujumu wa uchumi, kama moja ya kazi zetu”,aliongeza.

Alieleza kuwa, kama hadi sasa Wizara husika imeshaingiza shilingi milioni 900.661, kwa ukodishaji wa mashamba ya serikali, basi mchango wa ZAECA, baada ya kuyaibua mashamba hayo 30 kati ya 1,451, ni shilingi miloni 84.7, ni mchango wetu.

Alisema walizipata taarifa hizo, baada ya kuhojiana na wananchi na wengine kufika ofisini kwao kutoa taarifa, juu ya uwepo wa mashamba ya mikarafuu ya serikali, kwenye maeneo ambayo zoezi limeshapita.

Tayari mashamba ya mikarafuu ya eka tatu tatu 1,451 yameshakodishwa na wizara ya Kilimo, Maliasiali, Mifugo na Uvuvi Pemba, na laiti kama waliokodi wengeshalipa fedha zote hizo, serikali ingejipatia wastani wa zaidi ya shilingi bilion 2.393.

Ingawa hadi sasa katia fedha hizo ziliotarajiwa kupatikana, hadi Oktoba 17, ni shilingi bilioni 1.492 zilizokuwa hazijalipwa na wanchi mbali mbali waliokodia mashamba ya mikarafuu ya serikali kisiwani Pemba.

 Zoezi la ukodishaji wa mashamba ya mikarafuu kisiwani Pemba, lilianza mwezi Julai mwaka huu, ambapo jumla ya mashamba 1,451 yalishakodishwa, kati ya mashamba 1,525 yaliotarajiwa kuibuliwa kabla ya kuanza kwa zoezi la ukodishaji.

                                                                                        

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.