Habari za Punde

Waziri Aboud: Bei mpya ya karafuu bado sana



NA HAJI NASSOR, PEMBA

WAZIRI wa Nchi Afisi ya Makamu wa Pili wa rais Zanzibar Mhe: Mohamed Aboud Mohamed, amesema bado serikali haijafikiria, suala la kuongeza bei mpya ya zao la karafuu, na kuwataka wananchi na wakulima kuridhika na bei iliopo kwa sasa.

Alisema, serikali hufika wakati hulifidia ZSTC kutokana na kujiendesha kihasara, hasa kutokana na bei ilipo sasa ya shilingi 14,000 kwa kilo moja, ambao inambeba mkulima kwa kupata asilimia 80 ya bei hiyo.

Mhe: Aboud alieleza hayo, kabla ya kulitembelea shamba la serikali lililoko Makuwe wilaya ya Wete, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kukagua shughuli za uchumaji na uuzaji wa zao la karafuu, linaloendelea kisiwani Pemba.

Alisema ZSTC halifanyi biashara ya karafuu na wananchi, bali ni kutekeleza agizo la serikali kuu, kuwahudumia wananchi na hasa wakulima wa zao la karafuu, ili kutimiza malengo yao kwenye sekta hiyo.

Alisema tayari serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwajali wananchi wake, imshajidhatiti kuwa haitoshusha bei iliopo sasa, hataka kama soko la dunia bei itashuka.

Hivyo, Waziri Aboud alisema, kutokana na ZSTC kujiendesha kihasara na wakati mwengine kulazimika kuomba kuwezeshwa na serikali kuu, suala la kupandisha bei mpya kwa sasa bado halijakuwa la kuwaweka kitako na kulizungumza.

“Bei iliopo sasa ya zao la karafauu, ipo kwa ajili ya kuwaneemesha zaidi wakulima wetu, na serikali imeshatamka mara kwa mara kuwa, bei hiyo haitoshushwa, maana vyenginevyo, ni kuwaumiza wakulima wetu”,alisema.

Katika hatua nyengine Waziri Aboud, aliitaka Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi kupeleka mpango kazi wa kuliimarisha shamba hilo la Makuwe, ili liimarike zaidi.

Alisema shamba hilo ambalo ni tegemeo, kwa sasa linaonekana kuanza kuchakaa kwa miti yake ya matunda na biashara, hivyo lazima uongozi wa Wizara, ukae na wataalamu wake, ili wawe na andiko la kuliimraisha.

“Sasa inaoenekana miti kama mikarafuu imeshakuwa mikongwe, sasa hebu tuleteeni mpango maalum wa kitaalamu, mutuombe ili kuliimarisha, maana hii ndio hazina yetu”,alisema.

Katika hatua nyengine Waziri huyo kutoka Afisi ya Makamu wa Pili wa rais, Mhe: Mohamed Aboud Mohamed, amewataka wale waliokodi mashamba ya mikarafuu ya serikali, kufanya hima kurejesha fedha hizo.

Alisema kama kunachangamoto iliojitokeza baada ya zoezi la ukodishaji kukamilika, wafike kwa wahusika ambao ni Wizara ya Kilimo, ili kufanya mazungumzo ambayo yatasababisha kuondoa mivutano.

Mapema Mkuu wa Idara ya Misitu kisiwani Pemba, Said Juma Ali, alimueleza waziri huyo, kuwa shamba hilo lenye hekta 79.7 linaundwa na ploti 10, ambapo ndani yake mna mashamba sita yaliokwisha kodiwa kwa thamani ya shilingi milioni 294.8.

Alisema kati ya fedha hizo, zilizokwisha lipwa na waliokodi ni shilingi milioni 154, ambapo shamba hilo linaiingiza mapato makubwa serikali, maana misimu iliopita ilianza na shilingi milioni 80, na sasa kufikia shilingi milioni 294.8.

Mmoja kati ya wananchi waliokodi mashamba ya serikali, Jecha Mohamed Faki, aliomba serikali kumuongezea muda wa kurejesha fedha alizotakiwa kulipa, kutokana na msimu kuingiliwa na mvua.

Alisema, alikodi mashamba sita ya serikali kwa thamani ya zaidi ya shilingi milioni 217, na tayari wastani wa shilingi milioni 120, amesharejesha, ingawa ujio wa mvua zimesitisha uwanikaji na uvunaji.

Mapema Mdhamini wa ZSTC Pemba, Abdalla Ali Ussi, aliwataka wananchi na wamiliki wa mashamha ya mikarafuu, kuendelea kufuata taratibu, ikitokezea mchumaji ameangua mkarafuu.

Alisema ZSTC imeshakabidhi kiasi kikubwa cha fedha kwa Shirika la Bima, kwa ajili ya kuwafanyia tathimini wananchi walioanguka wakati waliokoa zao la taifa na kisha kulipwa.

“Hivi sasa, tunao tayari idadi ya watu 60 kwa Mkoa wa kaskazini Pemba, pekee wakiwa wameshanguka kutoka juu ya mkarafuu, hivyo wakitokea wengine waripoti kwa sheha, wapite Polisi na waende hospitali na kukusanya taarifa zao”,alisema.

Wakati huo huo Waziri huyo na ujumbe wake, ulikagua kitalu cha miche ya aina mbali mbali na wanakaya masikini wa shehia ya Mtambwe kaskazini, waliojifufua upya, baada ya kitalu chao cha awali kutiwa moto.


Mratibu wa TASAF Pemba Mussa Said Kisenge, alisema kwa hatua za awali wanakaya hao maskini, waliigawa bure miche kwa wananchi, ingawa kwa mvuno wanatarajia kupanga namna ya kuwauzia ili nao kurejesha gharama zao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.