Habari za Punde

Watendaji taasisi za Umma watakiwa kuepuka visasi

  Katibu Mkuu Mpya wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Kulia aliyevaa Shati la Kitenge Nd. Shaaban Seif  Mohamed akipokea Taarifa ya utekelezaji wa Muongozo pamoja na Majukumu ya Ofisi hiyo kutoka kwa Katibu Mkuu aliyepita Dr. Idriss Muslim Hijja aliyehamishiwa Wizara ya Elimu hivi sasa.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed kati kati akiendesha Kikao cha Makabidhiano ya Taarifa ya utekelezaji wa Muongozo pamoja na Majukumu ya Ofisi hiyo kufuatia mabadil;iko ya Makatibu Wakuu wa Wizara za SMZ yaliyofanywa hivi karibuni na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein.
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Dr. Idriss Muslim Hiija akitoa shukrani zake kwa Viongozi na Watendaji wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Vuga Mjini Zanzibar aliyokuwa akiifanyia kazi kwa kipindi cha Miezi Mitano.
Katibu Mkuu Mpya wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Shaaban Seif  Mohamed  akizungumza na Viongozi na Watendaji wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar mara baada ya kukabidhiwa utekelezaji wa Muongozo pamoja na Majukumu ya Ofisi hiyo.
Picha na – OMPR – ZNZ.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed  ametahadharisha kwamba kufanya kazi kwa visasi kati ya Viongozi na Wafanyakazi wa Taasisi za Umma ni jambo baya linalosababisha kukosekana kwa ufanisi wa uwajibikaji katika maeneo ya kazi.
Alisema nia safi inayohitajika kupatikana miongoni mwa nyoyo za Viongozi na Watendaji wao katika Taasisi za Umma ndio silaha pekee itakayoiwezesha Serikali kupitia Taasisi hizo kuwajibika vyema katika mfumo wa kuwahudumia  vyema Wananchi wake.
Waziri Mohamed Aboud Mohamed alitoa tahadhari hiyo wakati wa kikao Maalum cha makabidhiano ya Taarifa ya utekelezaji wa Muongozo pamoja na Majukumu ya Wizara yaliyofanywa kati ya Katibu Mkuu aliyepita wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Dr. Idriss Muslim Hijja na yule aliyeteuliwa Nd. Shaaban Seif  Mohamed kufuatia mabadiliko ya Wizara na Taasisi za Serikali yaliyofanywa na Rais wa Zanzibar hivi karibuni.
Alisema jambo la msingi wakati inapotokea changamoto ndani ya uwajibikaji ni vyema kwa Watumishi hao wa Serikali kukaa pamoja katika kuitafutia ufumbuzi changamoto hiyo huku wakijiepusha na adui mkubwa wa fitina na majungu yanayoviza utendaji uliotukuka.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza na kuwashukuru Viongozi, Maafisa na Watendaji wote walio chini ya Ofisi hiyo kwa jitihada zao za kazi zilizopelekea ufanisi wa Wizara unaoonekana kwenye uwajibikaji wa jumla jambo ambalo linapaswa kuendelezwa.
Aliwakumbusha Viongozi na Watumishi wa Taasisi za Umma kwamba mabadiliko ya utendaji katika Wizara na Taasisi za Umma ni utaratibu wa kawaida unaopaswa kueleweka na watendaji hao sambamba na kuukubali kuufanyia kazi kwa mujibu wa Katiba na Sheria zilizopo hapa Nchini.
Mheshimiwa Mohamed Aboud alieleza kwamba mabadiliko ya utendaji huo wa Serikali umo ndani ya Katiba ya Zanzibar  ya Mwaka 1984 ambao humpa mamlaka Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar kuutekeleza wakati na saa yoyote pale anapohisi inahitajika kufanya hivyo.
Akitoa shukrani zake Katibu Mkuu aliyepita wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Dr. Idriss Muslim Hijja ambae kwa sasa ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar  alisema kipindi chake kifupi cha Utumishi ndani ya Miezi Mitano kimemuondoshea hofu ya Uwajibikaji wake ndani ya Ofisi hiyo kutokana na msaada mkubwa alioupata kutoka kwa Viongozi na Watendaji wake.
Dr. Idriss alisema Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ina  watendaji wenye upeo mkubwa wa kufikiri na kufanya kazi kwa nguvu na uzalendo uliyojidhihirisha machoni mwake hasa wakati yanapojitokeza masuala ambayo yanahitaji kutekelezwa mara moja na wakati hayamo katika muongozo na ratiba za kawaida za kazi.
Alisema hali hiyo wakati mwengine hujitokeza katika vipindi visivyotarajiwa hasa ikizingatiwa kwamba  Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ndio inayoratibu utendaji wote wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Naye kwa upande wake Katibu Mkuu Mpya wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Shaaban Seif  Mohamed alisema anajivunia Timu imara iliyopo ndani ya Ofisi yake akitarajia wazi kwamba atatekeleza majukumu yake kwa kujiamini.
Hata hivyo Nd. Shaaban alisema Watendaji lazima waendelee kupenda kazi ili kuondoa hofu iliyojengeka miongoni mwa Viongozi Wakuu ya kuona baadhi ya Watumishi wa Wizara pamoja na Taasisi za Umma hawapendi kufanya kazi.
Alisema jambo hili limekuwa likilalamikiwa sana na Viongozi hao la kufanya kazi kwa mazoea ambalo kwa sasa wakati umefika kulipiga vita ili liwe historia miongozi mwa Watumishi hao.
Dr. Idriss Muslim Hijja anayewajibika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa sasa pamoja na Nd. Shaaban Seif  alyeanza uwajibikaji Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ni miongoni mwa Makatibu Wakuu wa Taasisi za Serikali walioteuliwa hivi karibu na Rais wa Zanzibar kushika nyadhifa hizo nzito za Serikali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.