Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein akitoa risala ya kuukaribisha Mwezi mtukufu wa Ramadhan kwa Wananchi wa zanzibar na tanzania kwa ujumla katika ukumbi wa Ikulu Mjini Zanzibar leo,pia amewataka waumini wa Dini ya Kiislamu na Wananchi kuwa na mashirikiano ya pamoja na kumcha Mwenyeezi Mungu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein ametoa wito kwa wafanyabiashara wa jumla
na reja reja waitumie vyema azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya
kuwapunguzia ushuru wa bidhaa za chakula katika mwezi wa Ramadhani, ili
wananchi wapate bidhaa hizo kwa bei nafuu.
Alhaj Dk. Shein aliyasema
hayo katika risala maalum aliyoitoa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari
katika kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani mwaka huu wa 1439 Hijria sawa na
mwaka 2018 Miladia.
Katika risala yake hiyo,
Alhaj Dk. Shein aliendelea kuwakumbusha wafanyabiashara kujitahidi kadri wawezavyo
ili wasipandishe bei za bidhaa bila ya sababu za msingi au kuwauzia wananchi
bidhaa zilizopita muda wake wa matumizi.
Alieleza kuwa wafanyabiashara
wanapaswa kujitahidi kuwa waadilifu, waaminifu na kutenda haki katika kufanya
biashara zao pamoja na kuhakikisha kuwa vipimo vyao vya kuuzia bidhaa ni vya
halali kwani ni kinyume na sheria watu kudhulumiana katika vipimo.
Kutokana na hali hiyo,
Alhaj Dk. Shein aliziagiza Taasisi zinazohusika kulisimamia vyema jambo hilo na wasichelee kuwachukulia
hatua za kisheria wale wote watakaobanika, kufanya biashara kinyume na sheria,
kanuni na taratibu za nchi.
Aidha, Alhaj Dk. Shein
aliwahimiza wananchi kujiandaa na Ramadhani kwa kufanya zaidi mambo mema na
ibada za Saumu, Sala na utoaji Sadaka katika mwezi huo wote sambamba na
kuzidisha kusoma Qur-an na kuielewa pamoja na Hadith za Bwana Mtume Muhammad (S.A.W),
ili waweze kuzitekeleza ibada zao vizuri.
Pia, Alhaj Dk. Shein
alisisitiza kuwa katika mwezi wa Ramadhani himizo linatolewa katika kuzidi
kutendeana wema na ihsani na kusisitiza kuwa utoaji wa sadaka ni jambo la
msingi ili wenye kipato kidogo nao wawe wenye furaha katika mwezi huo.
Alisisitiza haja ya
kufanya mambo yatakayoleta faida, yatakayolinda maadili na kutoa mafunzo mema
kwa watoto huku Alhaj Dk. Shein akihimiza ucha Mungu ili mwezi wa Ramadhani
uache neema katika jamii pamoja na kuhudhuria kwa wingi katika darsa.
Pamoja na hayo, Alhaj
Dk. Shein alieleza kuwa Ramadhani mwaka huu imekuja ikiwa bado msimu wa mvua za
Masika unaendelea hivyo, aliwaomba wananchi kwa umoja wao washirikiane katika
kuiweka miji yao katika usafi ili wajiepushe na janga la maradhi ya
kipindupindu pamoja na maradhi mengine ya miripuko.
“Tutakapojitahidi
kuchukua tahadhari ya kuweka mazingira yetu safi na kufuata taratibu zote za
kinga, hapana shaka tutayaepuka mardhi mengi yanayotokana na uchafu, naamini
kwamba Allah naye atatusaidia”,alisisitiza Alhaj Dk. Shein.
Aidha, Alhaj Dk. Shein
aliwanasihi wananchi wasiowajibika na Saumu kama kawaida yao washirikiane na
wenzao wanaofunga na waendelee kuwa wastahamilivu na kuitumia fursa hiyo vyema
bila ya kufanya vitendo vya karaha ya kuwaudhi wengine.
Hivyo, Alhaj Dk. Shein alitoa
wito kwa wananchi wanaomiliki mikahawa na nyumba za starehe wajitahidi kuzingatia
sheria,taratibu na utamaduni uliopo ili kuzuia kero na maudhi kwa wananchi
wenzao wenye kutekeleza ibada ya funga.
Pia Alhaj Dk. Shen, aliwataka
madereva na watumiaji wa barabara kuzingatia sheria za usalama barabarani hasa
wakati wa jioni ambapo watu wengi huwa wanakimbilia kufutari, huku akiahidi
kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kuimarisha ulinzi wa watu na mali zao kwa
kushirikiana na vijana wa ulinzi shirikishi ili wananchi wapate utulivu na
kutekeleza saumu kwa amani.
Kama kawaida yake Alhaj
Dk. Shein aliwakumbusha viongozi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati pamoja
na uongozi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) wachukue hatua ya kuwapelekea
maji wananchi kwa magari kwenye maeneo yao wanayoishi ambayo huduma hizo
zimepungua.
Pamoja na hayo, Alhaj
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kueleza jinsi uchumi wa Zanzibar ulivyoimarika
sambamba na utoaji wa huduma na ustawi wa wananchi huku akiwapongeza wakulima
wa karafuu kwa mafanikio makubwa yaliopatikana ambapo msimu uliopita jumla ya
tani za karafuu 8,539.39 zenye thamani ya TZS bilioni 119.14 zimenunuliwa na Shirika
la Biashara la Taifa la Zanzibar (ZSTC) hadi Mei 15 mwaka huu.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment