Habari za Punde

Serikali kuhakikisha wote waliojiandikisha kwenda Hijja mwaka huu , nia yao itatimia

 Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Tanzania na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dr. Augustine Mahige akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofika nyumbani kwake Bara bara ya Haile Selassie Jijini Dar es salaam kubadilishana mawazo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Tanzania na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dr. Augustine Maige akiwa kwenye Makaazi yake Bara bara ya Haile Selassie Jijini Dar es salaam.
Picha na  - OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR
Waziri ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dr. Augustine Mahige amesema Wizara hiyo itasimamia ipasavyo na kuhakikisha kwamba nia ya Mahujaji wa Tanzania waliojiandikisha kwenda kutekeleza Ibara ya Hijja Nchini Saudi Arabia Mwaka huu inatimia.
Alisema Wizara yake inafuatilia hatua za mwisho katika kuona tatizo lililojitokeza kwa Baadhi ya Taasisi za Usafirishaji Mahujaji Upande wa Tanzania Bara kukabiliwa na madeni Nchini Saudi Arabia linapata ufumbuzi wa haraka kabla ya kumalizika kwa muda wa mwisho wa uthibitisho wa Mahujaji wa Mwaka huu.
Dr. Augustine Mahige alisema hayo wakati alipofika katika Makazi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Bara bara ya Haile Selassie Jijini Dar es salaam kubadilishana mawazo kuhusu masuala ya Hijja yaliyoleta usumbufu kwa Mahujaji wa Tanzania.
Alisema atalazimika kuzungumza na Mufti  Mkuu wa Tanzania pamoja na Uongozi wa Baraza Kuu la Waislamu {BAKWATA} ili kujua hatua walizofikia katika kuona Taasisi zinazosimamia Usafirisdhaji Mahujaji upande wa Bara wamemaliza matatizo yanayowakabili.
Balozi Mahige alimthibitishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Uongozi wa Wizara yake utalazimika kutoa baraka kwa Mahujaji wanaosimamiwa na Taasisi za Zanzibar pekee iwapo zile za Tanzania bara mpaka hatua ya mwisho zitashindwa kumaliza changamoto zao.
Hatua ya Balozi Mahige imekuja kufuatia baadhi ya Taasisi za Usafirishaji Mahujaji za Tanzania Bara kushindwa kulipa Madeni na kupelekea Wizara inayosimamia masuala ya Mijja Nchini Saudi Arabia kutishia kuzuia Mahujaji wa Tanzania kuingia Nchini humo kwa Ibada ya Hijja Mwaka huu.
Akigusia Miradi ya Kiuchumi inayolenga kustawisha Maendeleo ya Tanzania Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Afrika Mashariki Balozi Mahige alisema ipo haja ya kufuatilia Miradi iliyopata Mikopo na Ufadhili wa Kimataifa ili kujua maendeleo yake.
Balozi Mahige aliitaja baadhi ya Miradi hiyo ni ni pamoja na ile ya  Ujenzi wa Gati ya Mpiga Duri Kisiwani Unguja na ile ya Gati ya Wete Kisiwani  Pemba ambayo imo ndani ya Mpango Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Alisema wakati umefika kwa kila muhusika wa Miradi hiyo akiainisha Wafadhili, Serikali pamoja na Jumuiya yenyewe kubeba jukumu katika kuhakikisha hitilafu na mapungufu yanayojitokeza yanachukuliwa hatua kwa wakati kwa lengo la kuondoa urasimu wa muda mrefu.
Naye kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alimpongeza Balozi Maige kwa hatua alizoamua kuzichukuwa katika kukabiliana na changamoto zilizojitokeza kwenye masuala ya Hijja.
Balozi Seif alisema Ibada ya Hijja ni miongoni mwa nguzo Tano wanazowajibika Waumini wa Dini ya Kiislamu wenye uwezo kuzitekeleza ambayo imo ndani ya Imani za Waumini jambo ambalo wasimamizi wa masuala hayo wanalazimika kuwa makini katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Akielezea furaha yake kutokana na uamuzi wa Tanzania kuweka nia ya kutaka kufungua Ubalozi wake Nchini Jamuhuri ya Cuba Balozi Seif  alisema hatua hiyo muhimu itaongeza chachu ya uhusiano wa Kihistoria uliopo kati ya Tanzania na Cuba.
Balozi Seif alisema Cuba Taifa la kwanza lililoyatambua na kuyaunga mkono Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964 imekuwa mshirika mkubwa kwa Tanzania hasa katika kusaidia Taaluma kwenye miradi iliyomo ndani ya Sekta za Kilimo, Afya na hata masuala ya Viwanda.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.