Habari za Punde

Waziri Mkuu azindua tamasha la Mwaka kogwa Makunduchi


Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Mhe Kassim Majaliwa amesema ipo haja ya viongozi mbali mbali wa Serikali na vyama vya siasa kuhuburi umuhimu wa umoja na mshikamano sambamba na kuzikumbusha jamii zao kuenzi mila na tamaduni walizorithi kutoka kwa wazazi wao.


Waziri Majaliwa aliyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Makunduchi Mkoa wa kusini Unguja kufuatia maadhimisho ya sherehe maalumu za mwaka kogwa ambazo hufanyika kila mwaka.


Amesema tabia ya kuhifadhi mila ma desturi huwafanya wananchi kuendelea kuishi katika mazingira bora ya ujirani mwema.


Alieleza kuwa licha ya kuwa Tanzania ina makabila yasiopungua 120 lakini ni jambo la faraja sana hadi leo hii wananchi wa Makunduchi wanaendelea kudumisha mila walizorithi kwa wazazi wao tangu karne ya 18.


Pamoja na hayo aliwataka wazazi wa eneo hilo kuhakikisha utamaduni huo unaenziwa na kuendelezwa vizazi hadi vizazi.


"Cha kufurahisha zaidi ni kwamba nimeona sherehe hizi pia zinakuza utalii leo kuna wageni wamekuja kutoka Ujerumani na mataifa mengine ya Ulaya hivyo muna kila sababu ya kuendeleza na kulikuza" aliongeza Majaliwa.


Kwa upande wake mwakilishi wa jimbo la Makunduchi, Mhe Haroun Ali Suleiman alimtaka Waziri mkuu kutumia sherehe hio kama sehemu ya kuendeleza umoja baina ya watu wa Makunduchi na Tanzania bara.


Alieleza kuwa anaamini sherehe hizo zitaibua fursa mpya ya mashirkiano baina ya pande mbili za Jamuhuri ya Muungano licha ya kuwa wananchi hao wamekua na udugu wa miaka mingi.


Nae Naibu waziri wa Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar Lulu Msham Abdalla alisema sherehe hio pia ni fursa ambayo Zanzibar inaweza kuitumia kutangaza utalii wake.


Aidha alieleza kuwa kupitia tamasha hilo linaongeza kipato kwa wajasiriamali wa eneo hilo.




Aidha alisema Wizara yake imejipanga kuhakikisha matamasha mbali mbali yanaboreshwa kwa lengo la kuikuza na kuitunza Zanzibar ndani na nje ha Nchi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.