Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Mwani Hendrico Soewardjono alipowasili katika kiwanda cha kampuni hiyo leo na Ujumbe wake akimalizia ziara yake ya mualiko wa Makamo wa Rais wa Indonesia Dkt.Mohamed Jusuf Kalla,[Picha na Ikulu.]
INDONESIA imeahidi kushirikiana na Zanzibar katika kuliimarisha zao la mwani ambalo limekuwa ni miongoni mwa zao la biashara katika visiwa vya Zanzibar.
Uongozi wa Kampuni ya
mwani ya ‘AGAR Swallow’ ya nchini Indonesia umeeleza hayo ulipofanya mazunguzo
na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein katika
ofisi za Kampuni hiyo zilizopo mjini Jakarta wakati alipokitembelea kiwanda
hicho.
Akitoa maelezo katika
mazungumzo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo Hendrico Soewardjono alimueleza Rais Dk.
Shein azma ya Kampuni hiyo ya kushirikiana na Zanzibar katika kuliendeleza
zao la mwani.
Alieleza kuwa Kampuni hiyo
tayari imepata mafanikio makubwa ambapo aina ya bidhaa yake ya unga wa mwani
ambayo hutengenezewa bidhaa mbali mbali za vyakula na dawa imekuwa na soko
kubwa na bidhaa zake huzisafirisha nchi mbali mbali duniani.
Aliongeza kuwa kutokana
na Zanzibar kuliendeleza zao hilo la mwani na kulimwa kwa wingi Kampuni yake
iko tayari kutoa ushirikiano unaohitajika ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo juu
ya uendelezaji wa zao hilo pamoja na
utafutaji wa masoko.
Mkurugenzi Mkuu huyo
alimueleza Dk. Shein kuwa aina ya unga anaotokana na mwani wa aina ya
grasilarias unaotengenezwa kiwandani hapo umekuwa ukitumika sana kwa kutengenezea
bidhaa mbalimbali ambazo zimekuwa maarufu duniani.
Alieleza jinsi
wanavyolisarifu zao la mwani huku akieleza kuwa miongoni mwa bidhaa
zinazotengenezewa unga huo ni pamoja na kutengenezea baadhi ya vyakula, vipodozi,
dawa zikiwemo dawa za mswaki pamoja na kutengeneze bidhaa nyengine mbali mbali.
Aidha, kiongozi huyo wa
Kampuni ya AGAR alieleza namna Serikali ya Indonesia kupitia Kampuni hiyo
inavyoliendeleza na kulisimamia zao la mwani pamoja na kushirikiana na kampuni
ndogo ndogo zinazofanya biashara ya zao hilo.
Nae Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliipongeza azma ya
Kampuni hiyo ya kushirikiana na Zanzibar katika kuliimarisha na kuliendeleza
zao la mwani.
Rais Dk. Shein alieleza
kuwa hatua hiyo itaendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano uliopo ambao ni
wa kihistoria kati ya Indonesia na Zanzibar.
Alieleza kuwa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kushirikiana na Indonesia katika
kuhakikisha zao hilo linaimarika kwani Zanzibar ni miongoni mwa wazalishaji
wakubwa wa zao hilo duniani.
Dk. Shein pia, aliueleza
uongozi huo kuwa ziara yake ya kukitembelea kiwanda hicho ni azma moja wapo ya
kujifunza sambamba na kuangalia utaalamu uanaofanyika kutoka kwa kampuni hiyo
kwa lengo la kupanua wigo.
Nao viongozi aliofuatana
nao Rais Dk. Shein katika ujumbe wake wakichangia katika mazungumzo hayo
walieleza kuwa ni biashara ya zao la mwani kwa upande wa Zanzibar inahitaji
mashirikiano ya kutosha kwani tayari wananchi wameshajenga matumaini makubwa
kwa zao lao hilo.
Walieleza kuwa miongozi
mwa changamoto kubwa iliyopo katika uimarishaji na uendelezaji wa zao hilo ni
pamoja kutokuwepo kwa soko la uhakika la mwani visiwani Zanzibar.
Pia, viongozi hao
waliongeza kuwa kutokana na Kampuni hiyo kupata mafanikio makubwa itakuwa ni
jambo la busara katika kushirikiana kuliimarisha zao hilo pamoja na kuonesha
uzoefu na mafanikio waliyoyapata kwa wakulima wa mwani wa Zanzibar
Wakati huo huo, baadhi ya
viongozi na watendaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar walitembelea na
kufanya mazungumzo yenye lengo la kujifunza katika kiwanda maarufu nchini
Indonesia na duniani kwa ujumla cha INDESSO kilichopo nje kidogo ya mji wa
Bali.
Katika maelezo yao
viongozi wao wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar walieleza kufurahishwa kwao
na mapokezi mazuri yaliyoyanywa na Kampuni hiyo sambamba na azma ya ushirikiano
walio ahidi kuutoa kwa Zanzibar.
Katika maelezo yake,
Mkurugenzi Uzalishaji wa Kampuni hiyo Dk. Efendi Aroma alieleza kuwa Kampuni ya
mafuta ambayo imeanzishwa 1968 imeweza kuimarika sana kutokana na mikakati
maalum iliyojiwekea katika uzalishaji ambayo kampuni kubwa inayozalisha mafuta
ya mimea yakiwemo ya karafuu.
Kampuni hiyo hutoa
mafuta ya mimea mbali mbali ambayo hutumika kwa manukato katika utenegezaji wa
bidhaa za manukato, mafuta ya mimea na
aina mbali mbali za unga unaotumika katika utengenezaji na upishi wa vyakula.
Kampuni hiyo imepata
mafanukio makubwa kutokana na soko la uhakika kutoka kwa nchi za Marekani,
Ulaya na Asia kutokana na bidhaa za mafuta wanazozizalisha yakiwemo mafuta ya
karafuu kuwa na soko kubwa.
Sambamba na hayo,
viongozi wa Kampuni hiyo ya INDESSO walieleza kufarajika kwao kwa kutembelewa
pamoja na kukaa pamoja na kubadilishana mawazo kati yao na viongozi na
watendaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar jambo ambalo walieleza kuwa
limewapa faraja na matumaini makubwa ya mashirikiano.
Pamoja na hayo, viongozi
hao wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar walitumia fursa hiyo kwa kutembelea sehemu mbali mbali za
kiwanda hicho ambacho kina mitambo ya kisasa.
Dk.
Shein anatarajiwa kurejea nchini hapo kesho Jumatatu ya tarehe 6 Agosti, 2018
baada ya kumaliza ziara yake nchini Indonesia
ambapo katika ziara hiyo alifuatana na viongozi mbali mbali akiwemo Mke
wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein pamoja na Mawaziri na watendaji
wengine wa Serikali.
Ziara hiyo ya Dk. Shein aliifanya
kufuatia mwaliko wa Makamo wa Rais wa Indonesia Muhammad Jusuf Kalla ambapo
mbali ya kutembelea na kufanya mazungumzo na viongozi mbali mbali wa Indonesia katika
mji wa Jakarta pia, alitembeleaa kisiwa cha utalii cha Bali na kufanya
mazungumzo na viongozi wa kisiwa hicho pamoja na kutembelea maeneo mbali mbali
ya maendeleo ya kitalii, kihistoria, utamaduni na sanaa.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment