Habari za Punde

Waziri Haroun Afanya Ziara Kutembelea Ofisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba Sheria Utumishi wa Umma na Utawala Bora Zanzibar Mhe. Haroun Ali Suleiman akizungumza na Watendaji wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar wakati ziara yake kutembelea Ofisi hiyo iko chini ya Wizara yake.

Na Raya Hamad (ORKSUUUB)

Waziri wanchi Ofisi ya Rais Katiba Sheria Utumishi wa Umma na Utawala bora  Mhe Haroun Ali Suleiman amewataka watendaji na wafanyakazi katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kuziangalia sheria zilizopitwa na wakati na zile zinazotakiwa kufanyiwa marekebisho ili kuenda sambamba na  mabadiliko ya kiutendaji  .

Waziri Haroun ameyasema hayo wakati alipokutana na watendaji wakuu  na wafanyakazi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu  iliyopo Mazizini   wilaya ya Magharibi B , ambapo amesema kuwa zipo baadhi ya sheria ambazo zimepitwa na wakati hivyo Ofisi ya Mwanasheria mkuu ina wajibu wa kuzimamia sheria na kuishauri Serikali kwa uadilifu

Aidha Maalim Haroun amewataka  wanasheria kutoridhika na elimu walionayo na badala yake kuendelea kutafuta elimu  “huwezi kuwa mwanasheria bila ya kujishughulisha kusoma sana na kuitumikia vyema na kwa uadilifu nafasi uliyopo”

Waziri Haroun amewasisitiza wanasheria kuwafikia wanachi maeneo yao hasa  vijijini  wananchi wanakosa haki zao kwa sababu ya kutoelewa sheria hivyo Ofisi hii ina wajibu wa kuwaelimisha wananchi  ili kuondosha mlolongo wa makosa yanayotokana na kutoelewa sheria.

Katika hatua nyengine waziri Haroun ameagiza uongozi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu  kuwaunganisha na kuwakutanisha wanasheria wote na viongozi wakuu wa taasisi  kwa kuwapa mafunzo maalum ikiwemo kufahamu majukumu yao na mipaka yao kisheria ili kutokinzana na sheria za nchi na amri ya Mahakama na  kuepuka migongano katika mhimili  wa dola.

Nae Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Mh Said Hassan Said amesema kuwa katika kutekeleza wajibu wa kazi  Afisi inafanya shughuli mbali mbali za Serikali ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri wa kisheria kwa taasisi mbalimbali za Serikali , uandishi wa miswaada ya sheria , pamoja na kanuni za sheria zake, kusimamia kesi na mashauri ya madai kwa niaba ya serikali , kuandaa hati na nyaraka za kisheria , kusimamia mikataba yote ambayo serikali ni sehemu ya mikataba hiyo na kufanya mambo mengine ya kisheria kwa niaba ya serikali .
Jumla ya miswaada ya sheria ishirini na mbili imewasilishwa Baraza la Wawakilishi kujadiliwa na kupitishwa ambapo tayari miswaada hio imeshawekwa saini na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mpinduzi  Dr Ali  Mohamed Sheni na zinaendelea kutumika ambapo Ofisi imeandaa kanuni 32 zinazotokana na sheria tofauti kwa lengo la kuzifanyia sheria hizo ziweze kutekelezeka kwa ufanisi zaidi.

Akitoa taarifa kuhusiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu Naibu Mwanasheria Mkuu Mhe.Mzee Ali Haji amesema  Ofisi  imedhamiria kutekeleza mfumo wa mageuzi ya utowaji huduma za sheria pamoja na kujiwekea mikakati ya utekelezaji wa mfumo wa mageuzi ya utowaji wa huduma za sheria ikiwemo kufuatilia indhari za kuishitaki serikali, kuiwakilisha serikali na taasisi zake mahakamani, kuwajengea uwezo watumishi kwenye uandishi wa sheria na usimamizi wa kesi na mikataba ndani na nje ya nchi.

Kushiriki katika mapatano na  utekelezaji na usimamizi wa mikataba ,kutoa msaada wa kisheria kwa jamii juu ya masuala ya miswaada mikataba na kesi za madai , kufanya utafiti katika Nyanja mbalimbali kuhusiana na kesi za madai ,uandishi wa sheria na masuala ya mikataba,   kuthibitisha muongozo wa mikataba na kutayarisha , kuhifadhi na kusimamia masuala yahusio uandishi wa miswaada , kanuni na matangazo ya kisheria  

Nao wafanyakazi katika Ofisi hio wamemuomba Waziri  Haroun kuwaangalia kwa jichola huruma watendaji ambao wanakaribia kustaafu wakiwemo makatibu muhtasi

“Mhe.tunaomba kuthaminiwa kutokana na usowefu tulionao hasa katika suala la kupandishwa kwa daraja la kazi ukweli sisi masekretari ndio tunaodhibiti siri za viongozi lakini inasikitisha kuona tunastaafu tukiwa masikini tunatamani kuongeza elimu lakini chuo hatuna hapa Zanzibar kulingana na viwango vinavyotakiwa vya ufaulu wa sasa”alisema Khadija Ali 

Ndugu Ali Ali Hassan ambae ni mkuu wa kitengo cha Madai amesema kukosekana kwa mashirikiano kwa baadhi ya taasisi za Serikali kunapelekea kuonekana kupuuzwa kwa amri za mahakama wakati kesi inapokuwa tayari ipo mahakamani  nae, Bi.Fatma Saleh mkuu wa kitengo cha mikataba ameomba ushirikishwaji zaidi ndani ya Taasisi kuzipitia document na kujiridhisha kabla ya kuziwasilisha kwa Mwanasheria Mkuu



Ziara hiyo  ya Mhe. Waziri Haroun ni mfululizo wa kuzitembelea taasisi zilizomo ndani ya Ofisi ya Rais Katiba Sheria Utumishi wa Umma na utawala bora .  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.