Habari za Punde

DKT TIZEBA AWASILISHA TAARIFA YA ZAO LA KAHAWA KWA KATIBU MKUU CCM, USHIRIKA WAUNGWA MKONO KWA KAULI MOJA

Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba, Waziri wa kilimo akitoa ufafanuzi kuhusu zao la kahawa wakati akiwasilisha taarifa ya mwenendo wa soko la kahawa nchini kwa Dkt Bashiru Ali Kakurwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi mkutano uliohudhuriwa na wabunge kutoka maeneo yote yanayozalisha kahawa, Jana Tarehe 14 Septemba 2018 katika ukumbi wa Chama Cha Mapinduzi maarufu White House Mjini Dodoma. (Picha Zote Na Mathias Canal, WK)
Washiriki wa mkutano wa uwasilishaji wa mwenendo wa zao la kahawa wakifatilia kwa makini taarifa iliyowasilishwa na Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba, Waziri wa kilimo mbele ya Dkt Bashiru Ali Kakurwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi mkutano uliohudhuriwa na wabunge kutoka maeneo yote yanayozalisha kahawa, Jana Tarehe 14 Septemba 2018 katika ukumbi wa Chama Cha Mapinduzi maarufu White House Mjini Dodoma. 
Dkt Bashiru Ali Kakurwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi akizungumza mara baada ya Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba, Waziri wa kilimo kutoa ufafanuzi kuhusu zao la kahawa wakati akiwasilisha taarifa ya mwenendo wa soko la kahawa nchini, Jana Tarehe 14 Septemba 2018 katika ukumbi wa Chama Cha Mapinduzi maarufu White House Mjini Dodoma. 
Dkt Bashiru Ali Kakurwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (Wa pili kushoto) akiendesha kikao mara baada ya uwasilishwaji taarifa ya mwenendo wa soko la kahawa nchini, Jana Tarehe 14 Septemba 2018 katika ukumbi wa Chama Cha Mapinduzi maarufu White House Mjini Dodoma. Wengine ni Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba, Waziri wa kilimo (Kushoto), Naibu waziri wa kilimo Mhe Omary Mgumba (wa kwanza kulia) na Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Kanali Mstaafu Ngemela Lubinga (wa tatu kulia)
Wataalamu kutoka wizara ya kilimo wakifatilia mkutano wa uwasilishaji wa mwenendo wa zao la kahawa taarifa iliyowasilishwa na Mhe Mhandisi Dkt Charles Tizeba, Waziri wa kilimo mbele ya Dkt Bashiru Ali Kakurwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi mkutano uliohudhuriwa na wabunge kutoka maeneo yote yanayozalisha kahawa, Jana Tarehe 14 Septemba 2018 katika ukumbi wa Chama Cha Mapinduzi maarufu White House Mjini Dodoma.

Na Mathias Canal-WK, Dodoma
Katika vipindi mbalimbali vya historia ya Tanzania masoko ya Kahawa yamekuwa yakiendeshwa kwa mfumo wa ushirika na soko huria, Mfumo wa soko huria uliruhusu makampuni na watu binafsi kununua mazao moja kwa moja kutoka kwa wakulima pasipo udhibiti hali iliyopelekea kuwepo kwa changamoto mbalimbali zikiwemo bei isiyokuwa na tija kwa mkulima, ubora hafifu wa mazao, ukwepaji wa kodi kwa wanunuzi na ukosefu wa takwimu sahihi za uzalishaji na mauzo.

Kutokana na changamoto za mfumo wa soko huria, Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli iliamua kurejesha ununuzi wa mazao matano ya kimkakati (Korosho, Tumbaku, Pamba, Kahawa, na Chai) kupitia vyama vya ushirika tangu mwaka 2016 ili kunufaisha wakulima, wanunuzi/wafanyabiashara na serikali.

Hayo yamebainishwa jana tarehe 14 Septemba 2018 na Mhandisi Mhe Dkt Charles Tizeba, Waziri wa kilimo wakati akiwasilisha taarifa ya mwenendo wa soko la kahawa nchini kwa Dkt Bashiru Ali Kakurwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi katika ukumbi wa mikutano wa CCM Makao makuu maarufu kama White House, Mkutano uliohudhuriwa na wabunge kutoka maeneo yote yanayozalisha kahawa, Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Kanali Mstaafu Ngemela Lubinga, Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa (NEC) Makongoro Nyerere, Naibu waziri wa Kilimo, Mhe Omary Mgumba, wataalamu kutoka wizara ya kilimo akiwemo Naibu katibu mkuu Prof Sizya Tumbo, Mrajis wa vyama vya ushirika,vyama vya ushirika na wawakilishi wa wakulima kutoka maeneo yanayolima kahawa.

Katika taarifa hiyo Dkt Tizeba alieleza kuwa kamwe hawezi kuruhusu mtu mmoja mmoja au kundi la watu kuvunja ushirika ambao hivi karibuni umeanza kuimarika mahususi kwa ajili ya kumkomboa mkulima uamuzi ambao umebainishwa kwenye ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020 katika sura ya pili ibara ya 22 ikisisitiza kuviimarisha na kuviwezesha vyama vya ushirika kuwa na uwezo wa kutafuta masoko ya mazao ya wakulima ya ndani na nje kwa kuweka mfumo madhubuti wa ukusanyaji, uchambuzi na uenezaji wa taarifa za masoko na kutoa elimu juu ya uongezaji wa thamani na biashara.

Alieleza kuwa zipo faida nyingi kwa mkulima anapouza kupitia ushirika na hasa vyama vya msingi ambazo ni pamoja na wakulima kuwa na nguvu ya pamoja ya kushauriana ili kupata bei nzuri na kunufaika na kilimo, wakulima kupata nguvu ya kuanzisha na kuendesha maghala na viwanda vya kuongeza thamani ya mazao yao, kuwawezesha wakulima kutunza ubora wa mazao kwa mujibu wa sheria, kanuni na miongozo ya mazao husika.

Faida zingine ni kuwawezesha wakulima kupunguza gharama za uzalishaji kwa kuagiza pembejeo kwa pamoja, kuwezesha upatikanaji mazao ya uhakika na yenye ubora kwa wanunuzi, kuwezesha serikali za mitaa na serikali kuu kupata mapato yake stahiki kulingana na uzalishaji halisi, kuwezesha upatikanaji wa takwimu sahihi za idara ya wakulima na uzalishaji; na kuwawezesha wanunuzi kufanya malipo ya mazao kwa kuzingatia makubaliano yaliyofikiwa katika minada.

Aidha, Dkt Tizeba alisema kuwa mwenendo wa mauzo ya kahawa kwa msimu wa mwaka 2016/2019 ni mzuri ukilinganisha na misimu miwili iliyopita ya mwaka 2016 na 2017. Mauzo ya kahawa kwa mwezi Agosti 2018 ni mara mbili ya mauzo ya msimu wa mwaka 2017 ni mara nne ya msimu wa mwaka 2016. “Mauzo ya kahawa mwezi Septemba 2018 kwa mnada mmoja uliofanyika ni zaidi ya mauzo yote ya mwezi Septemba 2017 na ni sawa na mauzo yote ya kahawa kwa mwezi Septemba msimu wa mwaka 2016” Alisisitiza Dkt Tizeba

Kwa upande wake Dkt Bashiru Ali Kakurwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi akizungumza mara baada ya mjadala huo kutuama kwa masaa 8 kujadili namna ya kupata masoko ya mazao ya kilimo, urahisi wa upatikanaji wa mitaji, siasa ya kilimo kupitia ushirika na maandalizi ya miundombinu rafiki katika kilimo, alisema kuwa nchi ya Tanzania ipo katika mageuzi makubwa ya kimfumo na kimuundo hivyo mgogoro wa kiuchumi ni lazima ujitokeze kutokana na watu kulazimisha mazoea na haramu kuwa halali.

Alisema kuwa viongozi wote wa chama na serikali wanapaswa kuunga mkono jitihada za serikali kumkomboa mkulima kupitia ushirika, kujenga uchumi kupitia mshikamano lakini ushirika unaotakiwa ni ule wa Demokrasia wenye mizizi imara ili kuimarisha usalama wa nchi katika kilimo ambao unategemea wakulima wadogo.

Dkt Bashiru aliongeza kuwa ni lazima CCM kiwe chama kinachoingoza na kuisimamia serikali kwa kujenga utamaduni wa kujadiliana mambo muhimu ya kitaifa ili kukifanya chama hicho kuongeza imani maradufu kwa wananchi waliokiamini chama hicho na kukipa dhamana ya kuongoza Dola kupitia ilani ya ushindi ya mwaka 2015-2020.

Katika hatua nyingine ameitaka Wizara ya kilimo na Wizara zingine zote sambamba na taasisi za umma kutoa taarifa za mara kwa mara kwenye vyombo vya habari kuhusu yale yanayofanywa na serikali, kueleza mikakati ya serikali katika kuimarisha uchumi, sambamba na kutaja mafanikio yanayofanywa na serikali ili kuongeza uelewa kwa wananchi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakipotoshwa.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.