Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Azungumza na Uongozi wa Kampuni ya MOBH Nchini Dubai.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi akimsikiliza Mkurugenzi wa Bodi pia Meneja Mkuu wa Kampuni Bwana Omar Mohammad Bin Haider wakati wa hafla ya utiaji saini Mkataba wa Makubalizno ya kuunga mkono jitihada za Serikali yaMapinduzi ya Zanzibar katika masuala ya kuimarisha Uwekezaji.(Picha na OMPR)

Na.Othman Khamis OMPR.
Safari ya Zanzibar kuelekea katika mtazamo wa matarajio ya kuwa Dubai ya Afrika Mashariki inaanza kuchipua kidogo kidogo kufuatia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutiliana saini Mkataba na Kampuni ya Kimataifa ya Mohammed Omar Bin Haider Holding Group { MOBH } ya Nchini
Dubai.

Saini ya Mkataba huo imelenga kuunga mkono jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika masuala ya kuimarisha Uwekezaji na Maendeleo ya Zanzibar Kiuchumi.
Waziri wa Fedha na Mipango Dr. Khalid Salum Mohamed alitia Saini Mkataba huo kwa Niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakati Kampuni ya Mohammed Omar Bin Haider Holding Group ikatiwa Saini na Mkurugenzi wa Bodi akiwa pia Meneja Mkuu wa  Kampuni hiyo Bwana Omar
Mohammad Bin Haider hafla iliyofanyika katika Hoteli ya Kimataifa ya Grand Exelsior Mjini Al Barsha Nchini Dubai.

Hafla hiyo fupi ilishuhudiwa pia na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyetokea Nchini China kuhudhuria Maonyesho ya 15 ya Kimataifa ya China- Asean Expo 2018 yaliyofanyika katika Mji wa Nanning katika Jimbo la Guangxi.

Akizungumza baada ya utiaji saini Mkataba huo Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Dr. Khalid Salum Mohamed alisema Zanzibar imeahidi na kuwa tayari kuiona Kampuni hiyo yenye Makao Makuu yake Nchini Dubai inazitumia furza za Uwekezaji zilizopo Visiwani Zanzibar.

Dr. Khalid alisema Zanzibar iliyokuwa kitovu cha harakati za
Kibiashara kilichokuwa kikiunganisha Bara la Asia na Ukanda wa Kusini na Mashariki mwa Bara la Afrika lenye Wakaazi zaidi ya Milioni 360,000,000 hivi sasa imepania kuirejeshea hadhi yake kwa kutanua maeneo mengine ya Uwekezaji.

Alisema Miundombinu iliyoimarishwa katika Sekta za Mawasiliano ya Anga, Uvuvi wa Bahari Kuu, Utalii na Biashara ikiambatana na Sera inayotekelezeka imezingatia kuwajengea Mazingira bora Wawekezaji wa ndani na Nje kuwekeza Miradi yao katika mfumo watakaopenda ukiwemo ule wa Ubia.

“ Tunakaribisha Wawekezaji wa kigeni zaidi katika kusaidia kuimarisha Uchumi wa Zanzibar hasa katika Sekta ya Utalii inayounganishwa hivi sasa na safari za moja kwa moja za Anga kutoka maeneo mbali mbali ya Dunia”. Alisema  Dr. Khalid Salum.

Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar aliueleza Uongozi huo wa Kampuni ya MOHB Holding Group kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika juhudi za kuimarisha Uchumi wake imeanzisha maeneo mengine ya uwekezaji ili kutanua wigo wa Uchumi wake.

Aliyataja baadhi ya maeneo hayo kuwa ni pamoja na  Mradi Mpya wa Utafiti wa Mafuta na Gesi Asilia unaoendelea pamoja na matayarisho ya Ujenzi wa Bandari ya Mizigo ya Mpiga Duri maeneo ambayo Kapuni hiyo inaweza kufikiria namna ya kusaidia kwake.

Alisema Dira ya Maendeleo ya 2025 na Mpango wa Maendeleo 2020 imelenga kuinyanyua Zanzibar Kiuchumi ili Wananchi wake wafikie hatua ya Ustawi uliotukuka mipango inayohusishwa pia na Taasisi, Mataifa na Mashirika ya Maendeleo ya ndani na nje ya Nchi.

Dr. Khalid alifahamisha kwamba Kampuni ya Mohammed Omar Bin Haider Holding Group kutokana na uzoefu wake wa muda mrefu iliyonayo na mtandao mzuri wa Uwekezaji bado wana fursa ya kuangalia maeneo zaidi wanayoweza kufikiria kuwekeza Zanzibar.

Uongozi wa Kampuni hiyo umeridhika na ukarimu mkubwa walionao Watu wa Visiwa vya Zanzibar wakati wa ziara ya Ujumbe huo uliyoifanya Zanzibar mwishoni mwa Mwezi Agosti 2018 ambao umeshawishika kutaka kuwekeza Miradi yao ya Kiuchumi Visiwani Zanzibar.

Katika kuunga mkono jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwenye uimarishaji wa Uchumi wake Taasisi hiyo ya Uwekezaji imeonyesha nia ya kuwasilisha maombi yake ya kutaka kuwekeza miradi katika sekta mbali mbali kama Mawasiliano, uvuvi wa Bahari Kuu, Kilimo pamoja na
Viwanda.

Kampuni ya MOHB Holding Group yenye Makampuni  tofauti zaidi ya Sita katika Mataifa mbali mbali ya Mashariki ya Kati  inajishughulisha
zaidi na Miradi  mbali mbali ya Ujenzi wa Miji ya Kisasa, Huduma za Afya, Elimu, Miundombinu, Biashara pamoja na Sekta ya Utalii.


Muungano wa Nchi za Falme za Kiarabu {UAE} imewekeza Nchini Tanzania Miradi mbali mbali ya Kiuchumi inayokadiriwa kuwa na gharama ya Dola za Kimarekani Milioni 991 kuanzia Mwaka 2003 hadi 2016.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.