Habari za Punde

Tanzania Inaongoza Kwa Uwekezaji Ukanda wa Afrika Mashariki - Mhe Kassim Majaliwa.




Na.Khadija Mussa. OWM.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania inaongoza kwa kupokea uwekezaji wa kigeni  wa moja kwa moja katika Ukanda wa Afrika ya Mashariki. 

“Mtiririko wa uwekezaji wa kigeni wa moja kwa moja nchini umeongezeka kwa zaidi ya miaka 10 iliyopita na sasa wawekezaji wameipa kipaumbele Tanzania kama kitovu cha uwekezaji barani Afrika.”

Ameyasema hayo leo (Jumapili, Septemba 02 ,2018) wakati akihutubiaKongamano la Biashara kati ya Tabnzania na China kwenye Hoteli ya  Winstin jijini Beijing nchini China.

Waziri Mkuu amesema Tanzania imethibitika kuwa ni Taifa lililodhamiria  kwa dhati  kujenga uchumi wa viwanda , pamoja na kulinda na kudumisha amani na utulivu.

Amesema ripoti ya uwekezaji duniani iliyotolewa mwaka 2018, inaonesha kuwa Tanzania  inaongoza kwa kupokea  uwekezaji  katika ukanda wa Afrika ya Mashariki na imepokea kiasi cha Dola za Marekani bilioni 1.2 mwaka 2017.

Waziri Mkuu amesema Tanzania inafanya juhudi kubwa  ili iweze kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo  mwaka 2025, hivyo imeweka mkazo  mkubwa katika  kujenga msingi imara wa viwanda.

“Ili kufanikisha hilo tumeandaa Ukanda wa Kuzalisha kwa ajili ya mauzo ya Nje na Ukanda maalum wa Kiuchumi tukilenga kutimiza  mkakakati wetu wa kukuza  uchumi wa viwanda na biashara.”

Akizungumzia kuhusu sekta ya fedha, Waziri Mkuu amesema Tanzania inawakaribisha wawekezaji  kuanzisha Taasisi za Kifedha kama vile benki kwa ajili ya kutoa mikopo midogo midogo, benki za uwekezaji, benki za kilimo na benki za biashara.

Kuhusu uwekezaji kutoka China uliosajiliwa na Kituio cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kati ya Novemba 2015 hadi Oktoba 2017,  Waziri Mkuu amesema  umefikia thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.077 na umejikita katika meneo ya kilimo, majengo ya biashara, rasilimali watu, viwanda na utalii.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesemakuna fursa nyingi kwenye sekta ya huduma hususan katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambayo ni miongoni mwa sekta ndogo zinazokuwa kwa haraka nchini Tanzania. 

Pia kumekuwa na ukuaji na mageuzi ya haraka katika soko la TEHAMA nchini kwa miaka 10 iliyopita. “Soko la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano limekuwa kwa ongezeko la watumiaji, aina ya huduma zinazotolewa pamoja na kupanuka kwa eneo ambalo huduma hizo hutolewa.”

Waziri Mkuu ameongeza kuwa, “Tanzania kuna fursa zisizo na ukomo katika eneo hili huku kukiwa na matarajio ya kukuwa kwa soko la kikanda.” 

“Maeneo ya kuwekeza ni pamoja na utoaji wa huduma za simu hususan katika maeneo ya vijijini, utoaji na uendeshaji wa huduma za mtandao pamoja na ukarabati na matengenezo ya vifaa vya mawasiliano. Tunawakaribisha wawekezaji kuwekeza katika maeneo haya.”

Amesema kwa wale ambao nia yao ni kuwekeza katika kilimo, Tanzania ina hekta milioni 44 za ardhi inayofaa kwa kilimo na takribani hekta milioni 29.4 kwa ajili ya umwagiliaji.

 “Ninawakalibisha wawekezaji kuja kuwekeza katika kilimo cha biashara kwa mazao kama miwa, mpunga, ngano, kahawa, chai na mahindi. Tuna fursa kubwa ya kuwekeza katika kilimo cha miwa na uzalishaji wa sukari.”

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, SEPTEMBA 02, 2018.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.