Habari za Punde

Breaking Nyuuuuzzzz.... : Mfanyabiashara Mo Dewji apatikana *Apatikana baada ya waliomteka kumtupa viwanja vya Gymkhana Dar *Waliomteka inadaiwa walikuwa wanaongea lafudhi ya South Afrika *MO mwenyewe awashukuru Watanzania kwa dua zao kwake





Na Said Mwishehe,Globu ya jamii
MFANYABIASHARA maarufu Mohammed Dewji 'MO' aliyekuwa ametekwa akiwa katika Hoteli ya Collessium jijini Dar es Salaam hatimaye amepatikana akiwa mzima na mwenye afya njema.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa amethibitisha kupatikana kwa MO ambapo anasema yeye amemuona na amezungumza naye akiwa mzima na tayari ameungana na familia yake.

Kamanda Mambosasa akifafanua zaidi leo jijini Dar es Salaam amewaambia Watanzania, MO alitupwa viwanja vya Gymkhana usiku wa kuamkia leo wa Oktoba 20 mwaka huu."Baada  ya kutekwa tarehe Oktoba 11,2018 gari ya watekaji iliendeshwa speed takribani dakika 15 na kuwekwa kwenye chumba akiwa amefunikwa  ili asiwatambue watekaji."

Amesema kwa mujibu wa MO ni kwamba watekaji hao walikuwa wakiongea lugha za Afrika Kusini na hivyo inathibitisha waliomteka hawakuwa Watanzania na kinachoendelea Polisi nao wanaendelea kukamilisha taratibu za kiuchunguzi.

Mambosasa amesema kuwa MO kwa siku zote ambazo alikuwa anashikiliwa na watekaji alikuwa kwenye mazingira magumu lakini wanashukuru amepatikana akiwa salama kwani kwa kipindi chote Jeshi la Polisi lilikuwa likihangaika kuhakikisha anapatikana na kweli amepatikana.

Ameongeza kupitia upelelezi wao walipata taarifa MO ametupwa maeneo ya Gymkhana na hivyo baada ya kupata taarifa hizo yeye pamoja na maofisa wake wa upelelezi wamefika nyumbani kwa mfanyabiashara huyo ambaye ameungana na familia yake.

Hata hivyo Mambosasa alimuomba MO kama hatojali kuzungumza ili Watanzania waweze kumuona na kumsikia ambapo alimpa nafasi ya kusalimia.Kwa upande wake MO amesema kuwa anawashukuru Watanzania wote na katika shukrani hizo ameanza kwa kumshukuru Rais Dk.John Magufuli na kisha akatoa shukrani kwa Jeshi la Polisi kutokana na jitihada zao za kuhakikisha anapatikana.

"Ahsante wote na nawashukuru Watanzania wote ,nipo salama," amesema MO Dewji akiwa nyumbani huku Mambosasa akiwataka Watanzania kuendelea kuwa watulivu.Kwa kukumbusha tu Mo alitekwa Oktoba 10 mwaka huu saa 11 asubuhi baada ya kufika kwenye hoteli ya Collessium kwa ajili ya mazoezi ambapo kabla ya kushuka kwenye gari yake watekaji walimteka na kuondoka naye kwenye gari aina ya Toyota Suff na kisha kwenda kusikojulikana.

Hata hivyo Polisi waliamua kuweka mikakati ya kuhakikisha MO anapatikana.Wakati wakiendelea na upelelezi wao jumla ya watu 27 waliwashikilia kwa mahojiano lakini hadi jana walikuwa wamebaki na watu nane.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro wakati anazungumza jana asubuh na waandishi wa habari alisema jeshi hilo halijalala tangu MO alipotekwa kwani wanaendelea kufuatilia na kukusanya taarifa ambazo zitafanikisha kupatikana kwake.

IGP Sirro pia alionesha picha ya gari ambayo ilihusika katika tukio la kutekwa MO pamoja na risasi mbili ambazo zilikuwa eneo la tukio ambazo nazo walizichukua kwa ajili ya uchunguzi ambapo aliwahakikishia Watanzania jeshi lao la Polisi liko imara na linafanyakazi zake kwa weledi.

Mfanyabiashara Mo Dewji amepatikana. Waziri January Makamba amesema kuwa amemuona na kuongea nae kwa kirefu, ni mzima wa afya isipokuwa ana alama za kufungwa kamba mikononi na miguuni. Ameongeza kuwa, majira ya saa nane za usiku, watekaji walimtupa kwenye viwanja vya Gymkhana, Dar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.