Habari za Punde

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe Eng.Hamad Masauni Akabidhiwa Orodha ya Majina ya Wauzaji Dawa za Kulevya Zanzibar.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad (kulia), akiangalia majina ya watu wanaotuhumiwa kujihusisha na uuzaji wa dawa za kulevya wakati wa mkutano wa hadhara na wananchi hao ikiwa ni jitihada za Serikali kudhibiti matukio ya uhalifu  yaliyoanza kushamiri katika maeneo mbalimbali  Visiwani Zanzibar.Wengine kutoka kushoto ni Mkuu wa Polisi Jamii Zanzibar, Emmanuel Lukula, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Saleh Mohamed Saleh na Katibu wa Naibu Waziri, George Mwansasu. 
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad (kulia), akizungumza na wananchi wa eneo la Sogea, Wilaya ya Mjini Unguja (hawapo pichani), wakati wa mkutano wa hadhara na wananchi hao ikiwa ni jitihada za Serikali kudhibiti matukio ya uhalifu  yaliyoanza kushamiri katika maeneo mbalimbali Visiwani Zanzibar.Wengine kutoka kushoto ni Kamishna Msaidizi wa Polisi, Saleh Mohamed Saleh na kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka Zanzibar, Masoud Mabalila
Mwananchi wa eneo la Sogea, Wilaya ya Mjini Unguja, Ally Saleh Ally, akielezea kero ya uhalifu kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad (kulia),wakati wa Mkutano wa Hadhara uliokuwa na lengo la kujadili jinsi ya kukomesha matukio ya uhalifu yanayoanza kushamiri Visiwani Zanzibar
Mwananchi wa eneo la Sogea, Wilaya ya Mjini Unguja, Mariamu Said Ali, akielezea kero ya uhalifu kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad (kulia),wakati wa Mkutano wa Hadhara uliokuwa na lengo la kujadili jinsi ya kukomesha matukio ya uhalifu yanayoanza kushamiri Visiwani Zanzibar

Kamishna Msaidizi wa Polisi, Saleh Mohamed Saleh, akizungumza na wananchi wa eneo la Sogea, Wilaya ya Mjini Unguja (hawapo pichani), wakati wa mkutano wa hadhara na wananchi hao ikiwa ni jitihada za Serikali kudhibiti matukio ya uhalifu yaliyoanza kushamiri katika maeneo mbalimbali  Visiwani Zanzibar.Kulia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Na Mwandishi Wetu
Wananchi wa eneo la Sogea, Wilaya ya Mjini Unguja wamemkabidhi Naibu Waziri  wa  Mambo  ya  Ndani ya Nchi, Mhandisi  Hamad  Masauni, orodha ya watu  wanaoshukiwa  kujihusisha na uuzaji wa dawa za kulevya Visiwani Zanzibar.
Wananchi hao wamekabidhi orodha hiyo baada ya Naibu Waziri Masauni kuwataka waorodheshe majina ya watu wanaowafahamu wakituhumiwa kujihusisha na biashara hiyo ambayo imekuwa ikiaribu nguvu kazi ya Taifa na kusababisha  kuwepo  kwa  matukio ya uhalifu katika sehemu mbalimbali Visiwani humo.
Awali  wakiwasilisha  kero zao kwa nyakati  tofauti wananchi hao waliiomba serikali  kudhibiti  biashara  hiyo  ya dawa za kulevya  kwani  imekua ikishamiri kwa kasi Visiwani humo na wakishangaa ukimya wa mamlaka husika kuacha biashara hiyo ikizidi kuleta madhara katika jamii.
Akizungumza katika Mkutano huo wa hadhara, Naibu Waziri Masauni amewaahidi  wananchi  hao  kuchukua  hatua  madhubuti  kukabiliana  na  wauzaji wa dawa za kulevya huku akitoa maelekezo kwa  Jeshi  la  Polisi  kuwakamata watu  wote waliotuhumiwa  na  uchunguzi  uanze  mara moja.
“Hatuwezi  kama  Taifa  tukawa  na vijana ambao hawana faida katika jamii, vijana  ni  nguvu kazi ya Taifa, tutahakikisha majina yaliyoletwa hapa tunayafanyia  kazi na natoa maelekezo kwa Jeshi la Polisi kuhakikisha watuhumiwa hao wanakamatwa na nitahitaji ripoti hiyo ndani ya wiki mbili, haiwezekani watu wachache waharibu nguvu kazi ya Taifa kwa maslahi yao binafsi na familia zao,” alisema  Masauni
Akizungumza katika mkutano huo , Kamishna Msaidizi, Saleh Mohamed Saleh, aliwaomba wananchi kuzifikisha  taarifa  za  uhalifu  katika  vituo  vya  Jeshi la Polisi au Serikali ya Mtaa  ili  hatua ziwe zinachukuliwa ili kuweza kudhibiti  uhalifu  katika  maeneo yao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.