Habari za Punde

Kampuni ya Simu ya TTCL Yapongezwa Kwa Uzalendo Wake Kuinga Mkono Serikali Katika Masuala ya Kuhifadhi Mazingira.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif akiupongeza Uongozi wa Kampuni ya Simu Tanzania kwa uzalendo wao wa kujitolea kujenga ukuta wa kuzuia athari ya Mmong’onyoko wa Ardhi.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kati kati akiwa na baadhi ya Viongozi wakiangalia ukuta wa Mawe uliojengwa na Kampuni ya Simu Tanzania {TTCL} chini ya Mlima uliopo Mtaa wa Michakaeni Chake Chake Pemba. 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi,akimsikiliza Meneja wa TTCL Tawi la Pemba Ndugu Khamis Ishaq Ngwali akimueleza Balozi Seif  hatua iliyofikiwa na Kampuni hiyo katika ujenzi wa ukuta huo wenye Mita 14.
Muonekano wa Ukuta wa mawe uliotumia na Waya uliojengwa na Kampuni ya Simu Tanzania hapo katika Mtaa wa Michakaeni ambapo upo Mnara wa Kampuni hiyo.(Picha na OMPR)


Na.Othman Khamis.OMPR. 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameushukuru na ameupongeza Uongozi wa Kampuni ya Simu Tanzania {TTCL} kwa Uzalendo wake inaojitolea wakati wote wa kuiunga mkono Serikali katika masuala ya kutunza Mazingira.
Alisema kitendo cha Kampuni hiyo kujitolea kujenga ukuta wa Mawe uliotumia Taaluma ya Kisasa kwa kuzuia athari ya Mmong’onyoko wa Ardhi katika eneo la Michakaeni Chake chake Pemba mbali ya kunusuru Mnara wao wa Mawasiliano lakini pia umesaidia kuepusha athari kwa Nyumba na Skuli iliyopo jirani.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa pongezi hizo baada ya kuukagua Ukuta huo wenye urefu wa Mita 14 ambao uko chini ya Mlima unaoonekana kuathirika mara kwa mara na Mvua za Masika za kila Mwaka hasa zile zilizonyesha Mwaka jana na kuleta athari kubwa.
Alisema ukuta huo kwa kiasi kikubwa umeweza kuleta Faraja kubwa kwa Wakaazi wanaouzunguuka Mlima wa hapo Michakaeni ambapo pia alizikumbusha Taasisi nyengine na Wananchi hapa Nchini waendelee kuchukuwa hadhari kukinga athari zinazoweza kuleta Mmong’onyoko.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliushauri Uongozi huo wa Kampuni ya Simu Tanzania {TTCL}  kuendelea na mipango yao mengine ya kusaidia huduma za Kijamii na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari  kuongeza nguvu katika kuona miradi hiyo inafanikiwa vyema.
Alisema TTCL ni Kampuni ya Kizalendo iliyoundwa  kwa lengo la kutoa huduma bora kwa  Wananchi  kurahisishia  kupata Mawasiliano ya uhakika yatakayoongeza chachu ya maendeleo yao ya kila siku.
Mapema Meneja wa Kampuni ya Simu Tanzania kwa upande wa Pemba Nd. Khamis Ishaq Ngwali alisema Ujenzi wa ukuta huo wa kuzuia Mmong’onyoko wa Ardhi umekuja kufuatia mvua kubwa za Mwaka jana zilizoathiri eneo hilo.
Nd. Ishaq alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Uongozi wa TTCL kupitia Bodi ya Kampuni hiyo ulifikia hatua ya kujenga ukuta huo ili kunusuru uharibikaji wa mazingira katika eneo hilo lililozunguukwa na Majengo ya huduma.
Alisema kutokana na mazingira halisi ya eneo hilo lilivyo likiwa na Mlima TTCL ina malengo ya kuendelea na ujenzi wa ukuta huo kwa awamu Mbili zijazo ili kupafanya pawe salama mahali hapo.
Meneja huyo wa TTCL Pemba alifahamisha kwamba jumla ya Shilingi Milioni 39,344,000,000/- zimetumika katika ujenzi wa ukuta huo uliotumia Mawe na Waya lakini gharama hizo zingepanda zaidi iwapo wangeamua kutumia ujenzi wa zege.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.