Habari za Punde

Vijana Wanaohitimu Vyuo Watakiwa Kuzitumia Fedha Vizuri Zinazotengwa na Halmashauri Kujiongezea Kipato.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Khatib Kazungu (wa pili kushoto), akiwa katika maandamano wakati wa mahafali ya 32 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) Kanda ya Ziwa Jijini Mwanza, ambapo wahitimu zaidi ya 1200 walitunukiwa vyeti vya ngazi ya Astashahada, Stashahada na Stashahada za Uzamili.
Kaimu Mkuu wa Chuo Cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP), Prof. Hozen Mayaya, akiishukuru Serikali kwa kuboresha Sekta ya huduma za jamii wakati wa mahafali ya 32 ya Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini (IRDP) Kanda ya Ziwa Jijini Mwanza ikiwa ni mahafali ya sita kufanyika katika Chuo hicho.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Khatib Kazungu, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali ya 32 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) Kanda ya Ziwa Jijini Mwanza, akiwataka wahitimu hao (hawapo pichani) kuchangamkia fursa zilizopo katika  mtengamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kupata ajira kwa kuwa wanavigezo vya ushindani wa ndani na nje ya nchi.
Wahitimu wa ngazi ya Stashahada za Uzamili wakiwa tayari kutunukiwa vyeti wakati wa mahafali ya 32 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) Kanda ya Ziwa Jijini Mwanza.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Khatib Kazungu, akimtunuku mmoja wa wahitimu wa ngazi ya Stashahada za Uzamili wakati wa mahafali ya 32 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) Kanda ya Ziwa Jijini Mwanza.
Baadhi ya wahitimu wa stashahada wakipunga kofia kwa furaha baada ya kutunukiwa vyeti vya kuhitimu wakati wa mahafali ya 32 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) Kanda ya Ziwa Jijini Mwanza.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Khatib Kazungu (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi na wahitimu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) Kanda ya Ziwa Jijini Mwanza.

(Picha na Josephine Majura, Wizara ya Fedha na Mipango)
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Khatib Kazungu (wa pili kushoto),  akitembelea moja ya banda la maonesho ya wajasiriamali waliopata mafunzo katika Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) Kanda ya Ziwa Jijini Mwanza kabla ya kuwatunuku vyeti wahitimu wa Chuo hicho.
(Picha na Josephine Majura, Wizara ya Fedha na Mipango)

Na. Josephine Majura na Peter Haule WFM- Mwanza
Serikali imewataka wahitimu wa vyuo mbalimbali nchini kuhakikisha wanatumia fursa ya uwepo wa fedha zinazotengwa na Halmashauri katika Wilaya zote nchini kila mwaka kwa ajili ya kuwawezesha vijana na wanawake kiuchumi.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Khatibu Kazungu, kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Philip Isdor Mpango, wakati wa Mahafali ya 32 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) Kanda ya Ziwa Jijini Mwanza.
Dkt. Kazungu alisema kuwa, Halmashauri zote nchini hutenga asilimia tano ya mapato yake ya ndani kila mwaka ili kuwawezesha vijana na wanawake kutumia fedha hizo kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo na kuwataka wahitimu wa vyuo ambao hawana ajira katika Sekta rasmi, waanzishe vikundi vya umoja wa uzalishaji mali ikiwa ni moja ya kigezo cha kuweza kupata fedha hizo.
“Serikali ya Awamu ya Tano imejidhatiti kuwaletea wananchi maendeleo endelevu kwa kuhakikisha kila mtu kwa nafasi yake anafanya kazi uzalendo, uadilifu,  bidii na maarifa lakini pia kudumisha amani na mshikamano ili kuwa na maendeleo endelevu kwa manufaa ya kizazi hiki na  kijacho.”alisema Dkt. Kazungu.
Aidha aliwataka Wahitimu hao kuchangamkia fursa ya mtengamano wa Afrika Mashariki kwa kupata ajira si tu ndani ya nchi na hata nje ya nchi kwa kuwa Wahitimu hao wamebahatika kuwa na elimu yenye ubora inayoweza kuingia katika ushindani ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo Cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP), Prof. Hozen Mayaya, ameishukuru Serikali kwa kufanya maboresho katika sekta ya Huduma za Jamii ikiwemo elimu ambayo imewezesha Taasisi  za Elimu ya Juu kuwa sehemu bora ya kujifunzia.
Alisema kuwa tangu kuanzishwa kwa chuo hicho miaka 39 iliyopita, hakijaacha kusimamia ubora wa elimu kwa kuzingatiaa miongozo na kanuni zilizowekwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE).
Mkurugenzi wa Chuo cha IRDP Kanda ya Ziwa Dkt. Benedict Kilobe, alisema kuwa Mahafali hayo yamefanyika kwa mara ya sita katika kituo cha Mwanza, ambapo jumla ya wanafunzi 1,203 wamehitimu mafunzo ya programu mbalimbali zinazotolewa na chuo hicho wakiwemo Wanaume 519 sawa na asilimia 43.1 na Wanawake 684 sawa na asilimia 56.9.
Mahafali ya 32 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) Kanda ya Ziwa Jijini Mwanza yalihusisha Wahitimu wa ngazi ya Astashahada, Stashahada na Stashahada za Uzamili ambao walipata mafunzo kwa vitendo katika maeneo mbalimbali nchini ambayo yatawafanya kuwa chachu ya mabadiliko katika vituo vya kazi.
Naye Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo, Bi. Mugage Mtani, amesema mafanikio ya chuo hicho yametokana na ushirikiano wa wadau mbalimbali ikiwa pamoja na Serikali Kuu, Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Asasi zisizo za Serikali, Taasisi za Mafunzo ndani na nje ya nchi na Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) - Malawi na Tanzania.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango amewapongeza wahitimu  wote wa chuo hicho kwa kusoma kwa bidii na hatimae kutunukiwa vyeti na kuwataka wanaoendelea na masomo chuoni hapo kuiga mfano mzuri uliooneshwa na watangulizi wao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.