Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi.Uwepo wa Chuo Kikuu Huria Hutoa Matumaini Kwa Mtoto wa Kitanzania.

Wahitimu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania {Open University} wakiwa katika  Gwaride Maalum  wakiingia katika Uwanja wa Mahafali  yao ya 35 yaliyoshirikisha katika wale wa Kiwango cha Shahada, Stashahada na Astashahada  yaliyofanyika hapo Bungo Kibaha Mkoa wa Pwani.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Rizirki Pembe Juma kwa Niaba ya Pacha mwenzake Waziri wa Elimu Sayansi wa Tanzania akitoa salamu kwenye Mahafali ya 35 ya Chuo Kikuu huria Tanzania.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwahutubia Wahitimu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania hapo Bungo Kibaha Mkoa wa Pwani.
Wahitimu wa Shahada ya Uzamivu ya Udaktari wa Falsafa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania wakitafakari baada ya kutawadhwa rasmi ufaulku wao wa Udokta.
Baadhi ya Wahitimu mbali mbali wa Shahada, Stashahada na Astashahada wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania wakifuatilia matukio mbali mbali yaliyojitokeza wakati wa Mahafali yao.
Baadhi ya Wahitimu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kutoka Visiwani Zanzibar wakitafakari mambo mbali mbali baada ya kumaliza mafunzo yao ya ngazi mbali mbali katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ambae pia Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mh. Mizengo Kayanda Peter Pinda akimpongeza Mbunge wa Jimbo la Welezo Mheshimiwa Saada Mkuya Salum baada ya kupokea Shahada ya Uzamivu ya Udaktari wa Falsafa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis.OMPR. 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameushauri Uongozi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kutumia Programu za kutayarisha Walimu Tarajali watakaowaandaa Wanafunzi wa Skuli za Msingi na Sekondari kuwa na Stadi na maadili ya kujiendeleza kupitia mfumo wa Elimu Huria na Masafa.
Alisema uwepo wa Chuo hicho  unaendelea kutoa matumaini kwa Mtoto wa Kitanzania anayeanza Darasa la kwanza kuwa na uhakika wa kupata Elimu hadi ngazi ya Chuo Kikuu ikiwa na maana halisi ya Elimu endelevu kama haki ya Binaadamu.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa ushauri huo wakati akiwahutubia Wahitimu wa Mahafali ya 35 wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania {Open University} yaliyofanyika hapo Bungo Kibaha Mkoa wa Pwani.
Alisema Elimu Huria na Masafa inajitanabahisha kama Mfumo wa kisasa na mahiri katika kutoa Elimu na mafunzo yenye ubora unaokubalika  na kutambulika Kitaifa, Kikanda na Kimataifa ukizingatia taratibu na kukidhi Vigezo vya ithibati vya Mamlaka husika.
Balozi Seif aliukumbusha Uongozi wa Chuo hicho kwamba katika jitihada zake za kutekeleza majukumu yake ni vyema ukaendelea kujikita katika kauli mbiu isemayo elimu bora na nafuu kwa wote kwa mujibu wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014.
Alieleza kwamba Kanuni za Chuo hicho katika masuala ya Udahili, kufundisha, kujisomea pamoja na kutathmini Maendeleo ya Wanafunzi ni fursa pekee itakayoweza kuisaidia Taifa kuongeza kiwango cha Udahili kwa Wananchi wake katika Elimu ya juu.
Balozi Seif alisema kwa mujibu wa Takwimu za Benki ya Dunia, Uchumi wa Kati na wa Viwanda hauwezi kufikiwa au kuwa endelevu pasipo kuwa na kiwango cha udahili katika Elimu ya juu cha angalau kufikia asilimia 23%.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema kiwango cha Tanzania kama zilivyo Nchi za Burundi na Madagaska hivi sasa kimefikia asilimia 4%  kikiwa chini kutokana na sababu zilizobainishwa kwenye Sera ya Elimu na Mafunzo 2014.
Balozi Seif  alisema huo ndio mfumo ambao unahitaji kuhuishwa na Mfumo wa Elimu huria na masafa ili Elimu ifikie kuwa  Haki ya Msingi ya kila Mwananchi kama ilivyo haki nyengine zote za Binaadamu.
Alisema Serikali imekusudia kuleta Mapinduzi ya Kiuchumi ili kuibadili Tanzania iwe Nchi ya Uchumi wa kati ifikapo Mwaka 2025, mbapo Sekta ya Elimu na mafunzo kwa mujibu wa Dira ya Maendeleoya Taifa na Mpango wa muda mrefu wa Maendeleo inatarajiwa kuleta Maendeleo ya haraka.
Alifahamisha kwa kutambua kuwa Elimu ni haki ya Msingi ya Binaadamu Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imeamua kubeba wajibu wa kutoa Elimu ya Msingi na Sekondari biya ya malipo kwa Watoto wote waliofikia umri wa kwenda Skuli, uamuzi ambao pia umefanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Balozi Seif  ameunga mkono rai iliyotolewa na Uongozi wa Chuo Kikuu Huria Tanzania kuwa mamlaka  husika hususan Wizara ya Elimu, Tume ya Vyuo Vikuu, Baraza la Elimu na Ufundi pamoja na Chuo Kikuu Huria Tanzania zishirikiane katika kubuni taratibu zitakazotekeleza azma ya Serikali kama ilivyoainishwa ndani ya Sera ya Elimu.
Alielezea matumaini yake kwamba Chuo hicho kitaendelea kuwa chemchem ya Elimu inayotiririka kila pembe ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na kunufaisha pamoja na kukinaisha Watanzania wengi zaidi.
Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kukipatia eneo la ujenzi wa Ofisi Chuo hicho ili kijenge Kituo chake cha Pili kwa ukubwa Nchini Tanzania Jamii ikiamini kuwa uwepo wao Zanzibar utasaidia kudumisha Muungano.
Akizungumzia suala la Wahitimu Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema ni vyema kwa Vyuo Vikuu vya Tanzania kuunda Jumuiya ya Wahitimu { Alumni Associations} zenye nguvu ili kupata nafasi ya kuwashirikisha Wahitimu kwenye Maendeleo ya Vyuo vyao.
Alisema maendeleo ya Vyuo Vikuu vingi mashuhuri Duniani yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na Wahitimu wake ambao wengine hunyookewa kimaisha na kuwa Matajiri wakubwa katika Jamii zinazowazunguuka.
“ Wengi wetu hapa kwenye Meza kubwa tumesoma kwenye Vyuo vya hapa Nchini lakini sifikirii kama Vyuo vyenyewe vina habari na sisi”. Alisema Balozi Seif.
Aliwaomba Watitimu wote waliopata elimu Chuo hicho kusaidia kuchangia maendeleo yake kwa njia tofauti ikiwemo mawazo, ubunifu, ufadhili kwa Wanafunzi maskini pamoja na kufadhili tafiti mbali mbali za Chuo.
Akitoa Taarifa ya Chuo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Profesa Elifas Tozo Bisanda alisema utumiaji wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano {TEHAMA} katika ufundishaji umewezesha kupatikana kwa ongezeko kubwa la Vituo vya Mitihani  33 katika maeneo yote Tanzania Bara na Zanzibar.
Profesa Elifas alisema ongezeko hilo la Vituo vha Mitihani limesaidia kuibua Wataalamu wengi waliohamasiska kupata Taaluma zaidi ya Elimu Huria na Msafa kwenye chuo hicho kinachofikia Miaka 25 sasa tokea kuasisiwa kwake Mnamo Mwaka 1994.
Alisema Jumla ya Wahitimu Elfu 3,053 wa ngazi ya Shahada, Stashahada na Astashahada wamefanikiwa kukamilisha mafunzo yao mwaka huu na kuifanya idadi ya Wahitimu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kufikia 39,934 toke kuanzishwa kwake.
Alisema inapendeleza kuona wanafunzi wa Chuo hicho kwa sawa wanatoka sehemu mbali mbali za Dunia hasa katika Mataifa ya Bara la Afrika hali iliyokifanya Chuo hicho kuimarisha vituo vya nje kaika Nchi za Kenya, Namibia, Zambia, Ghana na mazungumzo yanaendelea kufungua Kituo chengine Nchini Ethiopia.
Mapema akitoa salamu za Uongozi wa Chuo Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Profesa Rwekaza Makandala alisema Chuo hicho kimelenga kuwa na Maabara ya Tafiti zote ili kiwe sehemu ya Taifa ya Mabadiliko ya Uchumi.
Profesa Ujenzi huo wa Mabara unakwenda sambamba na Mpango Mkakati ulioanza Mwaka 2018-2019 na 2020 – 2022 unaokusudia kujenga uwezo wa Kitaaluma kwa Mwanafunzi popote alipo kwenye Kituo chake.
Mwenyekiti huyo wa Baraza la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania alizishukuru na kuzipongeza Serikali zote mbili Nchini Tanzania kwa kusimamia Mikakati inayochangia Maendeleo ya Chuo hicho Huria Nchini.
Akimkaribisha Mgeni rasmi kuzungumza na Wahitimu hao Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh.Riziki Pembe Juma kwa Niaba ya Waziri pacha mwenzake wa Elimu Sayansi na Teknolojia wa Tanzania alisema Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kimesaidia kujenga uwezo wa kukidhi mahitaji ya Serikali.
Mh. Riziki alisema Serikali zote mbili Tanzania ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi ya Zanzibar zinathamini Mchango wa Chuo hicho kwa kuimarisha Sekta ya Elimu Nchini.
Waziri Riziki Pembe alisisitiza kwamba kusudi la Serikali ni kukiwezesha Chuo hicho kuwa mfano Bora wa Chemchem ya Elimu kwa kukisaidia kuunganisha Vituo vyote vya Mitihani kutumia Mkonga wa Taifa Mawasiliano ili kupunguza Gharama pamoja na kuwajengea uwezo zaidi wa Kitaaluma Wanafunzi wake.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.